Kiongozi wa mila aangua kilio baada ya ng'ombe wake 800 na mbuzi 700 kuondolewa kwenye makazi yake |Shamteeblog.


Na Woinde Shizza Monduli,

Katika hali isiyo ya kawaida kiongozi wa mila ya wamasai nchini maarufu kama Laigwanani,Isaac Ole Kisongo amejikuta akiangua kilio hadharani baada ya mifugo yake kuondolewa katika makazi yake na askari wanaodaiwa kuwa ni wa wanyamapori, kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi wa serikali ya kijiji cha Lemoot wilayani Monduli mkoani Arusha.

Mifugo hiyo ni pamoja na zaidi ya ng'ombe 800 pamoja na mbuzi 700 ambapo walichukuliwa katika eneo la Lemoot katika makazi ya kiongozi Huyo na kisha kupelekwa mpaka Loksale umbali wa kilomita 40 na kisha kutelekezwa.

Akihojiwa na waandishi wa habari waliofika eneo la tukio Ole Kisongo alisema kwamba baadhi ya askari wa idara ya wanyamapori,askari wa jeshi la polisi wilayani Monduli sanjari na baadhi ya viongozi wa serikali ya kijiji na kata ya Lemoot walifika katika makazi yake majira ya usiku na kuamuru vijana wake kuiondoa mifugo yake kwa madai kwamba wamevamia eneo la malisho.

Ole Kisongo alisema kwamba Mara baada ya kupokea taarifa hizo alianza kufanya juhudi za kufuatilia mifugo yake ambapo alifanikiwa kuikuta ikiwa imetelekezwa eneo la Loksale ikiwa haina maji wala chakula huku baadhi ya mifugo ikifariki kutokana na njaa.

"Baada ya vijana wangu kunipa taarifa ndipo nilienda polisi kutoa taarifa na tukaanza kuifuatilia na kisha tukaikuta eneo la Loksale ikiwa imetelekezwa haina maji wala chakula na ng'ombe wapatao watatu tuliwakuta wamekufa " alisema Lekisongo

Hatahivyo,alisisitiza ya kwamba baadhi ya viongozi wa kisiasa kabla ya uchaguzi mkuu walitoa ahadi za kisiasa kwamba pindi wakichaguliwa wataondoa mifugo yote iliyovamia maeneo la malisho na hivyo kinachoendelea kwa sasa ni matokeo ya kauli hizo.

"Mimi sijavamia eneo lolote la malisho hili eneo ninalofuga nilinunua mwaka 2007 na ninalimiliki kisheria kinachoendelea kwa sasa ni ahadi za wanasiasa "

"Niiombe serikali ifanye hatua za haraka mifugo yangu irejeshwe walikoitoa Mimi ni mfugaji na familia yangu inategemea hii mifugo" alisema kwa uchungu

Salome Ole Kisongo ambaye ni mke wa kiongozi Huyo alisema kuwa walikuta mifugo yao imetelekezwa karibu na makazi yake kitongoji cha Lengolwa ambapo mifugo hiyo haikuwa na maji wala chakula .

Yohana Milya pamoja na Munisi Leboy ambao ni wakazi eneo jirani na mifugo ilipotelekezwa walisema kwa nyakati tofauti kwamba walikuta ng'ombe watatu wamefariki na wanahofia kuwa huenda ni kutokana na njaa.

Mkuu wa wilaya ya Monduli,Edward Balele alipotafutwa alisema kwamba taarifa ya tukio hilo haijamfikia mezani na kumtaka mhusika kuwasilisha taarifa ofisini kwake.

Hata hivyo,taarifa za uhakika zimeeleza kwamba tayari jeshi la polisi mkoani Arusha linamhoji mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Lemoot,Marite Laiser pamoja na baadhi ya wananchi kutokana na kushiriki kuiondoa mifugo hiyo katika makazi ya Ole Kisongo.

Laiser, alipotafutwa ili kujibu madai hayo amekiri kuitwa mbele ya ofisi za makao makuu ya jeshi la polisi jijini Arusha hivi karibuni na kuhojiwa kuhusu tukio hilo huku akidai kwamba anaviachia vyombo hivyo vichunguze na kutenda haki.


 


By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post