Na Mashaka Mhando, Tanga
WATU wenye ulemavu wa kusikia (Viziwi), wanakutana na changamoto mbalimbali za kupata huduma ikiwemo kuandikiwa dawa zisizohusiana na maradhi wanayougua.
Akizungumza katika warsha ya siku mbili iliyoandaliwa na Chama Cha Viziwi nchini (Chavita), Mratibu wa mafunzo ya kukuza hadhi ya lugha ya alama nchini, Lupi Maswanya alisema Viziwi wengi wanapokutana na daktari wanashindwa kuelewana.
Alisema licha ya mgonjwa kushindwa kuelewana na watoa huduma za afya, lakini pia ndugu na walezi wa watu hao wenye ulemavu na wao pia hawawezi kuwasiliana nao ili kumbainishia tatizo la mgonjwa daktari.
Alisema kutokana na kukosekana kwa mawasiliano, viziwi wamekuwa wakipatiwa dawa zisizokuwa sahihi kutokana na kutokuelewa tatizo hasa analougua.
"Kuna changamoto kwa viziwi kushindwa kuwasiliana na madaktari na ndugu pia hawawezi kuwasiliana nao, unakuta kiziwi anapewa dawa isiyokuwa ya ugonjwa wake, hii ni hatari sana," alisema Maswanya ambaye pia ni ofisa Ustawi wa Chavita.
Alisema kuwa njia pekee ya kuondoa tatizo hilo ni kuwa na wakalimani katika sehemu za huduma ikiwemo hospitali, mahakamani na maeneo mengine muhimu ambayo viziwi wamekuwa wakienda kufuata huduma.
Mratibu huyo alisema ili jamii iweze kuwasiliana na watu wenye ulemavu wa kusikia ni vema sasa masomo yakafudishwa kwa lugha ya alama ili kuwajengea uwezo viziwi pamoja na jamii nyingine.
Mratibu huyo alisema kwa upande wa elimu lipo tatizo katika ufundishaji wa masomo ya sayansi katika shule za sekondari ambako kuna baadhi ya alama hazipo.
"Masomo ya sayansi kwa shule za sekondari kuna baadhi ya alama zimekosekana hivyo wanafunzi viziwi wanashindwa kwenda sambamba na wenzao hali iliyopelekea mwaka 2016 viziwi walifeli mitihani ya kidato cha nne hasa mkoa wa Njombe.
Hata hivyo, alisema mafunzo wanayotoa kwa viongozi wa serikali wakiwemo walimu, Ustawi wa jamii na polisi kupitia dawati la jinsia litawaongezea ufahamu wa lugha ya alama kwa kazi zao za kila siku.
"Mradi umekuja baada ya changamoto wanayokutana nayo viziwi…Huu mradi ni wa miezi 18 na tumechagua mikoa ya Mtwara, Tanga na Dodoma," alisema.
Awali mwenyekiti wa Chavita mkoani Tanga, David Nyange alisema lengo la warsha hiyo ni kuwajengea uwezo na mwamko wa ufahamu wa lugha ya alama wazazi pamoja na viongozi wa serikali.
Alisema ipo haja kwa kuongeza wakalimani katika maeneo ya huduma ili watu wasiosikia waweze kuwasiliana na watu wengine.
Pia mwenyekiti huyo alitoa wito kwa wazazi wenye watoto viziwi kuhakikisha wanajifunza lugha za alama ili waweze kuwasiliana katika mambo mbalimbali.
Mwenyekiti wa Chama Cha Viziwi mkoa wa Tanga David Nyange
By Mpekuzi
Post a Comment