Na Said Mwishehe, Michuzi TV
UONGOZI wa Wildlife Conservation Society of Tanzania(WCST), umesema utalii wa ndege ukitumika ipasavyo unaweza kuvuta watalii wengi zaidi kuja nchini kwa ajili ya kuona aina mbalimbali za jamii ya ndege ambazo nyingine hazipatikani nchi yoyote zaidi ya hapa nchini.
Akizungumza baada ya kufanyika programu ya wanachama wa taasisi hiyo kuangalia aina ya jamii za ndege zinapatikana Posta Dar es Salaa, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo Nsajigwa Kyonjola amesema utalii wa ndege nchini umeendelea kushika kasi kutokana na watalii kutoka mataifa mbalimbali kuja kuona aina ya jamii ndege zilizopo.
"Ujue tunakokwenda watu wengi watakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu Simba na mazingira yake na anakula nini lakini kuna watu wachache sana wanaojua kuhusu ndege.Huko tunakoelekea utalii wa ndege utakuwa mkubwa sana , sasa ukienda maeneo mbalimbali ya milima ya Usambara na Morogoro watalii wanaokuja maalumu kwa ajili ya kuangalia ndege wanaongezeka, kwa hiyo ni fursa kutumia rasimali kubwa ya ndege tulizonazo kujitengenezea kipato kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
"Nakumbuka mwaka 2013 kule Usambara alikuja mzee mmoja mwenye umri wa miaka 95 aliyetokea nchini Marekani na shauku yake kubwa alikuja kumuona ndege aina ya Kigong'ota wa Usambara kwani alikuwa ameshaona aina nyingine zote za ndege huyo.
"Hivyo kijana wetu alifanikiwa kumuonesha ndege huyo na yule mzee alichokifanya alimpa Dola 3,000 , pamoja na vifaa vyote vya kuangalia ndege alivyokuwa navyo akidai katika maisha yake ametimiza ndoto yake ya kuona ndege huyo.
"Kwa hiyo katika maeneo ambayo watu wanatambua jamii za ndege na kutoa maelekezo yake vipato vyao sio sawa na mtanzania wa kawaida, wenzetu Kenya wametoa nafasi kubwa kuhusu utali wa ndege, hivyo taasisi yetu nayo imekuwa ikihamasisha watanzania kujikita kwenye kuufanya utalii huo kwani unalipa sana,"amesema.
Amesisitiza Tanzania ambayo ina jamii nyingi za aina ya ndege, eneo hilo linaweza kutumika kama fursa ya kutoa ajira kwa vijana huku akitoa mifano kadhaa ya vijana ambao wamepita kwenye taasisi yao na kupata elimu ya kutosha ya kutambua ndege, aina zake , mazingira yao na vyakula wanavyokula pamoja na mambo mengine, wamekuwa wakijiingizia kipato cha kutosha.
"Ukiwa unatambua aina ya ndege zaidi ya jamii 100 kwa maana ya kuwatolea maelezo vizuri, mtalii akija analipa zaidi ya Dola 150,000 kwa siku.Bahati nzuri Wizara ya Maliasili na Utalii inaambua kuhusu utalii wa ndege lakini nitoe mwito bado tunahitajika kuongeza nguvu zaidi,taasisi yetu tunayo programu ya kwenda shuleni na vyuoni kwa ajili ya kuhamasisha vijana kujifunza kuhusu utalii wa ndege,"amesema.
Amefafanua wamekuwa wakitoa elimu kuhusu manufaa ya ndege, kuwatambua, milio yake, aina ya vyakula wanavyokula, mazingira wanayoishi , jisni waavyochagua mazingira.
Alipoulizwa kuhusu mabadiliko ya tabianchi iwapo yamekuwa na athari kwa ndege, amejibu kuwa mabadiliko hayo yanaathari kwa kiwango kikubwa kutokana na sababu mbalimbali na vema ikafahamika ndege wameishi kwenye haya mazingira kwa mamilioni ya miaka.
"Unapozungumzia mabadiliko ya hali ya hewa hasa hasa unazungumzia mabadiliko ya tabianchi ambapo athari zake ni ongezeko la joto ambalo linakwenda kusababisha mvua zikija zinakuwa nyingi kupita kiasi au kwa kiwango cha chini, na athari kubwa mabadiliko haya yanakwenda kuharibu mazingira kuanzia mimea inayozalisha vidudu ambavyo ndege huvila kama chakula.
"Pia uharibu mazingira ambayo ndege hutengeneza viota, kwa hiyo ndege moja kwa moja wanapata athari.Tunafahamu kuna ndege ambao wamekuwa wakitoka nchi za Ulaya kuja Tanzania, hivyo mazingira yanapokuwa tofauti madhara yake kwa ndege hayo ni makubwa,"amesisitiza Kyonjola.
Kuhusu programu ya kuangalia ndege maeneo ya Posta, amesema lengo ilikuwa kujenga uelewa wa wanachama wao kuhusu aina za ndege wanaopatikana eneo hilo lakini na mazingira wanayoishi, lakini tukilenga waweze kufanya viumbe hivi kama burudani , kupumzisha akili na kubwa zaidi kutumia rasimali hii ya viumbe hai kuvutia utalii wa ndege na mazingira yake."
Wanachama wa WCST wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kuamua kupiga picha kwenye moja ya mti mkubwa ulikuwepo maeneo ya Gymkhana walipokuwa katika programu ya kuangalia ndege.
Sehemu ya wanachama hao wakiangalia ndege katika maeneo ya Posta jijini Dar es Salaam.Naibu Mkurugenzi Mkuu wa WCST Nsajigwa Kyonjola akifafanua jambo katika ofisi za taasisi hiyo kabla ya kuanza kwa programu ya kwenda kuangalia ndege maeneo ya Posta.
Ofisa Programu wa WCST Benedict Lisoso (kushoto) akiangalia ndege wakati wa programu hiyo.
Baadhi ya wanachama wa taasisi ya Wildlife Conservation Society of Tanzania(WCST),wakiangalia aina ya ndege kwenye kitabu wakati walipokuwa kwenye programu maalum iliyaondaliwa na taasisi hiyo kwa ajili ya kuangalia ndege katika maeneo ya Posta jijini Dar es Salaam.
Wanachama wa WCST wakiwa makini kuangalia aina ya ndege kwenye kitabu chenye aina mbalimbali za ndege wakati wa programu ya kuangalia ndege walioko Posta ,Dar es Salaam.
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa WCST Nsajigwa Kyonjola(kushoto) akitoa maelezo kwa wanachama wa taasisi hiyo kuhusu aina za ndege na mazingira wanayoishi wakati wa programu maalum ya kuangalia ndege.
Wanachama wa WCST wakiwa na Naibu Mkrugenzi Mkuu wa taasisi hiyo Nsajigwa Kyonjola wakiangalia ndege maeneo ya Gymkhana jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wananchi wa WCST wakiangalia ndege kwenye kitabu wakiwa na lengo la kujiridhisha na aina ya ndege waliyemuona katika maeneo ya Posta walipokuwa kwenye programu ya kuangalia ndege iliyoandaliwa na taasisi hiyo.
By Mpekuzi
Post a Comment