Jeshi la Chad lachukua madaraka baada ya kifo cha rais |Shamteeblog.






Jeshi la Chad limetangaza kuvunjwa kwa serikali na bunge kufuatia kifo cha rais Idriss Deby wa nchi hiyo lakini limeahidi kutakuwa na uchaguzi huru wa kidemokrasia baada ya kipindi cha mpito cha miezi 18. 

Tangazo ya kuvunjwa kwa serikali na bunge limetolewa saa chache baada ya jeshi kutangaza kifo cha ghafla cha rais Deby kilichotajwa kutokea wakati akiongoza mapambano dhidi ya waasi akiwa mstari wa mbele.

Jeshi limesema Baraza la Mpito tayari limeundwa na litaiongoza nchi hiyo kwa muda wa miezi 18 kabla ya kuitishwa uchaguzi mkuu. Baraza hilo linaongozwa na mtoto wa hayati rais Deby aitwaye Mahammat na jeshi limewatolea wito raia wa Chad kuimarisha amani, uthabiti na utii wa sheria katika kipindi chote cha msiba wa taifa.

Kifo cha rais Deby kilitangazwa na jeshi mapema mchana wa leo na kulingana na taarifa iliyosomwa mbele ya televeshini na radio ya taifa, kiongozi huyo ameaga dunia akiwa kwenye uwanja wa mapambano alikokwenda kuwaunga mkono wanajeshi wake.

Msemaji wa jeshi la Chad Azem Agouna aliyesoma tangazo la kifo cha rais Deby alisema "Ni kwa huzuni kubwa kwamba leo hii tunawatangazia raia wa Chad kifo cha kamanda Idris Deby Itno kutokana na majereha aliyoyapata akiwa kwenye uwanja wa mapambano"

Tangazo la kifo cha rais Deby limetolewa saa chache baada ya tume ya uchaguzi nchini humo kumtangaza kuwa mshindi wa uchaguzi wa rais uliofanyika April 11, ushindi ambao ungemwezesha kuitawala Chad kwa muhula wa sita.

Kufuatia kifo hicho jeshi limetangaza siku 14 za maombolezo huku marufuku ya kutoka nje usiku imetolewa na mipaka yote ya anga na ardhini nchini Chad imefungwa.

Mazingira yaliyopelekea kifo cha rais Deby hayajaweza kuthibitishwa na duru huru za habari kutokana na ugumu wa kufikiwa kwa eneo la mapigano.

Jeshi limesema kiongozi huyo alichukua msimamo wa kishujaa kwa kuongoza opereshini dhidi ya magaidi walioingia Chad wakitokea Libya lakini alipata majeraha na kisha kukimbizwa hospitali ambako mauti yalimkuta.

Mwanasiasa aliyezimudu vyema hamkani za kanda ya Sahel 

Deby, mkuu wa zamani wa jeshi, aliingia madarakani mwaka 1990 baada ya vikosi vyake vya waasi kuuangusha utawala wa rais wa wakati huo Hissene Habre.

Kwa miaka mingi alinusurika majaribio chungunzima ya uasi dhidi ya utawala wake na kufanikiwa kusalia madarakani hadi kuzuka kitisho cha hivi karibuni kutoka kundi la waasi wanaojiita Vuguvugu la Mabadiliko nchini Chad.

Waasi hao wanaaminika wamekuwa wakipatiwa mafunzo na silaha kwenye taifa jirani la Libya kabla ya kuingia Chad mnamo April 11.

Deby amekuwa mshirika muhimu wa Ufaransa katikamapambano dhidi ya makundi ya itikadi kali kwenye kanda ya Sahel na nafasi hiyo ilimwezesha kukwepa lawama za kimataifa juu ya  rikodi mbaya ya utawala wake katika usimamizi wa haki za binadamu.



from Author

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post