STAMICO yachangia matibabu ya watoto wenye vibiongo |Shamteeblog.

 KATIKA kuunga mkono kampeni ya uchangiaji wa matibabu kwa watoto wenye matatizo ya vibiongo, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), limetoa msaada wa mahitaji mbalimbali kwa watoto hao pamoja na wengine waliolazwa katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI).


Pia STAMICO imetoa kiasi cha Sh milioni tatu kuchangia matibabu ya watoto zaidi ya 40 wanaosubiri matibabu ya tatizo la vibiongo.

Akikabidhi msaada huo leo Juni 25, 2021 jijini Dar kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Stamico, Deusidedit Magala alisema wameamua kuungana na majirani wenzao yaani Moi kuhitimisha wiki ya utumishi wa umma kwa kutoa msaada huo.

“Kwa kile tunachokipata tumeamua sehemu yake tujitolee kwa ajili ya kuwasaidia watoto hasa wanaotarajiwa kufanyiwa operesheni za kibiongo kwa hiyo tumekuja na vitu vya kuwagawia wagonjwa lakini pia katika hiyo kampeni tumechangia jumla ya Sh milioni tatu.

“Hii ni sehemu ya kuadhimisha utumishi wa umma ambapo wafanyakazi tunaungana kwa pamoja kuwaona wenzetu waliopo hapa Muhimbili,” alisema.

Aidha, akipokea msaada huo, Kaimu Mkurugenzi huduma za uuguzi taasisi ya mifupa Moi, Fidelis Lucas Minja aliishukuru Stamico kwa msaada waliowapatia ikiwamo kuunga mkono mbio za Marathoni ambazo zinalenga kukusanya zaidi ya Sh milioni 800 kwa ajili ya matibabu ya watoto hao wenye matatizo ya vibiongo.

“Wenzetu wanapohitimisha siku ya utumishi wa umma wameona ni vizuri kuchangia mbio za marathoni na kuwasaidia watoto wenye vibiongo na kuwaona wenye matatizo mbalimbali.

“Ni tendo la huruma kusaidia, hata sisi kama wauguzi na watumishi tunaweza kufanya lakini tunawaalika wengine kutoka taasisi mbalimbali na mashirika waje kuwasaidia watoto wenye shida kwani mahitaji ni mengi na serikali peke yake haiwezi. Hivyo kupitia taasisi hizi tunaweza kutimiza malengo ya nchi yetu“, alisema.

Alisema zaidi ya watoto 40 wenye shida ya vibiongo wanatarajiwa kutumia gharama zaidi ya Sh milioni 800 za matibabu ambapo motto mmoja pekee huhitaji zaidi ya Sh milioni 21.

“Watoto waliopo ni wengi, tunawaomba watu kutoka taasisi mbalimbali wachangie hasa kupitia marathoni hii itakayofanyika Jumapili Juni 27, mwaka huu.

“Kuna mbio ndefu za kati na awali yaani kilomita tano, 10 na 21. Vigezo hakuna isipokuwa unatakiwa kuchangia Sh 35,000 kiingilio ila ukichangia Sh 500,000 unatambulika kama mmoja wa wafadhili wa mpango huu“, alisema.
 Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Stamico, Deusidedit Magala (kushoto) akimkabidhi Kaimu Mkurugenzi huduma za uuguzi taasisi ya mifupa Moi, Fidelis Minja fedha taslimu Sh milioni tatu ambazo ni mchango wa Stamico kwa ajili ya kuchangia matibabu ya watoto wenye matatizo ya vibiongo. Wafanyakazi hao wa Stamico jana walitembelea taasisi hiyo na kuwaona watoto wagonjwa waliolazwa katika wodi za taasisi hiyo kwa magonjwa mbalimbali.


Mmoja wa watumishi wa Shirika la Taifa la Madini – Stamico (kushoto) akitoa msaada kwa baadhi ya wagonjwa waliolazwa katika wodi za taasisi ya mifupa Muhimbili –Moi jijini Dar. Leo Juni 25, 2021 wafanyakazi wa Shirika hilo wakiongozwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Stamico, Deusidedit Magala walitoa mchango wa Sh milioni tatu kuchangia matibabu ya watoto wenye matatizo ya vibiongo.


Baadhi ya wafanyakazi wa Shirika la Taifa la Madini -Stamico wakiwa ndani ya wodi ya watoto wenye matatizo mbalimbali katika Taasisi ya Mifupa Moi. Wafanyakazi hao walitembelea taasisi hiyo na kuwaona watoto wagonjwa waliolazwa katika wodi za taasisi hiyo na kuwagawia mahitaji mbalimbali.


By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post