Na Grace Semfuko, MAELEZO.
Waziri wa Madini Mhe. Doto Biteko amesema Wizara yake itayafanyia kazi mapendekezo sita, yaliyotolewa na Wachimbaji wakubwa na wa kati wa madini kwenye kikao cha wadau wa sekta hiyo waliokutana Mei 12, Jijini Dar es Salaam.
Mapendekezo hayo ni pamoja na kuweka vivutio na sera nzuri za biashara ya Madini ili kuwavuta wawekezaji wengi zaidi wa ndani na nje ya nchi, kufanya tafiti za madini, kuweka mazingira wezeshi ya biashara hiyo, kuwa na ulinzi na usalama wa uhakika wa biashara hiyo, uibuaji wa vipaji na mafundi wa madini wa kitanzania na uboreshwaji wa mindombinu kwenye maeneo ya migodi.
Akifungua mkutano wa siku moja wa majadiliano baina ya Serikali na Wachimbaji wa Madini wakubwa na wa kati, wenye lengo la kukuza sekta hiyo nchini, Biteko amesema Wizara yake inayafanyia kazi mapendekezo ya wachimbaji hao ili yaweze kuleta tija ya kiuchumi.
“Naomba niwahakikishie tutayafanyia kazi mapendekezo yenu yote mliyoyatoa hapa, lengo letu ni kuhakikisha biashara hii inazidi kukua na kuleta tija ya kiuchumi” amesema Waziri Biteko.
Amesema Serikali inaendelea kusimamia sekta ya madini ili iendelee kuwa na tija, kutokana na sekta hiyo kuongoza kwa ukuaji wa uchumi wa asilimia saba kutoka asilimia 3.8 ya mwaka 2015, na kutajwa kuongoza kwa kuliingizia Taifa pato la kigeni.
Biteko pia amesema asilimia 52.4 ya bidhaa za Tanzania zinazouzwa nje ya nchi, zinatokana na mazao ya madini na hivyo kuifanya sekta hiyo izidi kuimarika kwenye mapato na kuchangia sekta nyingine katika ukuaji wa uchumi.
“Sekta ya Madini imetoka mbali, imepita katika historia ndefu sana, historia mbaya na nzuri, imetoka kwenye kundi ambalo biashara ilikuwa ikifanywa kwa kificho, leo imekuwa ni sekta ambayo biashara inafanywa kwa uwazi, mchango wake unaweza kupimwa katika maeneo mbalimbali ikiwepo kukuza uchumi wa nchi kutoka asilimia 3.8 hadi asilimia 7” amesema Biteko.
Naye, Mwenyekiti wa Chemba ya Madini Mhandisi Philbert Rweyemamu ameishauri Wizara hiyo, kujadiliana na wadau ili kuangalia namna bora ya kuongeza migodi mipya ya uchimbaji wa madini, na kuongeza mitaji kutoka katika masoko ya hisa ya nchi za nje.
“Tunahitaji pesa za wawekezaji kutoka nje ya nchi kwa sababu soko la hisa la Dar es Salaam halijakidhi mahitaji ya sasa, na mara nyingi pesa za kuanzisha hii miradi zinatoka kwenye masoko makubwa ya hisa ya nchi za nje, kwa hiyo tunashauri Wizara tujadiliane kwa yale ambayo tunafikiri kama yakiwekewa mkazo au yakabadilishwa, yataongeza tija na tutaona migodi mipya ikianzishwa” amesema Mhandisi Rweyemamu.
By Author
Post a Comment