LEO naomba nami niandike kidogo tena kidogo sana kuhusu Dk.John Pombe Joseh Magufuli aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania .
Naandika kwasababu leo Hayati Magufuli ametiza siku 40 tangu alipofariki dunia,hakika nchi yetu bado iko kwenye giza nene ingawa kwa mapenzi ya Mungu , Watanzania tuko salama chini ya uongozi wa mama yetu mpendwa Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wakati leo Hayati Magufuli anatimiza siku 40 tangu kifo chake, hapa katikati yamezungumzwa mengi lakini Rais Samia Suluhu Hassan alitoa onyo dhidi ya wale waliokuwa wanatoa kauli ambazo hazikuwa na afya kwa nchi yetu na akasisitiza yeye na Magafuli ni kitu kimoja, wala hafurahishwi na wanaofananisha.Ahsante mama kwa kauli yako iliyojaa busara, Hayati Magufuli huko aliko najua anatabasamu kwa jinsi unavyomuenzi kwa vitendo.
Hata hivyo naomba nami nizungumze au nieleze kidogo kuhusu Hayati Magufuli, iko hivi Dk.Magufuli amekuwa Rais wetu kwa kipindi cha miaka mitano na miezi kadhaa kama sio mitano basi miezi sita.Leo hatunaye,ametimiza siku 40 tangu aondoke kwenye uso wa dunia hii,Mungu amemuita ,ameitka na amekwenda moja kwa moja.Hatarudi tena.Inaumiza lakini hatuna budi kukubali,ni mapenzi ya Mungu.
Amekwenda Dk.Magufuli ambaye alikuwa Rais kipenzi kwa Watanzania hasa watanzania wanyonge, waliotafuta kwa halali na wakala kwa halali.Amekwenda Chuma,amekwenda Tinga tinga ,amekwenda Mwamba ,ndio amekwenda na hatutamuona tena, naamini tunaonana baadae.
Amekwenda Jembe kama alivyomuita Rais Mstaafu Jakaya Kikwete wakati anamuelezea Dk.Magufuli na jinsi alivyomuamini na kumtumainia enzi akiwa Rais na JPM akiwa Waziri.
Kikwete katika siku hizi 40 amemzungumzia vizuri sana Hayati Magufuli, ameeleza jinsi alivyompenda kiasi cha jina lake kuliweka kwenye orodha ya Rais ambaye alitamani kuchukua nafasi yake na ikawa hivyo.
Dk.Magufuli amekwenda,katika uso wa Dunia hii hatutamuona tena, hatutasikia tena hotuba zake za 'Live'.Hotuba ambazo hazikuchosa kusikiliza, hotuba ambazo ziliposikika ziliacha matumaini kwa Watanzania, tunakumbuka wakati ule wa Corona hotuba zake zilikuwa dawa,akisema tunapata matumaini na pengine kupona kabisa.
Alijua kutufarijii, alijua kututetea,alijua kutupigania,alijua kutupigania,alijua kubeba maumivu yetu,alijua kubeba manyanyaso yetu.Hkika tumempoteza kiongozi muhimu kwa Taifa la Tanzania na Afrika.Najua leo ndio 40 yake lakini ataendelea kubaki mioyoni mwetu.
Nakumbuka namna ambavyo sauti yake ilipenya kwenye mioyo ya Watanzania, tulimsikiliza na kumuelewa.Najua kama binadamu kuna mahali huenda aliamua na kukosea lakini kwa jicho la kibinadamu, Dk.Magufuli amefanya mengi mazuri kuliko mabaya.Lala salama mzee wetu.
Mzee Ali Hassan Mwinyi ambaye ni Rais mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu alipata nafasi ya kumuelezea vizuri Dk.Magufuli, aliweka wazi jinsi alivyompenda na hata taarifa za kifo chake zilimnyima usingizi,hakuamini.Aliyoyasema mzee Mwinyi siku ile akiwa Chato wakati wa mazishi ya Hayati Magufuli bado tunayakumbuka.
Nakumbuka kule wakati naanza nilisema nitasema kidogo na nimeamua kusema kwasababu ndio 40 yake hayati Magufuli ,sasa naomba niseme, ongeza umakini kidogo kama hutajali.Binafsi nitamkumbuka Dk.Magufuli kwa mengi, nitamkumbuka kwa uzalendo na mapenzi yake mema kwa nchi yetu ambayo naye ni nchi yake.
Nitamkumbuka kwa jinsi alivyotamani Watanzania tuwe tunamtanguliza Mungu kwa kila jambo.Nitamkumbuka kwa namna alivyosimama imara kutetea Watanzania wanyonge.
Ni katika utawala wake ndipo Watazania tumeishi bila kusikia zile kauli za kwamba "Utanijua mimi nani" .Kauli za utanijua mimi nani zilitufanya wanyonge tukose la kufanya,tukose la kusema.
Waliokuwa wanatoa kauli hizo hawakuogopa yoyote, ilifika hatua hata watoa maamuzi nao waliwaogopa.Hakuna aliyeweza kuthubutu kunyoosha kidole .Walikuwa wameishika nchi mikononi,walisikika wao tu wengine woooote midomo tuliziba,tulibaki kimya.
Dk.Magufuli baada ya kuingia madarakani mwaka 2015 katika moja ya hotuba zake alitoa msimamo kwamba Watanzania wote ni sawa, mwenye cheo amheshimu asiye na cheo na asiye na cheo amheshimu mwenye cheo.Watu tukaheshimiana na hapo mwisho kusikia utanijua mimi nani.
Wanyonge wakapata nguvu ndani ya nchi yao.Leo tunadunda,hakuna wa kututisha.Ametimiza siku 40 lakini kwetu ataishi milele, Watanzania tulimpenda na tutaendelea kumpenda,hayuko nasi kimwili lakini kiroho tuko naye .
Nakumbuka katika hotuba hiyo alitoa msimamo wake kwamba matajiri katika nchi hii wengi wao walikuwa wanaweza kufanya chochote na Wabongo tukaa kimya lakini kwake ni tofauti tajiri anaweza kufanywa lolote.
Mbona matajiri walikuwa na adabu.Hakika tukawa tunaheshimiana, nitamkumbuka JPM kwa kuondoa manyanyaso ambayo tuliyapata kutoka kwa baadhi ya matajiri,sio wote,msininukui vibaya.
Uko uliko lala salama, katika hizi siku 40 ambazo haupo nasi, uliyetuachia anatuongoza vizuri tena vizuri sana,hakika ulimuandaa,ulimpika na akaiva kiungozi,tuko salama sana.
Kama nilivyoeleza hapo juu,mengi yamesemwa, ni ngumu kumuelezea Dk.Magufuli ukamaliza,mengi mazuri ambayo amefanya ukitaka kuyaelezea itachukua masiku kuyazungumza na bado hutamaliza .Ukipata nafasi sikiliza wimbo wa Peter Msechu ambao ameuimba baada ya kifo cha Dk.Magufuli.Utajua ,utasikia na kuelewa.
Wingi wa watanzania ambao walijitokeza na kutoa heshima zao za mwisho kwa Dk.Magufuli ni uthibitisho ni jinsi gani tulimpenda, tunaishi kwenye maono yake, ameicha Tanzania salama,ameicha Tanzania imara.
Ametuachia Samia Suluhu Hassan ambaye ndio Rais wetu, hatuna shaka naye, na bahati nzuri mwenyewe ameshasema tumemsikia, wale wenye mashaka naye wafahamu yeye ndio Rais.Ni kauli fupi lakini ina mamilioni ya maneno unapotaka kuitafsiri.Mama nimekusikia na Watanzania wamekusikia ,tuko pamoja nawe.
Wakati naendelea kumfikia Dk.Magufuli nimejikuta nakumbuka na upendo wake kwetu Watanzania.Alikuwa mkarimu ,alikuwa mnyenyekevu, hakika Dk.Magufuli nitakumbuka kwa upendo wako mkubwa.
Nashukuru Mungu nimekuwa miongoni mwa Watanzania ambao nimebahatika kupata mualiko wako kuja Ikulu, nakumbuka mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2016 mwanzoni.
Ulitualika wote ambao tulishiriki kwenye kampeni zao za kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, nakushukuru kwa mualiko ule,nitakumbuka ile picha yako tuliyoiga Ikulu mimi pamoja na waalikwa wengine.
Haikuishia hapo ulitualika Ikulu mara kadhaa , na kubwa zaidi katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2020 nikawa miongoni mwa Watanzania ambao tulizunguka na wewe nchi nzima, wakati unaomba ridhaa ya kuwa Rais kwa Awamu ya Pili.Ni hii ambayo hata hukuimaliza.
Tulikuwa nawe kwenye jua,tulikuwa nawe kwenye mvua ,tulikuwa nawe kila ulikokwenda kuomba kura.Katika uchaguzi Mkuu mwaka 2020 nilijufunza zaidi kuhusu JPM.
Nakumbuka wakati unaomba kura kwa wananchi wa Mburahati mkoani Dar es Salaam,ilinyesha mvua kubwa sana siku ile, wewe na sisi tuliloana.Uliyosema siku ile kwa wananchi hakika yaligusa mioyo ya wananchi.
Nakumbuka siku hiyo ulivyokuwa unatutazama mara kwa mara kwa jicho la huruma.Mvua ile iliishia miilini mwetu lakini ulituma ujumbe wako kwetu, uliwaambia wasaidizi wako waje watuambie" Unatupenda sana,unaona kazi tunayoifanya" .
Ahsante Rais kwa upendo wako kwangu na wengine tuliokuwa wote kwenye kampeni zako.Katika hizi siku 40 hapa katikati nimekumbuka mengi kuhusu Magufuli.Niliposikia anasemwa vibaya niliumia na kwa bahati mbaya wengine waliokuwa wanamsema na kumshambulia alipokuwa hai walimshangilia na kumpigia makofi.
Staki kuzngumzia Bandari ya Bagamoyo ambayo ujenzi wake uliukataa na ukatuambia kwa jinsi mkataba ulivyo anayeweza kukubali ni mwendawazimu tu, hakika tulikusikia tulikuelewa ingawa katika siku hizi ambazo haupo nasi, wapo wanaopigia chapuo ujenzi wa bandari ya Bagamoyo, kweli tena hata Spika wa Bunge Job Ndugai anafahamu.
Acha niendelee na yangu, nakumbuka wakato wa kampeni tena siku ile tukiwa Babati, jua lilikuwa kali sana yaani jua kali kweli, ulituangalia na kisha ukatuma tena ujumbe" waandishi nawapenda sana na hawa ndio waandishi wangu" .Ujumbe ulikuwa wa faraja, ulikuwa mfariji na mwenye kutia moyo,hakika siku 60 za kampeni zikawa nyepesi kwetu.
Hatukuchoka tena,tulisimama nawe .Kinachoniuma naandika haya ukiwa haupo,nani atasoma.Najipa moyo umeondoka kimwili lakini kiroho tuko wote.Maneno haya najua yatakufikia huko uliko.Pumzika Baba , nitakukumbuka sana,Watanzania tutakukumbuka daima, mioyo yetu inalia,machozi hayatafutika mapema kiasi hicho.Katika siku hizi 40 tumeendelea kukuombea kwa Mungu kwa kufanya sala na dua.
Hata hivyo natabasamu kuona msaidizi wako Samia Suluhu Hassan , atafuata nyayo zako na watanzania tunaamini atafanya mengine mazuri kwa ajili ya sisi watu wako.Ahsante Mungu kwa maisha ya Dk.Magufuli hapa duniani,ahsante Mungu kwa kumuwezesha Dk.Magufuli kuijenga Tanzania yetu na kuiletea maendeleo.
Miradi mikubwa aliyoifanya enzi za uhai wake na ile inayoendelea tutakukumbuka, utaishi nasi.Pumzika jemedari wetu,pumzika Mtanzania halisi,pumzika mwana mwema wa Afrika.
Naikumbuka sana siku ya Machi 26 saa 11 jioni wakati mwili wa Dk.Magufuli unapumzishwa ,nilihisi mwili kukosa nguvu,nilihisi ganzi.Chozi lilinitoka .Nilijua ndio mwisho wa kukuona, umetuacha tunakulilia.
Nitakukumbuka daima lakini nikisiliza wimbo wa Tutaona tena JPM ulioimbwa na Gethsemane Group Kinondoni napata faraja ndani ya moyo wangu.Ukipata nafasi usikilize ,utakufariji.Mama Janeth Magufuli na familia yako Watanzania tuko pamoja nanyi kama alivyosema Rais wetu Mama Samia.
Wakati leo mpendwa wetu anatimiza siku 40 kaburini nitoe rai tuendelee kumuombea kwa Mungu ampe pumziko la milele, iko siku tutaonana, msalimie Baba wa Taifa letu Mwalimu Julius Nyerere, na ukiomuona mzee Benjamin Mkapa mwambie watanzania tunamkumbuka na tunampenda.Pumzika Hayati Magufuli,pumzika Chuma, pumzika mwana mwema wa Bara la Afrika.
Said Mwishehe- 0713833822
By Mpekuzi
Post a Comment