Na Faraja Mpina, WMTH, Dodoma
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Faustine Ndugulile ameiagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kushirikiana na Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA-CCC) kuboresha vitengo vyao vya mawasiliano ili kuongeza kasi ya kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi sahihi ya huduma za mawasiliano kwa kuzingatia haki na wajibu pamoja na matumizi sahihi ya simu janja na mtandao.
Dkt. Ndugulile amezungumza hayo mbele ya waandishi wa habari baada ya kikao chake cha kazi cha Wizara na taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo cha kujadili na kufanya mapitio ya taarifa za mapato na matumizi za taasisi hizo kwa robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2020/2021 Kilichofanyika katika Ukumbi wa Hazina jijini Dodoma.
Aidha Dkt. Ndugulile ameziagiza taasisi hizo kuboresha mifumo ya wananchi kutolea malalamiko yanayohusu huduma za mawasiliano na kushughulikia malalamiko hayo kwa wakati na taarifa ya malalamiko hayo itakuwa ni ajenda ya kudumu katika vikao vya kila robo mwaka baina ya Wizara hiyo na taasisi zake.
Ameongeza kuwa elimu kwa umma ikitolewa kwa kiwango kinachojitosheleza kitapunguza baadhi ya malalamiko ya wananchi kwa mfano malalamiko ya vifurushi vya data kuisha haraka ambapo kwa namna moja ama nyingine inasababishwa na settings za simu janja kuruhusu programu zake kujiboresha zenyewe (automatic Updating).
“Kuna mambo ambayo ni muhimu wananchi kuyafahamu kwa mfano matumizi makubwa ya data yanayosababishwa na settings za simu janja ambazo zinaruhusu baadhi ya programu kujiboresha zenyewe nazo zinachangia vifurushi vya data kuisha haraka”, alizungumza Dkt. Ndugulile
Aliongeza kuwa Serikali inatengeneza mazingira wezeshi ya kuhakikisha mawasiliano yanafika kwa wananchi wote lakini kumekuwa na changamoto ya baadhi ya watu kutokuwa na matumizi sahihi ya huduma hii, hivyo wananchi wanahitaji kuelemishwa ili kuhakikisha wanajua wajibu wao na haki zao na kuwa na matumizi sahihi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Akizungumzia kikao cha Wizara na taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo cha mapato na matumizi Dkt. Ndugulile amesema kuwa lengo ni kusimamia nidhamu na matumizi ya fedha za taasisi hizo badala ya kusubiri mpaka mwisho wa mwaka CAG aje kuhoji.
“Sisi kama Wizara tunajipanga kuhakikisha fedha zinazopatikana zinaelekezwa katika kutekeleza majukumu ya msingi ya Wizara na taasisi zake ikiwa ni pamoja na kwenda kutekeleza miradi ya maendeleo.
Dkt. Ndugulile amezielekeza taasisi zilizo chini ya Wizara yake kutolea ufafanuzi maeneo ambayo yaliguswa katika taarifa ya CAG na kama kuna hoja zozote ziliyojitokeza zijibiwe kikamilifu na kuwasilishwa ndani ya wiki ijayo na taasisi ambazo hazikuwasilisha hesabu zao kwa CAG watoe maelezo kwa nini hawakuziwasilisha kwa mujibu wa taratibu za Serikali
Naye Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Kundo Mathew amezitaka taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo kufanya kazi kwa ushirikiano kwa kutambua kuwa Wizara inayowasimamia ipo makini kuhakikisha taasisi hizo zinatimiza wajibu wake wa kuhudumia wananchi na yeye kama msaidizi wa Waziri mwenye dhamana atashirikiana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo na Naibu wake kuhakikisha kuwa Wizara na taasisi zake zinafanya kazi zenye ubora na kwa wakati ikiwa ni pamoja na kuandaa taarifa zinazojitosheleza bila kusubiri maelekezo.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula, Naibu wake Dkt Jim Yonazi, Wakuu wa taasisi za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Tume ya Taifa ya Tehama (ICTC), Shirika la Posta Tanzania (TPC), Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA-CCC), Menejimenti ya Wizara pamoja na baadhi ya watendaji wa taasisi zake.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
By Author
Post a Comment