Ukaguzi wa daraja hilo ukiendelea.
Na Doto Mwaibale, Singida
MENEJA wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Mkoa wa Singida Mhandisi Matari Masige amepata ajali kwa kuteleza na kuanguka akiwa site anatekeleza majukumu yake ya kikazi wakati akijaribu kumuonyesha Mkuu wa Mkoa Dk. Binilith Mahenge baadhi ya kingo za chini za maendeleo ya ujenzi wa daraja la Sibiti, lililopo mpakani mwa mkoa wa Singida na Simiyu.
Tukio hilo limetokea leo eneo la Wilaya ya Mkalama, mkoani hapa unapotekelezwa mradi huo wakati kiongozi huyo wa Tanroads akishiriki ziara ya Dk. Mahenge ya kukagua miradi ya maendeleo ya ujenzi wa madaraja ya Sibiti na Msingi yanayotekelezwa na wakala huyo ndani ya mkoa.
Kwa mujibu wa Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Singida, Dk. Deogratius Banuba alisema Meneja Masige alifikishwa kwenye hospitali ya mkoa huo majira ya jioni akiwa na jeraha kichwani.
"Tumempokea na tunaendelea kumpa matibabu na anaendelea vizuri," alisema Dk. Banuba.
Hata hivyo, kabla ya kufikishwa hospitali ya mkoa chini ya usimamizi na uratibu wa mkuu wa mkoa, Masige alipatiwa huduma ya kwanza katika zahanati iliyopo Bukundi, Meatu Mkoa wa Simiyu jirani na ulipo mradi wa ujenzi wa daraja hilo.
Awali akitoa taarifa ya hatua za utekelezaji wa mradi huo, Mhandisi Masige alisema kukamilika kwa daraja hilo ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 95 utakwenda kurahisisha usafiri wa kutoka Singida hadi Bariadi kwa kupunguza urefu wa takribani kilomita 200. Ikilinganishwa na urefu wa kutoka Singida Nzega hadi Bariadi kilometa 674.
Pia kwa mujibu wa Tanroads daraja hilo lenye urefu wa mita 82, na likilojengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 28.5 linakwenda kurahisisha na kufungua huduma za kijamii na kiuchumi kwa wananchi wanaoishi mpakani wa mikoa ya singida na simiyu kwa kutumika na kama kiunganishi cha upatikanaji wa huduma za afya kwenye hospitali ya Rufaa ya Hydom.
By Mpekuzi
Post a Comment