Na Said Mwishehe, Michuzi TV
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) naomba kabla ya kuendelea na maelezo yangu ambayo nimekusudia kuyaelezea hapa , nianze kuwapongeza kwa kazi kubwa na nzuri ambayo mmekuwa mkiifanya katika eneo la sekta ya nishati ya umeme kwa kuhakikisha unapatikana wakati wote.
Binafsi kutoka moyoni, nikiri nimeendelea kutambua mchango wa TANESCO katika kuendelea kuboresha huduma ya nishati ya umeme nchini kwetu. Sina shaka na kazi wanayoifanya na katika hili sitaki kupepesa macho...TANESCO mnafanya kazi nzuri.
Siyo kwamba sitambui changamoto ambazo wakati mwingine zinatokea zikiwemo za kukatika kwa umeme kwa nyakati tofauti katika maeneo ya nchi yetu. Kwanza lazima tukubaliane umeme utakatika na sababu zipo lakini haukatiki kwasababu ya kutotosha, sio kweli , tunao umeme mwingi tu.Unabisha?
Unaweza kuuliza kama upo mwingi kwanini unakatika? Jibu ni kwamba unakatika na sababu ni nyingi lakini kubwa sote tunafahamu TANESCO ni shirika la umma la muda mrefu na ujenzi wa miundombinu ya umeme iliyopo mingi ni ya muda mrefu, hivyo kuna maeneo imechoka na kusababisha umeme kukatika.
Sababu ya pili inayosababisha umeme kukatika hutokana na maboresho ambayo yanaendelea kufanywa na TANESCO kwa mfano, wanapoamua kubalisha nguzo au waya lazima eneo husika litazimwa umeme, ili watalaamu waendeleee na maboresho.
Sababu ya tatu ni ile inayotokana na baadhi ya watu kuharibu miundombinu ya umeme, tena kwa makusudi kabisa. Ndio? Unashangaa nini? Hebu pata picha mtu anaamua kuchoma nguzo kisa tu anaandaa shamba.Ndivyo hivyo ndugu zangu.Ukikutana na watalaam wa TANESCO wataeleza vizuri kwani shida iko wapi.
Hata hivyo TANESCO kwa kutambua wajibu wake na umuhimu wake limeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha umeme unapatikana wakati wote. Muda wote wako kazini, wanawajibika kwa maslahi mapana ya nchi yao.
Nikiwapongeza TANESCO naamini niko sahihi, sina sababu ya kuwalaumu muda wote. Kwanza nyakati za kulalamika zimekwisha ,nyakati hizi za Serikali ya Awamu ya Tano zimekwenda mbele , zinapambana na utatuzi wa changamoto.Hakuna muda wa kulalamika tena.
TANESCO wamekuwa wawazi kwa kila ambacho wanakifanya, wakiboresha miundombinu wanatoa taarifa, wakiwa na jambo lolote wamekuwa wapesi wa kuulezea umma wa Watanzania.Hata wakitaka kukata umeme wanatoa taarifa na zinafika.Katibu Mkuu Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Dk.Hassan Abas anawapongeza TANESCO kwa kuwa wepesi wa kutoa taarifa ,amewapongeza kwa hilo.
Weka akili Dk.Abass ndio Msemaji Mkuu wa Serikali,hivyo anapotoa pongezi kwa TANESCO kutokana na uharaka wake wa kutoa taarifa ni jambo la kuleta faraja.Hongereni, na sitaki kujisahaulisha Meneja Uhusiano wa shirika hilo Johari Kachwamba na wasaidizi wako kwenye idara ya mawasiliano mnafanya kazi nzuri,timizeni wajibu wa kikatiba wa kuhakikisha umma unapata habari sahihi na kwa wakati.
Kunapokuwa na changamoto yoyote wamekuwa wepesi wa kutoa maelezo bila kuchelewa. Kwa mazingira ya aina hii kwanini nisiwapongeze.Aka mwaya... hongereni TANESCO.
Halafu ngoja nikwambia kitu, siku tatu zilizopita nimemsikia kwa masikio yangu Mkurugezi Mkuu wa TANESCO Dk.Tito Mwinuka wakati anaelezea mipango, mikakati na malengo ya shirika hilo wakati anazungumza na wahariri wa vyombo vya habari nchini waliokuwa kwenye kikao kazi kilichofanyika Mjini Morogoro.
Dk.Mwinuka ameeleza mengi kuhusu shirika hilo amewaaleza wahariri jinsi ambavyo wamedhamiria kuboresha upatikanaji wa huduma ya umeme nchini.Hakusita kuelezea kila kitu kwa wahariri hao.Unajua kwanini?
TANASCO wanaamini wahariri ni daraja imara la kufikisha taarifa sahihi za shirika hilo kwa wananchi.Kama unabisha fanya kama unajikuna kwa sauti ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora mzee wangu Agrey Mwanri.
Nimechoka bwana nimemmisi mzee wangu, uko aliko namtakia maisha mema na yenye afya tele.
Ngoja niendelee na ujumbe wa Dk.Mwinuka kwa wahariri,alipokuwa akizungumza nao nakumbuka aliwaambia hivi "Napenda kukutarifu kua kikao kazi hichi kinajumuisha Wahariri Waandamizi takribani 33 wa vyombo vya Habari Tanzania ambao ni wadau muhimu katika sekta ya Nishati.
Kama tunavyojua TANESCO ni Shirika la umma lenye jukumu kubwa la kuleta mabadilika kwa jamii za watanzania mijini na vijijini kwa kuwapatia nishati ya umeme ya uhakika na kwa bei nafuu.
"Katika kufanikisha hilo, Shirika limekuwa likitekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati itakayo saidia kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika na ustawi endelevu wa uchumi wa Nchi yetu. Katika uzalishaji Umeme, Serikali kupitia TANESCO inatekeleza mradi mkubwa wa kufua umeme wa maji wenye uwezo wa Megawati 2115 wa Julius Nyerere utakaogharimu kiasi cha shilingi Trilioni 6.5 fedha za watanzania.
"Pia tuna miradi kama vile Rusumo (MW 87) ambapo hadi sasa utekezwaji wake umefikia asilimia 76.8 na utagarimu kiasi cha shilingi billioni 263.Hata hivyo Serikali kupitia TANESCO, inatarajia kutaekeza miradi mingine mikubwa kama vile Ruhuji 358 MW, Rumakali 222MW, Mtwara MW 300, Somanga fungu MW 300, Kakono MW 87, Malagarasi 45 MW.
"Kupitia utekelezaji huu wa Miradi hii ya uzalishaji umeme, tunategemea hadi kufikia 2025 TANESCO kuwa na uwezo wakuzalisha Megawati 5,000. Hii itasidia Nchi kuwa na umeme wa kujitosheleza na utakaochochea ukuwaji wa uchumi na kuuza ziada itakayobakia nje ya Nchi. Hata hivyo, Shirika linatekeleza miradi mbalimbali ya kusafirisha umeme Nchini kama vile, 400Kv Kenya -Tanzania Interconnector, 400Kv Tanzania – Zambia Interconnector, 400Kv Julius Nyerere hadi Chalinze na 400kV Kigoma – Nyakanazi.
"Miradi hiyo yote itasaidia kusafirisha na kuimarisha hali ya umeme katika gridi ya Taifa nchini pamoja na kuwezesha biashara ya kuuziana umeme baina ya Nchi majirani. Shirika pia ina tekeleza miradi mbalimbali ya usambazaji umeme katika Mikoa, vijijini na Mijini.
"Ujenzi wa Njia ya Kusafirisha Umeme utakaotumika katika treni ya SGR Awamu ya Kwanza (Lot I) nao umekamilika kwa asilimia 100. Wahariri pia wakiwa njiani kutoka Dar es salaam wametembelea na kujionea miundombinu ya umeme utakaoendesha Treni za umeme".
Dk.Mwinuka hakuishia hapo akaedelea kuwaeleza wahariri hao kwamba kwasasa uwezo wa TANESCO kuzalisha umeme ni 1,602.04 MW wakati mahitaji halisi ,ya wateja ni 1,180.53MW."Hivyo mtaona tuna ziada ya takribani 520.51MW. Hii inamanisha umeme upo wakutosha wananchi na wawekezaji wanatakiwa kuchangamkia fursa hii ya umeme kuanzisha na kuendeleza shughuli mbalimbali za uzalishaji mali.Takribani asilimia 87 ya watazania wameweza kufikwa na huduma ya umeme hivi sasa".
Hayo ndiyo ambayo Dk.Mwinuka aliyaelezea tena hatua kwa hatua huku akuwa makini kuhakikisha anachokielezea kinakwenda kukaa kwenye vichwa vya wahariri na kisha ujumbe unaokwenda kwa umma uwe wenye tija, wenye kueleweka na kubwa zaidi utakaotoa matumaini kwa Watanzania kuhusu nishati ya umeme.
Dk.Mwinuka katika kuelezea miradi ya TANESCO alianza na ule mradi mkubwa wa Julius Nyerere ambao utakapokamilika utakuwa na kuzalisha umeme megawati 2115. Ni umeme mwingi sana utakaozalishwa kutoka kwenye mradi huo.
Hakika TANESCO mnastahili pongezi kwa kazi ambayo mnaifanya katika kuusimamia mradi huo wa kimkakati.Ni mradi mkubwa , ni mradi ambao unatokana na dhamira njema ya Rais Dk.John Magufuli, aliamua kutoa msimamo kuhusu mradi huo hasa bada ya kuona kuna baadhi ya mataifa yanataka kukwamisha.
Hakika Rais Dk.Magufuli kwenye mradi huo umeandika historia ambayo haitafutika katika nchi ya Tanzania, ni mradi mkubwa sana, ni mradi wenye kuileta nchi sifa na heshima .Nchi itapata sifa kwasababu ya ukubwa wa mradi wenyewe, umeme utakaotoka hapo utaifanya nchi yetu kuwa na umeme wa uhakika.Tutawauzia hadi nchi jirani.Nchi itakuwa na heshima kwasababu tunakwenda kuondokana na kukatika kwa umeme.
Tutakuwa mbali zaidi katika eneo la nishati ya umeme ukilinganisha na nchi nyingine hasa hizi ambazo ni majirani zetu.Namshukuru Mungu nimebahatika kufika kwenye mradi wa bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere.Ukifika kwenye mradi huo ndio utajua ukubwa wa kazi inayofanyika, hakika ni mradi mkubwa sana tena sana.
Nikiwa eneo la mradi niliwaza mambo mengi sana , lakini kubwa zaidi akili yangu ikajikita katika kumfikiria Rais Dk.John Magufuli, nilimfikiria zaidi ya mara 100, kwanza kwa uthubutu wake na pili kwa maono yake kwa Taifa letu la Tanzania.
Nafahamu bwawa hilo lilianza kuzungumzwa tangu enzi za Baba wa Taifa, na katika kipindi chota hakuna kilichofanyika, lakini Rais Magufuli kupitia Serikali anayoingoza akasema hapana, hili bwawa lazima lizalishe umeme.Kazi inaendelea.
Huko uliko Rais Magufuli kuwa na amani ya moyo, umefanya kazi inayoonekana katika nchi yetu, jukumu langu na Watanzania wengine tutaendelea kukuomba kwa Mungu azidi kukupa afya njema na maisha marefu.Haya unayofanya katika nchi yetu hatuna cha kukulipa zaidi ya kusema Ahsante Rais Magufuli, ahsante baba kwa moyo wako wa uzalendo.
Ni kupitia wewe tunashuhudia hata TANESCO wakijiendesha bila kutegemea ruzuku ya Serikali.Tunafahamu TANESCO ilifikia hatua likawa linashindwa kujiendesha lakini Rais Magufuli ukatoa muelekeo wa shirika hilo na kisha ukampa majukumu Dk.Mwinuka aongeze watumishi wengine kuhakikisha mambo yanakwenda.Na kweli yanakwenda,tunayaona, tunasikia.
Kinachoendelea mradi wa Julius Nyerere ni matunda ya maono yako na TANESCO wanayatekeleza maono hayo kwa vitendo.Wanapiga kazi usiku na mchana, nimekwenda katika mradi huo nimeona kwa macho yangu, watu hawalali , kasi ya ujenzi ni kubwa.
Sishangai Waziri wa Nishati Dk.Medard Kelamani anavyosisitiza kwamba Ifikapo Juni mwaka 2022 mradi huo utakuwa umekamilika.Usisahau mradi huo utakapokamilika utazalisha megawati 2115, usiseme sijakwambia, nilieleza mwanzoni na sasa narudia tena. Ujue nina kila sababu ya kuwapongeza TANESCO , hakika kazi wanayoifanya kwa niaba ya Watanzania ni kubwa , inastahili pongezi.
Narudia tena ni hivi kuhusu ninyi TANESCO acha niwaambie ukweli kabisa...nimeshindwa kusubiri, tambueni mnafanya kazi nzuri sana. Najua wako watakaobeza kazi yenu lakini hiyo ndio kawaida ya watu, hamna sababu ya kurudi nyuma, songeni mbele kwa maslahi mapana ya taifa letu.
INATOSHA kwa leo , uwe na siku njema.Sitaki kukuchosha na nikumbe tuendelee kuchukua tahadhari kuhusu Corona lakini tuache kutishana na kutiana hofu.
Tuwasiliane;0713833822
By Mpekuzi
Post a Comment