WATU 12 WAUAWA KWA KUCHINJWA NA WAASI |Shamteeblog.



Miili ya watu 12, wanaoaminika kuwa raia wa kigeni imepatikana ikiwa imekatwa vichwa katika mji wa Palma, Kaskazini Mashariki mwa Msumbiji, baada ya mji huo kuvamiwa na wapiganaji wa kiislamu mwezi uliopita, kamanda wa polisi wa eneo hilo ameiambia runinga ya serikali, shirika la habari la Reuters linaripoti.

Pedro da Silva aliwaonyesha waandishi wa habari mahali ambapo anasema kuwa aliizika miili hiyo 12.

"Walikuwa wamefungwa na kukatwa vichwa hapa," alionekana akisema katika mkanda wa video uliorushwa na televisheni ya serikali jana Jumatano.

Alinukuliwa pia akisema kwamba aliamini watu hao 12 walikuwa wageni kwa sababu walikuwa wazungu, lakini hakuwa na uhakika wa mataifa yao.

Miili hiyo 12 ilizikwa chini ya mwembe, karibu na lango kuu la hoteli ya Amarula ambapo watu wengi walikuwa wamekimbilia wakati wa shambulio la siku kadhaa huko Palma.

"Walikuwa wazungu, wazungu 12 ... mimi ndiye niliyeongoza mazishi," mwanaume aliyevalia koti la kujikinga dhidi ya risasi alinukuliwa akisema.

Makumi ya raia waliuawa na maelfu walikimbia makazi yao baada ya wanamgambo hao kuingia Palma mnamo 24 Machi.

Karibu siku 10 baadaye, jeshi limesema limepata udhibiti kamili wa mji huo, ambao uko karibu na mradi wa gesi ya mabilioni ya dola unaongozwa na kampuni kubwa ya nishati ya Ufaransa, Total.

Wakati huo huo, viongozi sita wa mataifa ya Afrika Kusini wanakutana Msumbiji kujadili jinsi ya kukabiliana na tishio linalozidi kuongezeka kutoka kwa wanamgambo hao.

Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi amekataa kupelekwa kwa wanajeshi wa kigeni, lakini amewaalika wakufunzi wa jeshi la Marekani kuwapa mafunzo wanajeshi wa Msumbiji.

Ureno pia inatarajiwa kutuma vikosi katika wiki chache zijazo kutoa mafunzo kwa wanajeshi wa Msumbiji.

CHANZO - BBC SWAHILI


By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post