Mwalimu akamatwa akijifanya Usalama wa Taifa ili atapeli |Shamteeblog.
SALVATORY NTANDU
Jeshi la polisi mkoa wa shinyanga linawashikilia watuhumiwa watatu Dismond Zakaria mwalimu (33) Feisal Husein mtaalamu wa teknolojia ya mawasiliano (27) na Juma Almasi (35)mfanyabiashara kwa tuhuma ya kupatikana na nyaraka za serikali za kughushi kwa lengo la kufanya utapeli kwa wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari wilayani Kahama kamanda wa Jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga (ACP) Debora Magiligimba amesema kuwa watuhumiwa hao wamekamatwa mei 26 mwaka huu katika mtaa wa namanga wilayani humo katika msako maalumu wa kupambana na wahalifu.
Alisema kuwa baada ya kukamatwa walipatikana na nyaraka mbalimbali za serikali ikiwemo kitambulisho cha Idara ya usalama wa taifa,vitambulisho viwili vya jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) mhuri mmoja na barua mbalimbali zenye nembo ya jeshi la hilo.
“Watuhumiwa hawa hutumia magari mawili kufanya utapeli katika maeneo mbalimbali ya Tanzania yenye namba za usajili T 677 BMA Toyota Carina na T 110 DSX Toyota Rumion kwa kujiwasilisha kwa wafanyabiashara hususani watoa huduma za kifedha kuwa wao ni maafisa wa umma na wakifanikisha azima yao hutoroka,”alisema Magilimba.
Kamanda Magiligimba amesema kuwa watuhumiwa hao wanatumia vitambulisho vya Jeshi la wananchi viwili vyenye cheo cha Kanali na kimoja cha idara ya usalama wa taifa,pamoja na sare kwa lengo la kuwahadaa wananchi ili kujipatia fedha kwa njia isiyo halali huku wakijua wazi kuwa suala hilo ni kinyume cha sheria.
“Tumewakamata wakiwa na karatasi bandia zinazotumika kutapelia watoa huduma za za fedha,walikuwa wanatumia mbinu ya kuacha mabegi yao yenye karatasi hizo bandia katika ofisi hizo na kisha hurudi jioni na kuwaaminisha kuwa ni fedha halali,jambo ambalo halina ukweli wowote,”alisema Magiligimba.
Amefafanua kuwa mbinu nyingine inayotumiwa na watuhumiwa hao ni pamoja na kuwatongoza na kuwanywesha pombe wanawake na kuwaibia vitu vya thamani kama vile simu na fedha pamoja na kuwaahidi kuwapatia kazi kwa idara ya usalama wa taifa na jeshi la wananchi wa Tanzania.
“Bado tunaendelea kuwahoji na upelelezi ukikamilika tutawafikisha mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili na kuwaomba wananchi kuendelea kutoa taarifa pindi wanapowatilia shaka watu wanamna hiyo ambao hutumia vibaya nyaraka za serikali kujipatia kipato kwa njia isiyo halali,”amesema Magiligimba.
Mwisho
By Mpekuzi
Post a Comment