DC LUDEWA AWATAKA WAZAZI KUWASILISHA CHAKULA MASHULENI KABLA YA MWEZI JULAI. |Shamteeblog.

Na Shukrani Kawogo, Njombe.

Mkuu wa wilaya ya Ludewa Andrea Tsere amewataka wazazi wote ambao hawajatoa mchango wa chakula mashuleni wa watoto wao kuvuna mahindi yao na kuyaanika na mpaka kufika Julai 1 mwaka huu wazazi wote  
wawe wamekamilisha michango hiyo.

Hayo ameyasema katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha kimelembe kata ya Nkomang'ombe wilayani humo uliolenga kutatua mgogoro kati ya wazazi na viongozi wa serikali ya kijiji juu ya michango ya maendeleo.

Tsere amesema kuwa kila mzazi ana wajibu wa kuchangia chakula cha mtoto wake shuleni kwa utaratibu waliokubaliana kwani wanapochelewesha hupelekea watoto husoma katika mazingira magumu.

Amesema endapo mzazi yeyote hatakamilisha mchango huo wa chakula kwa muda huo aliotoa atachukuliwa hatua kali za kisheria.

"Haiwezekani watoto wetu washinde na njaa wakati maharage mmeshavuna na mahindi tayari yamekomaa eti mnasubiri mwenzi wa saba ndo muanze kuvuna sasa mimi nawaambia mkatoe mahindi kiasi kinachotakiwa shuleni muanike mpaka julai 1 yatakuwa yamekaka vyema", Alisema Tsere.

Hata hivyo kwa upande wa wazazi hao wamekiri kuwepo kwa usumbufu wa kutoa michango kwa baadhi yao na kudai kuwa wamekuwa wakisumbuliwa na mgambo hadi nyakati za usiku.

Petro Henjewele ni miongoni mwa wazazi  ambao hawajakamilisha michango hiyo amedai kuumizwa kidole na mgambo hao majira ya usiku alipokuwa akitoka kwenye starehe zake na kudai kuwa kulipokucha alifika katika ofisi za kijiji kutoa taarifa ya kilichotokea lakini hakupata ushirikiano wa kutosha.

"Hawa mgambo wamekuwa wakifuata watu nyakati za usiku wengine wanakuwa wamelala na kuanza kuwakamata na kuwaweka lockup kitu ambacho tunaona hatutendewi haki", alisema Henjewele.

Naye Helena Ngatunga amesema ni wananchi wachache wanaogoma kuchangia michango hiyo lakini asilimia kubwa wanatoa michango hivyo ni halali kwa wasiochangia kuwajibishwa.

Naye mmoja wa mgambo hao Mathias Kayombo amesema kuwa wao wamekuwa wakienda kuwafuata wananchi hao nyakati za usiku kwakuwa mchana wamekuwa hawapatikani pia wanapowakuta huwaeleza taratibu lakini wamekuwa wakaidi na kutaka kukimbia hivyo inawalazimu kuwapunguza nguvu kidogo ili waweze kuwakamata na kuwafikisha mahala husika.

"Hawa watu wanatusumbua sana! Sisi tunawaeleza kwa utaratibu lakini wao wanaanza mapambano kuna wengine hutokea madirishani na kukimbia tena baadhi hukimbia huku wamefungwa kamba mikononi na ndiomaana wanapoanza usumbufu kama huo tunawapunguza nguvu kidogo ili kuwatuliza", Alisema Kayombo.

Deogratius Masawe ni kamanda wa polisi wilayani humo aliwataka wazazi hao kuwa watiifu pindi wanapotiwa hatiani kwani kupigwa na kuumizwa na mgambo kunatokana na wao kutotii sheria bila shuruti.

Amesema kwa sheria iliyopo mtuhumiwa anaweza kukamatwa muda wowote anaopatikana hivyo mgambo hao kufika katika nyumba zao nyakati hizo za usiku ni sahihi kulingana na upatikani wa watuhumiwa hao.

Masawe amesema kila mwamanchi ana wajibu wa kuchangia maendeleo ya eneo analoishi hivyo endapo atakaidi kufanya hivyo ni kosa kisheria.

"Hivi mnapotoa michango kwaajili ya kujenga zahanati, shule, madawati na vinginevyo vinawasaidia watu gani kama si ninyi wenyewe? Haya yote yanafanyika kwa faida yenu na si kwa faida ya mtu mwingine sasa mnapoenda kinyume ndipo linakuja suala la kuitwa na uongozi na usipoitikia wito ni lazima nguvu itumike ya kukukamata kwakuwa umeonyesha ukaidi", Alisema Masawe.

Mgogoro huo umemalizika kwa makubaliano ya kukamilisha michango kwa muda uliopangwa huku mkuu wa wilaya hiyo akiahidi kukaa na mgambo hao ili waweze kupunguza nguvu kidogo wanazotumia kwa wananchi.

Wananchi wa kijiji cha Kimelembe kata ya Nkomang'ombe wilayani Ludewa wakiwa kwenye mkutano na viongozi ngazi ya wilaya, kata na kijiji kutatua mgogoro wa michango ya maendeleo.
Wananchi wa kijiji cha Kimelembe kata ya Nkomang'ombe wilayani Ludewa wakifuatilia mjadala uliokua ukiendelea katika mkutano ulioitishwa na mkuu wa wilaya hiyo Andrea Tsere juu ya michango ya maendeleo.
Kamanda wa polisi wilaya ya Ludewa Deogratius Masawe akiwaelimisha wananchi juu ya utii wa sheria bila shuruti katika kuchangia michango ya maendeleo.

 Mkuu wa wilaya ya Ludewa Andrea Tsere (aliyenyoosha kidole) akiongea na wananchi juu ya kuwasilisha mchango wa chakula kwa wototo mashuleni. Kulia kwake ni kamanda wa polisi wilaya ya Ludewa Deogratius Masawe.


By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post