SERIKALI imesema imejidhatiti katika kuendelea kuboresha sera, miongozo na mazingira kwa ajili ya kuruhusu shughuli za kibunifu kufanyika katika mazingira ya kiushindani na kukua zaidi.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, ameyasema hayo leo Mei 22, 2021jijini Dar es Salaam wakati akifunga wiki ya ubunifu.
Amesema maboresho hayo yatalenga katika maeneo ya ushindani, ulinzi kwa wabunifu wenyewe, usajili, ulinzi katika kazi za wabunifu pamoja na masuala ya ujuzi.
Maeneo mengine ambayo amesema wanatarajia kufanyia maboresho ni katika kuhakikisha kwamba wabunifu wanapata kipato kupitia kazi zao za kibunifu hususani kwa kushirikisha na sekta binafsi kuwekeza katika kukuza sekta hiyo na kuzitumia kwenye viwanda.
Amesema kufanya hivyo kutasaidia sekta hiyo ya ubunifu kukua zaidi na kutumia teknolojia ya kidijitali katika soko la ushindani.
Ameongeza kuwa, Wizara yake imejipanga kuhakikisha kwamba masuala ya kidijitali yanaunganishwa kwenye mitaala katika viwango vyote vya elimu kuanzia shule za msingi mpaka vyuo vikuu.
"Hii itatusaidia kutoa wahitimu wenye uwezo wa kuajilika, wenye uwezo wa kushindana katika mabadiliko haya ya teknolojia ya kidijitali." Alisema Profesa Ndalichako.
Ameendelea kusema kuwa, Serikali imedhamiria kuendeleza bunifu kwa kuziorodhesha, kuzitambua na kusaidia wabunifu katika nyanja zote.
Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Christine Mususi, alisema tayari wamezindua mpango mpya unaojulikana kama Fagio utakaoendelea katika kuendesha shughuli za ubunifu kwa kushirikiana katika kuwawezesha wabunifu kiuchumi.
Mpango huo mpya utafanyika kwa kushirikiana kati ya UNDP, Umoja wa Ulaya (EU), British High Commission, HDIF pamoja na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa Mfuko wa Maendeleo kwa Watu (HDIF), Joseph Manirakiza, amesema bado kunahitajika nguvu ya pamoja kuendeleza shughuli za ubunifu nchini hususani katika eneo la uwezeshaji kiuchumi, kuwajengea uwezo wabunifu na kuboresha sera kwa ajili ya kuweka mazingira mazuri kwa wabunifu ili wanufaike na kazi zao.
"Na HDIF inasaidia katika maeneo matatu ikiwamo uwezeshaji kifedha, usaidizi wa kiufundi katika miradi ya kibunifu kwenye masuala ya afya na elimu kwa baadhi yao."Alisema Manirakiza.
By Mpekuzi
Post a Comment