Hospitali ya Benjamin Mkapa imepokea madaktari bingwa wa upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu, mfumo wa chakula na upandikizaji figo kutoka nchini Cuba na watakuwa katika hospitali hiyo kwa muda wa miaka mitatu.
Madaktari hao ni Marlon Bandera, Reginaldo Sarria, Felipe Cabrera na Martinez Matamaro.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Mei 28, 2021 mkurugenzi mtendaji wa hospitali hiyo, Dk Alphonce Chandika ametoa wito kwa wananchi wa mikoa ya Kanda ya Kati kutumia fursa ya uwepo wa wataalamu hao kupata huduma.
Amesema kutokana na kuwepo kwa hofu ya ugonjwa wa Covid-19 mipaka ya nchi nyingi kufungwa, Tanzania inapaswa kujiongeza kupata wataalamu kutoka nje ili kuepusha safari za kwenda nchi mbalimbali kwa ajili ya matibabu.
“Ninamshukuru sana balozi wetu wa Cuba kwani hakutuchoka kila mara tunapopeleka shida au kutaka ufafanuzi alitusaidia na kwa msaada wake leo tumepokea madaktari hawa,” amesema.
Naye Balozi wa Cuba nchini Tanzania, Lucas Domingo amesema wapo Watanzania wengi waliohitimu mafunzo kutoka nchini Cuba na kwa kuimarisha uhusiano huo wameona ni vema kuuendeleza kwa kubadilisha mawazo na ujuzi ili kutoa huduma bora za kimatibabu.
Mkurugenzi wa tiba wa Wizara ya Afya, Dk Wonanji Timothy amesema Tanzania imeendelea kuimarisha huduma zake katika sekta ya afya kwa kuendelea kushirikiana na wadau kutoka nchi mbalimbali ili kukuza ufanisi.
Amesema 2015/16 Tanzania ilipeleka wagonjwa zaidi ya 380 kutibiwa nje ya nchi lakini mwaka 2018/19 ilipeleka wagonjwa 82 na mpaka kufikia mwaka 2020 ilipeleka wagonjwa 43 tu.
“Madhumuni yetu ni kuimarisha huduma za Afya za kibingwa na tutahakikisha kile walichokuja nacho wanatuachia kwa Madaktari wetu ili tuimarishe zaidi huduma zetu” alisema.
By Mpekuzi
Post a Comment