Wakati malalamiko ya wafanyabiashara wa ndani kuendelea kutapeliwa na wafanyabiashara wa nje yakizidi kusikika kila siku, usiri umetajwa kuwa moja ya sababu.
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) imezitaka kampuni za ndani kutoingia mkataba wa kuuza au kununua bidhaa kimya kimya na kampuni kutoka nje bila kuwasiliana na mamlaka husika.
Kauli hii inakuja ikiwa ni siku chache tangu Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki kutoa tahadhari kwa wafanyabiashara wa ndani ni kwa namna gani wataweza kuepuka kupoteza fedha zao baada ya kununua bidhaa kwa watu wasiowajua.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Kaimu Mkurugenzi wa Ukuzaji wa Biashara Tantrade, Boniface Michael alisema baadhi ya kampuni zimekuwa zikiingia mikataba ya kuuza au kununua bidhaa kwa kampuni za nje bila kushirikisha mamlaka husika na mwisho wa siku kampuni za Tanzania huishia kupoteza fedha. “Kuna kampuni zimekuwa zikisafirisha bidhaa kwenda nje, baadaye hupewa fedha pungufu au isipate kabisa au wale wanaonunua bidhaa kutoka nje wamekuwa wakiletewa bidhaa tofauti kama ni mashine ya kiwango cha chini, tofauti au hailetewi kabisa bidhaa ambayo imeagizwa, hapo ndiyo utawasikia wakitoa malalamiko,” alisema Michael.
“Na wamekuwa wakiogopa kuwasiliana na mamlaka husika na kuamua kufanya siri wakihofia labda biashara yake itachukuliwa, napenda kuwaambia kuwa sisi ni taasisi ya Serikali inayohudumia Watanzania wote na akileta taarifa zake itakuwa ni siri na atahakikishiwa usalama wa mali zake,” alisema Michael.
Alisema suala hilo limewafanya baadhi ya wafanyabiashara kufilisika kabisa, jambo ambalo pia linakinzana na juhudi za Serikali katika kukuza uchumi wa nchi.
“Tantrade inapenda kuwatahadharisha wafanyabiashara hawa kuepuka hali hii kwa kutoingia makubaliano ya kuuza au kununua bidhaa na kampuni yoyote ya nje kabla ya kuhakiki uhalali wa kampuni hiyo kupitia vyombo husika.”
Michael alisema kampuni hizo zinapaswa kutambua kuwa Tantrade imekuwa ikitafuta masoko ya bidhaa za Tanzania kupitia balozi za Tanzania katika nchi mbalimbali, pia kupitia mikutano ya ana kwa ana ya kibiashara, hivyo ni vyema wakatumia masoko hayo.
from Author
Post a Comment