Charles James, Michuzi TV
CHAMA Cha Walimu Tanzania (CWT) kimewataka Walimu nchini kufanya kazi zao kwa weledi na uaminifu ili kuondoa tabia ya kuletwa kwa Askari Polisi na Migambo kuwasimamia wakati wanapokua wanasimamia mitihani mikubwa ya kitaifa.
Kauli hiyo imetolewa jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa CWT, Deus Seif kwenye kongamano lililoandaliwa na Chama Cha Walimu Wanafunzi Chuo Kikuu Cha Dodoma (UDOSTA).
Seif amesema kukosekana kwa uaminifu, weledi na ongezeko la utandawazi pamoja na kizazi cha digitali ndio sababu inayochangia Serikali kutumia Vyombo vya Dola kuwasimamia Walimu wanaosimamia mitihani hiyo kwenye chumba cha mitihani.
Amesema kama hali hiyo ya kukosekana kwa uaminifu itaendelea kuwepo haitoshangaza kuona Serikali inawapeleka wanajeshi kwenda kusimamia mitihani jambo ambalo litakua ni fedheha na aibu kwa kada ya ualimu na hivyo kushauri mabadiliko ndani yao ni lazima yawepo ili kuilinda kada yao.
" Ni lazima turejeshe nidhamu ambayo ilikuepo kwenye kada hii miaka ya nyuma, zamani Mwalimu alikua anachukuliwa popote kwa sababu alionekana ni mwaminifu, Sasa hivi sisi wenyewe tunaletewa Askari wa kutusimamia, ni lazima tubadilike, tujikosoe ili Imani ya Serikali na jamii irudi tena kwetu.
Kitendo cha Walimu kukosa uaminifu, kuvunja maadili na taratibu za utendaji wetu kinatutia aibu sisi wenyewe na kinatia dola taaluma yetu, na niwasihi Walimu kubadilika na kurejea kwenye miiko na maadili ya kazi yetu," Amesema Seif.
Amesema ni vema walimu watambue kuwa vitendo vya Askari kusimamia mitihani huwapa wanafunzi hofu ambayo muda mwingine huwasababishia wafanye vibaya na hivyo kuwataka walimu kurejea kwenye miiko na maadili yao ili kusiwe na kuletwa kwa Askari kwenda kusimamia mitihani.
Seif pia amesema CWT imeendelea kuwa chombo imara na madhubuti cha kutetea maslahi ya Walimu nchini na kwamba hadi sasa imefanikiwa kushinda asilimia 89 ya kesi zinazohusiana na madai na mashauri ya Walimu.
Akisoma risala ya UDOSTA, Katibu Mkuu wa Chama hicho, Emmanuel Mwangoka ametoa ombi kwa CWT kuhakikisha inaendelea kupambana kwa kushauriana na kuihimiza Serikali kuhusu upatikanaji wa ajira za walimu nchini lakini pia kuweka mazingira wezeshi ya Vijana kujiajiri wakati wakisubiri ajira za kudumu kutoka serikalini.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT), Deus Seif akizungumza kwenye kongamano lililoandaliwa na Chama Cha Walimu Wanafunzi Chuo Kikuu Cha Dodoma ( UDOSTA) jijini Dodoma.
By Mpekuzi
Post a Comment