CHANJO YA CORONA YAMUIBUA MGEJA..AMPONGEZA RAIS SAMIA KURUHUSU WATANZANIA KUCHANJWA,WANAOPOTOSHA WAKAE KIMYA |Shamteeblog.



Mwenyekiti wa Taasisi ya Tanzania Mzalendo Foundation ya Mjini Kahama mkoani Shinyanga, Khamis Mgeja akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) jana ofisini kwake muda mfupi baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuzindua chanjo ya kinga ya ugonjwa wa Covid 19 (Picha na Suleiman Abeid)

**
Na Suleiman Abeid,TimesMajira Online,Shinyanga

TAASISI ya Tanzania Mzalendo Foundation yenye Makao Makuu yake wilayani Kahama mkoani Shinyanga imempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake wa busara wa kuruhusu watanzania kupatiwa chanjo ya kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa Covid 19.

Pongezi hizo zimetolewa jana na Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi hiyo, Khamis Mgeja katika maongezi yake na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kahama muda mfupi baada ya Rais Samia kuzindua rasmi chanjo Covid 19.

Mgeja amesema kitendo cha Rais Samia kinastahili kupongezwa na kila mtanzania mwenye mapenzi mema na nchi yake na kwamba hatua hiyo itanusuru maisha ya watanzania wengi watakaokubali kuchanjwa chanjo hiyo japokuwa wapo wachache wanaopingana na msimamo huo wa Serikali.

“Nichukue fursa hii kumpongeza Rais Samia kwa uamuzi wa kuruhusu chanjo ya kinga ya Corona kuingizwa hapa nchini, na ameonesha njia kwa yeye mwenyewe kuanza kuchanjwa chanjo hiyo na ameifanya nchi yetu iwe miongoni mwa mataifa mengine duniani yanayowajari wananchi wake,”

“Pia nawapongeza wadau wengine wote walioungana na Rais wetu ikiwemo viongozi wa madhehebu ya kidini katika kujitokeza kuchanja chanjo hii, hili suala linagusa hatima ya maisha yetu, kila anayejisikia ni muhimu akachanjwa maana Rais kaisha onesha njia,” ameeleza Mgeja.

Hata hivyo Mwenyekiti huyo ambaye pia amewahi kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Shinyanga ametoa wito kwa watanzania ambao bado wanatoa maneno ya upotoshaji kuhusiana na chanjo hiyo ya kinga ya Covid 19 wakidai haifai na ina madhara.

Amefafanua kuwa ni vyema watu wanaotaka kupotosha ukweli wakakaa kimya badala ya kuendelea kuwapotosha watu kwa maneno yasiyokuwa ya kitaalamu ambapo ameiomba Serikali iharakishe kusambaza chanjo hiyo katika mikoa yote nchini ili watu waweze kuchanjwa.

“Jambo hili ni la hiari basi, hawa wanaotaka kupotosha tunawaomba wakae kimya, suala hili ni la kihiari, ni muhimu watu waendelee kushauriwa wajitokeze kuchanjwa, na sisi huku mikoani tunasubiri chanjo hii ifike haraka mikoani na mawilayani ili watu waweze kuchanjwa,”

“Hawa wanaopinga ni vyema sasa wakatupa mbadala wa kitaalamu tutumie njia gani katika kujikinga na ugonjwa huu, na jambo hili ni la hatari kuona watu wasiokuwa na utaalamu wa kidaktari ndiyo wanaosimama kidete kupinga, na watuoneshe kwa vigezo kwa nini chanjo hii haifai,” ameeleza.

Vilevile amewataka watu hao wanaoupinga msimamo wa Serikali wakaacha mambo ya kitaalamu yasemewe na watu wenye utaalamu wa masuala ya kiafya, suala la kitaalamu lisiingizwe kwenye siasa na wanasiasa waachiwe wafanye kazi zao za kisiasa.

Mgeja ameonesha kushangazwa na kitendo cha wanasiasa kuingilia masuala ya kitaalamu kwa kuukataa ukweli na kuupinga ambapo amehoji ni vipi upande wa wataalamu hawaingilii masuala ya kisiasa ambapo alisema upotoshaji wao unaweza kuliingiza Taifa la Tanzania katika matatizo makubwa.

“Vilevile nichukue fursa hii kuwapongeza viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama hapa nchini na viongozi wote wa kidini na wale wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa jinsi walivyoonesha msimamo mzuri katika kuunga mkono maamuzi ya Serikali kuhusiana na janga la ugonjwa wa Covid 19,”

“Niwaombe tu watanzania hivi sasa tupo kwenye janga zito na tukifanya mizaha tunaweza kuteketeza maelfu ya watanzania kwa jambo ambalo linaweza kuzuilika mapema kabla halijatuletea madhara makubwa, wakumbuke ule usemi wa “….Akili za kuambiwa changanya na za kwako, watauona ukweli na msimamo wa Rais Samia,” ameeleza Mgeja.

Rais Samia Suluhu Hassan jana amezindua rasmi chanjo ya kujikinga na ugonjwa wa Covid 19 ambapo alisema japokuwa wapo baadhi ya watanzania wanaopinga chanjo hiyo lakini wengi wao wanaunga mkono na kwamba Serikali itahakikisha wale wote wanaotaka kuchanjwa wanachanjwa.


By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post