WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO AKUTANA NA BALOZI WA CHINA NCHINI |Shamteeblog.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Innocent Bashungwa amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa China kwa lengo la kuboresha  ushirikiano kwenye Sekta  zilizo chini ya Wizara hiyo.

Mazungumzo hayo yamefanyika leo Aprili 22, 2021 katika Ofisi za TBC Jijini Dodoma ambapo wamegusia mambo kadhaa ya kuendeleza Wizara na taasisi zake kimkakati ili kuendana na kasi ya maendeleo ya sayansi, teknolojia na uchumi duniani.

 Waziri Bashungwa alimshukuru Mhe.Balozi kwa Jitihada walizozifanya kujenga Uwanja wa Taifa uliopewa jina la Uwanja wa Benjamin Mkapa na kumuomba Balozi kujenga Uwanja mwingine mkubwa Kanda ya Ziwa ili kumuenzi Hayati John Pombe Magufuli.

Kuhusiana na Tasnia ya Filamu nchini, Waziri Bashungwa amemuomba Mhe. Balozi  kuweza kusaidia kujenga maktaba ya vifaa vya filamu nchini ambayo itakuwa katika Chuo cha Sanaa Bagamoyo.

Amesema, maktaba hiyo itawasaidia wazalishaji Filamu nchini kuwa na kuweza kuazima na kurudisha vifaa tofauti na sasa ambapo kila mmoja anahangaika kutafuta vifaa peke yake na kwa gharama kubwa.

Pia alimuomba Mhe. Balozi  kuutangaza Utamaduni wa Tanzania nchini mwao na sehemu mbalimbali duniani kwa kuwa   nchi ya China imepiga hatua kubwa kwenye eneo la sayansi na teknolojia.

Kwa upande wake,  Balozi wa China nchini Mhe Wang Ke amempongeza Waziri Bashungwa kwa Kuteuliwa tena na kuaminiwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumpa nafasi ya kuongoza tena Wizara hiyo na kuahidi kushirikiana naye.

Mhe. Balozi Wang ameahidi kufanyia kazi maombi yote aliyotoa Mhe. Bashungwa ambapo amesema  atajadiliana  na Serikali yake ili kuona ni kwa namna gani wanaweza kushughulikia maombi hayo.

Balozi Wang amemuomba Waziri Bashungwa kuweka karibu ushirikiano wa TBC na Kampuni ya Star Times nchini ili kuweza kuimarisha Sekta ya Habari hapa nchini.

Ameipongeza Tanzania kwa kuwa miongoni mwa nchi  iliyoiunga mkono nchi ya China katika kuandaa Michuano ya Olimpiki 2008.

Balozi Wang ametoa fursa za nafasi za mafunzo kwa  watumishi wa Serikali nchini China ili kuweza kuongeza ujuzi wa kuhabarisha jamii kiujumla.

Tanzania imekuwa na  ushirikiano wa karibu na wa muda mrefu  na nchi ya China ambao umekuwa wa kihistoria tangu kipindi cha uhuru wake chini ya Hayati Mwalimu Julius Nyerere.




 

 

 



By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post