Waziri Wa Kilimo Aonesha Wazi Kutoridhishwa Na Mwenendo Wa KNCU |Shamteeblog.
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Moshi
Serikali imeonyesha kutoridhishwa na muenendo wa chama kikuu cha ushirika Mkoani Kilimanjaro (KNCU) ambapo wanachama wametakiwa kusimama imara wakati wa uchaguzi katika kuhakikisha wanapatikana viongozi bora ambao wataiwezesha KNCU kusonga mbele.
Taarifa ya tume ya waziri Mkuu kuhusu KNCU imebainisha madudu mengi ambapo baadhi ya mali mbalimbali zilihujumiwa na nyingine kuuzwa ikiwemo kuingiwa kwa mikataba isiyo sahihi.
Kati ya vyama vya ushirika 43 vilivyofanyiwa ukaguzi na shirika la ukaguzi wa mahesabu kwa vyama vya ushirika (COASCO), vyama 12 vimepata hati zisizoridhisha jambo ambalo halileti taswira nzuri.
Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda ameyasema hayo tarehe 28 Juni 2021 wakati akizungumza kwenye mkutano mkuu wa 36 wa chama kikuu cha ushirika Mkoani Kilimanjaro (KNCU) ambapo amesisitiza kuwa serikali inahitaji sheria hiyo ifanyiwe marekebisho ili kuiwezesha kuleta tija kwenye ushirika.
Amesema kuwa Serikali ipo katika mchakato wa kufanya marekebisho ya sheria ya vyama vya ushirika ya mwaka 2013 lengo likiwa ni kuondoa madhaifu yanayodidimiza vyama hivyo nchini.
Waziri Mkenda amewataka wanaushirika kuipitia sheria hiyo na kutoa maoni ambayo yatawezesha kuiboresha sheria hiyo na kuifanya kuwa na tija katika vyama vya ushirika nchini.
"Ingekuwa ni mamlaka yangu ningesema viongozi wote wa bodi waondoke na msigombe na tuchague wengine ila kwasababu ushirika ni mali ya wanaushirika niwaombe mtumie nafasi yenu kuhakikisha mnawashawishi wale wenye uwezo kugombe nafasi za uongozi" Amesema Waziri Mkenda na kuongeza kuwa
"Kwa hali hii naona vyama vya ushirika vishindane katika kupata hati safi maana ni lazima hesabu zipangwe vizuri maana mali bila daftari huisha bila habari"
Aidha, Prof Mkenda aliutaka umoja wa vyama 32 vya ushirika (G32) kufuata sheria kama wanavyopewa maelekezo na Mrajisi wa vyama vya ushirika nchini, katika kuanza kufanya biashara ya kahawa na kwamba iwapo watashidwa kufuata sheria serikali haitakuwa radhi nao.
Akizungumza katika mkutano huu, Mrajisi wa Taifa wa vyama vya ushirika, Dkk Benson Ndiege, amesema mkutano Mkuu wa uchaguzi wa KNCU uliahirishwa kwa lengo la kutoa frusa kwa wanachama kuchagua viongozi Bora ambao watakuwa na uwezo na ubunifu.
"Tatizo kubwa linalokabili vyama vya ushirika hapa nchini ikiwa ni pamoja na KNCU Ni kukosekana kwa dhana ya utawala bora, mkutano wa uchaguzi umeahirishwa tumieni nafasi hii kupata viongozi ambao wataitoa KNCU ilipo na kuisogeza mbele kwa manufaa ya wakulia" Amesema
Naye Mwenyekiti wa chama kikuu cha ushirika Kahama (KNCU), Emanuel Cherehani, amesema ili KNCU ifanikiwe ni lazima viongozi kuwa waaminifu, waadilifu pamoja wabunifu ili kusaidia chama hicho kupiga hatua zaidi na wakulima kuona mchango wake.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha kuendeleza Kilimo Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania-SAGCOT, Ndg Geoffrey Kirenga amesema kuwa KNCU ina nafasi kubwa kurudisha heshima ya Ushirika Tanzania.
By Author
Post a Comment