Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya akizungumza wakatia wa kikao cha wadau wa chai kilichongozwa na Waziri Mkuu leo mjini Njombe ambapo amesema waizara itaendelea kutatua changamoto za wakulima kupitia vikao vya majadiliano .
Baadhi ya Washiriki wa Mkutano wa Wadau wa Tasnia ya Chai Tanzania wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipoongoza Mkutano wao kwenye ukumbi wa Johnson, Njombe, Machi 10, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda akizungumza wakati wa kikao cha wadau wa zao la chai ambapo amesema katika bajeti ya 2021/22 maafisa ugani watapatiwa mafunzo ma vifaa wasimamie kuongeza tija na uzalishaji wa mazao nchini.
Serikali imeziagiza halmashauri zote zinazolima zao la chai nchini kuanzisha vitalu vya miche ya chai na kugawa bure kwa wakulima ili kuinua uzalishaji wa zao hilo nchini.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa agizo hilo leo (10.03.2021) wakati akifunga kikao cha wadau wa zao la chai kilichofanyika mkoani Njombe kujadili mwenendo wa uzalishaji wa zao hilo muhimu ambalo kuanzia mwaka 2018 uzalishaji wake umeonekana kudorora.
“Kila halmashauri ianzishe kitalu cha ekari tatu na kuotesha miche bora ya chao kisha igawiwe bure kwa wananchi wapande. Kazi hii ifanyike kwa kutumia fedha za mapato ya ndani ya halmashauri” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Zao la chai kwa hivi sasa linalimwa katika Wilaya 12 zilizopo kwenye mikoa sita ambayo ni Mbeya, Njombe, Iringa, Tanga, Kagera na Kilimanjaro. Jumla ya eneo lililopandwa chai ni hekta 22,721 ambapo wakulima wakubwa wana hekta 11,272 na wakulima wadogo hekta 11,449.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu ametoa siku tatu kwa wamiliki wa kampuni ya DL inayomiliki viwanda vya chai Ikanga, Luponde na Itona kuwalipa wakulima wadogo wa chai madai yao ya fedha kufuatia kuuza majani mabichi ya chai kwa muda mrefu .
“Natoa siku tatu kwa kampuni ya DL itoe maelezo kwanini haijalipa wakulima wadogo wa chai kwa kipindi kirefu wakati inaendelea na kazi ya kuzalisha chai” alisema Waziri Mkuu Majaliwa na kuongeza kuwa serikali inataka kuona wawekezaji makini ili wakulima wanufaike na kazi zao
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa pia maagizo kwa wizara ya kilimo kuhakikisha inakuwa na utaratibu wa kukutana na wadau wa mazao ya kilimo kusikiliza kero ,changamoto na kutafuta suluhisho la pamoja ili sekta ya kilimo itoe mchango mkubwa zaidi
Pia ameagiza wizara ya Kilimo kusimamia uanzishwaji wa vyama vikuu vya ushirika kwenye maeneo yanayolima zao la chai nchini ikiwemo kuwa na Viongozi waadilifu na wenye uwezo wa kukuza sekta ya ushirika uwe na manufaa kwa wakulima.
Ili kuhakikisha nchi inakuwa na viwanda vingi vya kuchakata chai Waziri Mkuu Majaliwa ameitaka wizara ya Kilimo kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara kuvutia uwekezaji kwenye uanzishwaji viwanda vidogo, vya kati na vikubwa vya kuchakata majani mabichi ya chai hali itakayosaidia wakulima kupata uhakika wa masoko.
Kuhusu upatikanaji wa miche bora ya chai Waziri Mkuu amegiza Bodi ya Chai Tanzania na Taasisi ya Utafiti wa zao la Chai (TRIT) kuhakikisha inafikisha miche ya kutosha na pia viuatilifu kwa wakulima ili tija na ubora wa chai inayozalishwa iongezeke na kuleta faida kwa wakulima Taifa kupata uhakika wa pato.
Naye Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda alisema wizara yake iko kwenye mapitio ya kuhakikisha maafisa ugani nchini wanajengewa uwezo wa kusimamia shuguli za kilimo vijijini ambapo kwa kuanzia katika bajeti ijayo itatenge fedha kugharimia mafunzo,ununuzi wa vifaa na vitendea kazi ili kuinua ari ya usimamizi wa kilimo kiwe chenye tija zaidi.
Kwa upande wake Naibu Waziri Nishati Stephen Byabato akizungumza kwenye kikao cha wadu wa chai ametoa wito kwa wawekezaji kuanzisha viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo kwani upatikanaji wa umeme ni wa uhakika.
“Tunao umeme wa kutosha ambapo kwa Njombe sasa tuna megawati 62.4 wakati matumizi kwa siku yamefikia wastani wa megawati 12.3 hivyo umeme ni wakutosha ,wawekezaji jengeni viwanda vya kutosha kuchakata chai na mazao mengine ya kilimo” alisema Naibu Waziri huyo wa Nishati.
By Mpekuzi
Post a Comment