Waziri Mhagama: Tatizo la ajira nchini, Tafiti mbili kwenye nguvu kazi na Rasilimali watu kufanyika mwaka huu. |Shamteeblog.


Katika kuhakikisha malengo ya kutatua masuala ya ajira na kazi, yanafikiwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), imepanga mwaka huu kufanya tafiti mbili kubwa ambazo zitajikita kwenye kubaini nguvu kazi pamoja na rasilimali watu.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama, wakati akifungua Kongamano la Wadau wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo  tarehe 27 Mei, 2021, Jijini Dodoma.

Ameeleza kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wanaendelea kushirikiana ambapo Wizara hiyo inapitia sera ya elimu na huku Ofisi hiyo ikifanya tafiti.

“Mwaka huu tumeamua kufanya tafiti mbili kubwa ambapo tafiti moja tunaendelea nayo ambayo ni hali ya nguvu kazi nchini. Utafiti huo utatausaidia kujua ni asilimia ngapi ya vijana wanaofundishwa ndani ya  nchi na  wanaweza kuajirika nchini  na kama hawajaajiriki ni kwa nini. Aidha Utafiti huo utatusaidia kuelewa sekta ipi yenye fursa nyingi kuliko sekta nyingine ya ajira hii itasaidia mafunzo ya ufundi yaendane na mahitaji yetu ya ajira” Amesisitiza Mhagama

Aidha, Mhe. Mhagama amefafanua kuwa serikali imeshakamilisha utaratibu wa kufanya utafiti wa Hali ya rasilimali watu nchini. Utafiti huo utasaidia kuelewa juu ya watanzania waliopo nchini na waliopo nje ya nchi kama wanaendana na mahitaji ya ajira kwa sasa.

Ameongeza kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu imekuwa ikisimamia vibali vya ajira kwa wageni, hivyo wataelewa sababu ambazo hupelekea wawekezaji kuhitaji kuwaleta watu wao wenye ujuzi ile hali wenye ujuzi wa viwango hivyo wapo hapa Tanzania, lakini pia itaeleweka maeneo gani ambayo nchi haina ujuzi na wangependa ujuzi huo upatikane hapa nchini.

Mhe. Mhagama amewataka wadau wa elimu ya Ufundi kuendelea kushirikiana na serikali katika kuhakikisha changamoto za ajira zinashughulikiwa ipasavyo nchini. Amesisitiza kuwa ili kuweza kuwa na uchumi wa kati endelevu hadi kufikia uchumi wa juu tunahitaji kuwa na mfumo rasmi wa kuwandaa vijana katika viwango vya juu vya maarifa, ujuzi, na stadi za kutenda.

Mhe. Mhagama amefafanua kuwa kwa sasa serikali inaendelea kutekeleza miradi ya kimkakati kwenye sekta ya nishati ya umeme, Reli ya kisasa, kwenye Sekta ya Afya na Elimu pamoja na Barabara na hivi karibuni utatekelzwa mradi wa Bomba la mafuta kutoka Tanzania hadi nchini Uganda. Ameeleza kuwa miradi hiyo ili iwe endelevu ipo haja ya kuwa na wataalamu wenye ujuzi wa kuendeleza uangalizi wa miradi hiyo.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la (NACTE), Prof. John Kondoro na Katibu Mtendaji (NACTE) Dkt. Adolf Rutayuga,wamefafanua kuwa  Kongamano hilo litalisaidia Baraza hilo kuwa na mipango ya kuunganisha nguvu ili kuwekeza kiasi cha kutosha katika Elimu ya Ufundi.

Aidha, wamefafanua kuwa wataweza kuwa na suluhisho kwenye masuala ya kupata maeneo ya kutosha ya mafunzo ya vitendo, Upatikanaji wa Takwimu sahihi za wataalamu kwenye sekta za ajira, Kuimarisha uhusiano kati ya Taasissi za Mafunzo na soko la ajira, na hatimaye Elimu na Mafunzo ya Ufundi itaweza kutoa mchango mkubwa katika Maendeleo ya sekta zote za kiuchumi hapa nchini.

Pia, Mkurugenzi Idara ya Wanachama, Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Zachy Mbenna ameiomba serikali kushirikiana na sekta Binafsi katika juhudi za kuendeleza kukuza ujuzi kwa kusimamia tozo inayotozwa ya kukuza ujuzi  kwa kuelekezwa kwenye kukuza ujuzi moja kwa moja  kwa kuishirikisha sekta Binafsi kwenye maoni ya matumizi yake.

Ameomba kiwepo chombo cha kitaifa kitakacho ratibu juhudi za kukuza ujuzi kwa kuwaunganisha wanaotoa mafunzo ya kukuza ujuzi. Aidha, ameomba kuwapa motisha waajiri wenye utaratibu wa kukuza ujuzi katika maeneo yao ya kazi kwa kupewa utambuzi wakati wa kulipa kodi, ameomba wadau hao wa sekta Binafsi wanaochangia masuala ya ujuzi kupewa mazingira ya kipaumbele wakati wa uwekezaji. Utekelzaji wa masuala hayo yatasaidia kuongeza idadi ya wadau wanaotekeleza masuala ya kukuza nchini.

Kauli Mbiu ya Kongamano hilo ilikuwa ni “Kuimarisha Ushirikiano wa Wadau katika Kukuza Ujuzi kwa Maendeleo ya Uchumi wa Viwanda” Wadau hao ni Serikali, Taasisi zinazotoa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, na Waajiri. Kongamano hilo limeandaliwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) kwa ushirikiano na Taasisi ya Sekta Binafsi.

MWISHO.




By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post