Na Amiri Kilagalila,Njombe
Ili kukuza sekta ya kilimo hususani kwa wakulima wa viazi na matunda ya parachichi mkoani Njombe,shirika la lisilo la kiserikali la Mwamvuli wa matumaini (Highland hope Umbrella-HHU) wameishauri serikali kudhibiti mfumo wa utumiaji wa madalali wanaosababisha anguko la kibiashara kwa wakulima wa mazao hayo.
Hayo yamebainishwa na mkurugenzi shirika la Mwamvuli wa matumaini Bi,Bethseba Liduke wakati akitoa wasilisho lake katika mdahalo wa pamoja na wakulima wa tarafa ya Igominyi kuhusu kutoka kilimo cha Mazoea na kuelekea kwenye kilimo bora uliofanyika mjini Njombe.
“Mikoa mingi kwa sasa imetoka kwenye kupima mazao kwa ujazo na wanapima mazao kwa kutumia kilo (KG) niombe halmashauri ya mji na sisi tubadirike tutoe maamuzi kwamba chakula chochote au mazao yoyote yapimwe kwa kilo ili wananchi na wakulima wafaidike”alisema Bi,Liduke
Kuhusu walanguzi amesema “Mimi ninashangaa sehemu kubwa unakuta kuna walanguzi lakini ukienda nchi nyingine hawa watu wa kati wanaoitwa madalali hawapo kwasababu kila mkoa kila wilaya inakuwa na kituo cha kuweka na kuuza mazao yao kwa bei elekezi.Tunahitaji kama halmashauri tukwa na hivi vituo vya kuuzia mazao na kwa bei elekezi kwasababu tukiendelea kutumia madalali tutaendelea kuumia”alisema Liduke
Aliongeza kuwa “Ninaiomba halmashauri hili tunaliweza tukiamua tunaweza na tutawasaidia wakulima wetu na mapato ya halmashauri yatapanda kwasababu hela kubwa inaenda kwa madalali”aliongeza
Nolasco Kilumile ni afisa wa mazao kutoka halmashauri ya mji wa Njombe (HQ),amesema serikali inatambua changamoto hizo kwa wakulima na inaendelea kushughulika changamoto zote huku akiwataka wakulima kutambua serikali imeweka utaratibu wa uhakiki wa wanunuzi kabla ya kuingia kwa wakulima.
“tulishawaelekeza wataalmu pamoja na wadau mbali mbali kwamba kama mnunuzi amefika kijijini lazima aripoti kwenye ofisi za mtendaji wa kijiji ama ofisi za kata lakini pia lazima afahamike katika ofisi za kitongoji mahala wanapovuna mazao na kama uongozi wa kijiji unakuwa hauna taarifa hapo kuna kuwa kuna shida”alisema Kilumile
Kwa upande wake mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Njombe Stanley Mayemba,amesema baadhi ya changamoto ikiwemo Lumbesa kwa wakulima wa viazi inayosababishwa na mlipuko wa madalali kwa muda mrefu ilishaanza kutatuliwa mpaka kwenye ngazi ya kitaifa.
“Hii haiwezi kutatuliwa na mkoa wa Njombe peke yake ni lazima libebwe kama tatizo la kitaifa na kwenye mkutano wetu wa RCC tulishawaagiza wabunge wetu kwenda kulijadili kitaifa kwasababu huwezi Njombe kuzuia Lumbesa wakati Mbeya labda wanasafirisha kwa Lumbesa na soko letu ni moja lakini pia kwenye zao la parachichi tunafika huko kwasababu ya soko holela ”alisema Mayemba Awali wakulima katika mdahalo huo waliisisitiza serikali kudhibiti changamoto hiyo kutokana na hasara ambazo wamekuwa wakizipata mara kwa mara katika mazao hususani ya viazi na parachichi.
By Mpekuzi
Post a Comment