Na Woinde Shizza ,Michuzi - Tv
SERIKALI imeridhishwa na utekelezaji wa miradi ya miundo mbinu ya elimu na miradi mingine ya maendeleo katika halmashauri ya Jiji la Arusha kwani imetekelezwa kwa viwango vinavyotakiwa kulingana na fedha zilizotolewa kwa miradi husika .
Mkuu wa Wilaya ya Arusha Kenan Kihongosi ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na Madiwani wa halmashauri ya Jiji la Arusha kwenye mkutano wa robo ya Pili wa Baraza la Madiwani katika Ukumbi wa mikutano wa Mkuu wa Mkoa.
Alisema kuwa anajivunia kuona fedha za miradi zilizotolewa na Serikali ya Dk.John Pombe Magufuli zimetumika ipasavyo na miradi imekamilika kwa asilimia 95 kwamba kukamilika huko kumewezesha wanafunzi kujiunga kidato cha kwanza bila kikwazo.
Aliendelea kwa kumpongeza Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Dk. John Pima kwa kusimamia vyema fedha za Serikali na kuwezesha miradi kukamilika kwa wakati.
Pamoja na mambo mengine alisema kuwa mafanikio hayo yamepatikana kwa ushirikiano wa madiwani na wataalam na kudai kuwa Serikali inajivunia uongozi huo.
Awali Meya wa Jiji la Arusha, Maximilian Iranqhe alipongeza jitihada za Mkuu wa Wilaya ya Arusha kwa kushiriki kikamilifu katika Ujenzi wa madarasa mwaka 2020 na kwamba Kiongozi huyo ni mfano wa kuigwa.
Iranqhe alisema kuwa nia ya Viongozi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha nikuwaletea Wananchi Maendeleo na kudai kuwa Arusha itakuwa mji wa mfano kwa kuwaletea wananchi maendeleo.
By Mpekuzi
Post a Comment