Hyasinta Kissima-Afisa Habari Halmashauri ya Mji Njombe
Wananchi wa Kijiji Cha Luponde Kata ya Luponde Halmashauri ya Mji Njombe wamefurahishwa na uzinduzi wa zahanati mpya ya Luponde katika Kijiji hicho ambapo kwa takribani miaka 45 kijiji hicho kukosa Zahanati na kupelekea Wananchi kutibiwa katika zahanati za mbali na zahanati ya kiwanda Cha chai luponde jambo lililokuwa likisababisha kero kwa wananchi kutokana idadi kubwa ya wagonjwa na hivyo kupelekea kuzidiwa kwa zahanati ya kiwanda.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ujenzi wa Zahanati hiyo Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Luponde Lucy Kayombo amesema kuwa uzinduzi wa huduma katika Zahanati hiyo mpya ni mkombozi kwa Wananchi wa Kata hiyo na maeneo ya jirani kwani kwa muda mrefu Kijiji hicho hakikuwahi kuwa na zahanati ya Serikali jambo lililowasukuma wananchi hao kuanza ujenzi na wameishukuru Halmashauri kwa kuchangia ujenzi na kuwapatia vifaa tiba, samani, mganga na mhudumu wa Afya kwa ajili ya kuendesha Zahanati hiyo.
“Ujenzi wa Zahanati hii umegarimu kiasi Cha shilingi milioni themanini na tisa laki saba na elfu kumi hii ikiwa ni mchango wa Halmashauri,nguvu za Wananchi, fedha za wahisani na mfuko wa jimbo ambapo Zahanati hii itahudumia Wananchi zaidi ya elfu nne.”Alisema
Diwani wa Kata ya Luponde Ultrick Msemwa amesema kuwa anawashukuru Wananchi wa Kata hiyo kwa ushiriki wao katika kuchangia miradi ya maendeleo na kuwaomba kutoa ushirikiano wa dhati ili kufanikisha ujenzi wa kituo cha afya ambapo kwa sasa wameshaanza ujenzi wa Msingi kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho.
“Leo nitatoa mchango wa shilingi laki tano kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa kituo Cha Afya Luponde ambapo tunataraji huduma zitakuwa bora zaidi. Mpango wetu ni kuwa ndani ya miaka miwili tunakamilisha ujenzi wa majengo yote muhimu ya kituo Cha Afya ili tuweze kwenda kwenye utekelezaji wa miradi mipya” Alisema Msemwa Diwani wa Kata hiyo
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe Illuminatha Mwenda amesema kuwa Wananchi wa Kijiji cha Luponde hawana budi kujipongeza kwa hatua hiyo kwani Zahanati hiyo ni miongoni mwa zahanati bora na kuahidi kushirikiana nao kwenye ujenzi wa kituo cha afya.
Akizungumza mara baada ya kupokea taarifa ya ujenzi mgeni rasmi katika hafla hiyo ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Njombe Romanus Mayemba amewapongeza Wananchi wa Kata hiyo kwa hatua hiyo na amewataka Wananchi hao kuwa mstari wa mbele na kujitoa ili kituo Cha Afya kiweze kujengwa na kukamilika. Aidha amewataka Wananchi hao kujiandikisha na huduma ya bima ya afya CHF iliyoboreshwa ili, zahanati hiyo iweze kujiendesha kwa kuwa na upatikanaji wa dawa za uhakika na zakutosha kwa kipindi Cha mwaka mzima.
“Zoezi la ujenzi wa kituo Cha Afya unakwenda kuanza mara moja. Lakini Halmashauri haitafanya chochote kama Wananchi hamtaanza ujenzi.Tunatarajia kuwapatia mifuko 250 ya saruji kadri mlivyoomba lakini hatutaki iwe stoo tuanze ujenzi kwa kile ambacho mtakua mmechangia.”Alisema mayemba
Wakizungumza kwa wakati tofauti tofauti baadhi ya Wananchi wa Kata ya Luponde wamepongeza uzinduzi wa Zahanati hiyo na kuahidi kushiriki kwenye uanzishaji wa ujenzi wa kituo Cha Afya
Roida malumbo, Marsela Ngailo na Oben Mkolwe wakazi wa kijiji Cha luponde wanasema kuwa uzinduzi wa Zahanati hiyo ni hatua muhimu kwao na wamehamasika kuanza uchangiaji wa kituo Cha Afya
“Changamoto kubwa tuliyokuwa nayo ni ukosefu wa huduma.Ukipata mgonjwa usiku inabidi usafiri mbali kwenda kupata huduma huku barabara ikiwa si rafiki.Tunaomba Wananchi tuchangie kwa bidii ujenzi wa kituo Cha Afya ili tuweze kupata huduma za upasuaji na huduma nyingine ziweze kuwa hapa.Alisema
Uzinduzi wa Zahanati ya Luponde unaifanya Halmashauri ya Mji Njombe kuwa na jumla ya Zahanati 52 na kuanza kwa ujenzi wa kituo Cha Afya Luponde kufanya ongezeko la vituo vya Afya 4 ambapo kwa sasa ipo katika ukamilishaji wa kituo Cha Afya makowo na kifanya vyote vikijengwa kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri na nguvu za Wananchi.
By Mpekuzi
Post a Comment