Wizara Ya Kilimo Yaweka Msukumo Kuzalisha Pembejeo Nchini |Shamteeblog.


 Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Arusha
WIZARA ya Kilimo imesema kwa sasa imeweka msukumo kwa wawekezaji kuzalisha pembejeo hapa nchini ili kurahisisha upatikanaji wake.

Aidha, imeeleza inapambana kutafuta masoko ili bei za bidhaa mbalimbali za mazao zipande na kuwa zenye tija kwa mkulima.

Kauli hiyo imetolewa jijini Arusha  tarehe 30 na Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda wakati akizungumza na waandishi wa habari ikiwa ni utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa kupitia hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan pamoja na maelekezo ya  Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Ndg Daniel Chongolo hivi karibuni kuhakikisha kilimo kinakuwa na tija.

Amebainisha kwa sasa wanaweka msukumo kwa wawekezaji kuzalisha pembejeo hapa nchini ambapo katika kufanikisha hilo hivi karibuni alitembelea kiwanda cha mbolea cha Minjingu kuhakikisha kinafanya upanuzi na kuongeza uzalishaji.

”Kuna kiwanda kingine kinajengwa Dodoma, kuna viwanda viwili vya viuatilifu vinajengwa hapa Arusha na tunataka kuwahakikishia wawekezaji hao kwamba tutawapa kipaumbele katika kununua pembejeo,” Amesema

Ameeleza kuwa baadhi ya maeneo matumizi ya mbolea yanahitaji kuwekwa chokaa ili iweze kuwa na tija katika kilimo hivyo kwa sasa wanaongeza juhudi za kupima afya ya udongo na aina yake.

Aidha, amesema yatafanyika mafunzo rejea mengi kwa mabwana shamba ili kutoa ushauri wa matumizi ya mbolea sehemu ambayo inahusika.

Amesema licha ya kutokuwa na shida ya soko la mafuta nchini kwakuwa ipo ardhi ya kutosha kuotesha alizeti, michikichi, pamba lakini bado yanaagizwa kutoka nje ya nchi.

”Tunakidhi mahitaji ya mafuta ya kula kwa asilimia 47 tu nchini na hiyo inatokana na tija ndogo ya uzalishaji kiasi kwamba inakuwa ni bei rahisi zaidi kuagiza mafuta kutoka Malaysia, Indonesia, kuliko kuchukua mafuta ya mawese au ya alizeti.

Kwa hiyo suala hapa kubwa ni tija na soko kwenye mafuta ya kula lipo, kwenye ngano lipo, takribani tani 800,000 mpaka milioni moja  humo ndani tunazalisha tani 77000, soko la ngano lipo, uzalishaji ni mdogo na tija ni ndogo kiasi kwamba ngano inayokuja kutoka nje inaonekana ni bei ndogo zaidi kuliko inayotumika hapa nchini,” Amesema.

Ameeleza unaweza kwenda na zao moja hado jingine ukagundua kuwa changamoto iliyopo ni tija na kwamba wamegundua ili kupambana na changamoto hiyo ni lazima kufanya utafiti ili kuwa na mbegu bora.

”Sasa kuna mbegu zimegunduliwa pale Kibaha kwenye kituo cha utafiti ambapo ikitumika kwa hekta moja unaweza ukapata kuanzia tani 22 mpaka 50 za mihogo.

Sasa hivi tunapata wastani wa tani 8 mpaka 3 kwahiyo hata soko la China ambalo tunataka kupeleka mihogo sasa hivi tunashindwa kufanya hivyo kukidhi mahitaji ya soko kwa sababu tija ni ndogo”

Ameongeza:”Lakini vilevile, mihogo inazalisha Starch, tunaagiza Starch toka nje kwa sababu hatujazalisha mihogo ya kutosha kuzalisha Starch hapa nchini kwa utafiti na mbegu bora tunaweza tukajitegemea kwenye vitu vingi, Lakini chamngamoto kubwa kwetu ni pembejeo kwa sababu nyingi zinaagizwa nje na kwa gharama kubwa,”.

Pia Waziri Mkenda amesema kuwa, kunapokuwepo changamoto ya soko la mazao ni lazima gharama za uzalishaji zitakuwa kubwa na matokeo yake mkulima halimi kwa faida.

Amesisitiza kuwa kwa sasa wanapambana na masoko kwakuwa ni suala ambalo lazima walivalie njuga na wanafanya hivyo ili bei ianze kupanda.

”Tunafuatilia bei za mahindi kwa mfano Ruvuma huko, Mbeya ziko chini sana ukilinganisha na gharamaza uzalishaji,” Amesisitiza

MWISHO


By Author

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post