Washindi wa Pikipiki za miguu mitatu aina ya Lifan Cargo wa Droo ya kwanza ya Kampeni ya Weka Pesa na Ushinde ‘Bonge la Mpango’ inayoendeshwa na Benki ya NMB, wamekabidhiwa zawadi zao hizo, huku droo ya pili ya promosheni hiyo ikiibua washindi wengine 12, wote wakitwaa zawadi zinazofikia thamani zaidi ya Sh. Mil. 23.
Hafla Kuu ya makabidhiano hayo ilifanyika NMB Tawi la Gongolamboto, ambako mkazi wa Kitunda jijini Dar es Salaam, Martha Mmasi, alikabidhiwa pikipiki yake na Meneja wa Kanda ya Dar es Salaam, Donatus Richard, huku hafla kama hiyo ikifanyika Tukuyu - Mbeya kumkabidhi mshindi mwingine.
Akizungumza kabla ya kumkabidhi Martha pikipiki yake, Donatus alibainisha kuwa NMB Bonge la Mpango, inalenga kutambua na kuthamini utamaduni chanya wa wateja kujiwekea akiba, pamoja na kurejesha kwa wateja wake sehemu ya faida ya benki hiyo ya mwaka uliopita, ambako walipata zaidi ya Sh. Bilioni 205.
“Wito wetu kwa wateja wetu, kuchangamkia zawadi tunazozitowa kupitia NMB Bonge la Mpango, ambazo ni pesa taslimu, pikipiki ya miguu mitatu kama hii aina ya Lifan, gari dogo ya mizigo aina ya Tata ‘Kirikuu’ na zawadi kuu ambayo ni gari ya kifahari aina ya Toyota Fortuner yenye thamani ya Sh. Mil. 169”.Alisema Donatus
Wateja wa NMB, wanachopaswa kufanya ni kuweka akiba katika akaunti zao kuanzia 100,000, kiasi ambacho kinaweza kuwa kianzio kwa wateja wapya, ili waweze kuwa sehemu ya wateja wanaowania zawadi ya pesa, pikipiki na Kirikuu. Pia unapaswa kuwa na akiba ya Sh. Mil. 10 ili kushindania Toyota Fortuner.
Kwa upande wake, Martha – mfanyabiashara aliyekiri kuathiriwa kibiashara na janga la virusi vya corona, lililotikisa toka mwaka jana, alisema alikua mwenye furaha isiyo na kifani kwa kuibuka mshindi wa pikipiki hiyo, licha ya kufichua kuwa ujio wa Bonge la Mpango ulimsukuma kuongeza kasi ya kuweka akiba.
“Kasi yangu ya kuweka akiba iliongezeka, nashukuru nikajikuta nashinda na kupitia pikipiki hii, ambayo nakiri kuwa nimeshinda kwa bahati yangu na sio aina yoyote ya upendeleo, biashara zangu zinaenda kupata nguvu mpya, kwani itasaidia kuniingizia kipato na kukuza uchumi wangu,” alisema Martha.
Baada ya makabidhiano hayo, droo ya pili ilichezeshwa mbele ya Mwakilishi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania, Elibariki Sengasenga, ambapo washindi 10 wa zawadi ya pesa taslimu kiasi cha Sh. Mil. 3.3 walipatikana, sambamba na washindi wengine wawili wa pikipiki aina ya Lifan Cargo ambao ni Yusuph Kyando wa Lushoto - Tanga na Rose Mgore wa Pamba Road Mwanza - jumla kuu ya thamani ya zawadi zao ikifikia Mil. 23.
Zawadi za wiki za Bonge la Mpango ni pesa taslimu na pikipiki 2 za Lifan Cargo, wakati zawadi za kila mwezi katika miezi mitatu ya kampeni hiyo ni gari dogo la mizigo aina ya 'Kirikuu' na zawadi kuu ikiwa ni Toyota Fortuner itakayotolewa mwishoni mwa kampeni hii.
Mshindi wa droo ya kwanza ya Kampeni ya NMB Bonge la Mpango Martha Mmasi akionyesha namba za usajili wa Pikipiki ya Miguu mitatu aina ya Lifan Cargo baada ya kukabidhiwa na Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Donatus Richard (wa pili kutoka kushoto) wakati wa hafla iliyofanyika katika Tawi la NMB Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Meneja wa Tawi la NMB Airport, Restus Assenga na kulia ni Meneja wa Tawi la NMB Gongo la Mboto, Demetrius Kagesha.
Mshindi wa Droo ya kwanza ya Bonge la Mpango Martha Mmasi akijaribu kuendesha Pikipiki ya Miguu mitatu aina ya Lifan Cargo baada ya kukabidhiwa na Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaan, Donatus Richard (wa pili kutoka kulia) wakati wa hafla iliyofanyika katika Tawi la NMB Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Meneja wa tawi la NMB Airport, Restus Assenga na kulia ni Meneja wa Tawi la NMB Gongo la Mboto, Demetrius Kagesha.
By Mpekuzi
Post a Comment