Kigamboni Yakabidhiwa Mradi Wa Viwanja 20,000 |Shamteeblog.

 


 Na Munir Shemweta, WANMM

Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia ofisi ya Kamishna wa Ardhi mkoa wa Dar es Salaam imekabidhi mradi wa viwanja 20,000 kwa halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni iliyopo mkoani Dar es Salaam ili iweze kusimamia na  kuendeleza eneo la mradi.


Hatua hiyo inafuatia maagizo ya Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi kutaka manispaa ya Kigamboni kukabidhiwa mradi huo ili kutunza eneo la mradi kwa mujibu wa mipangomiji ya wilaya ya kigamboni.


Akizungumza wakati wa kukabidhi mradi huo wa viwanja 20,000 tarehe 2 Julai 2021 Dar es Salaam kwa Mstahiki Meya ya Manispaa hiyo Ernest Mafimbo, Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Dar es Salaam Idrisa Kayera alisema, lengo la kukabidhi mradi ni kutaka manispaa ya kigamboni itunze eneo la mradi kwa mujibu wa mipangomiji sambamba na kuzuia uvamizi wa eneo hilo.


Kwa mujibu wa Kayera, awali eneo la viwanja 20,000 katika manispaa hiyo kulikuwa na changamoto mbalimbali kama vile uvamizi wa maeneo ya wazi na kubainisha kuwa, kutokana na mamlaka ya upangaji kuwa chini ya halmashauri wizara imeona ipo haja ya kukabidhi mradi huo kwa halamshauri.


"Wizara imeona ikabidhi mradi huu kwa kuwa halmashauri ina nafasi nzuri ya kusimamia mipangomiji pamoja na kuendeleza miundo mbinu ambapo awali jukumu hilo lilikuwa likifaywa na wizara na tuzingatie mamlaka ya upangaji iko chini ya halmashauri" alisema Kayera.


Maeneo ambayo mradi wa viwanja 20,000 upo katika halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni unaohusisha viwanja 15,000 vilivypo Gezaulole, Vijibweni, Muongozo, Kibada na Kisola.


Kwa upande wake meya wa manispaa ya Kigamboni Ernest Mafimbo mbali na kuishukuru wizara kwa kuwapatia mradi huo, alitaka kuwepo kwa hati ya makubaliano  ya mradi kati ya  Wizara na Manispaa ya Kigamboni ili kuwa na ufanisi wakati wa usimamizi na kuendeleza mradi huo kwa maslahi ya wananchi wa kigamboni.


"Sisi tumefurahi kukabidhiwa huu mradi maana utatusaidia sana kama manispaa hata kupata mapato na tutautumia kwa maslahi ya manispaa ya kigamboni" alisema Mafimbo.


Mwenyekiti wa Kamati ya Mipangomiji kwenye halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni Sanya Bunaya ambaye ni Diwani wa Kimbiji alisema, pamoja na manispaa kuupokea mradi huo lakini kuna wasiwasi wa kuibuka changamoto kutokana na kubadilika kwa msimamizi wa mradi na kushauri kuainishwa wazi kwa maeneo ya fidia na migogoro mingine ili manispaa ijue.


Hata hivyo, Kamishna Kayera alimtoa wasiwasi kuhusiana na suala la fidia katika maeneo ya mradi kwa kuekeza kuwa suala hilo kama wizara walishalifanyia kazi kwa kuwa wizara ya Ardhi ilipata mkopo kwa ajili ya wamiliki wote waliokuwa wakidai fidia na kusisitiza kuwa halmashauri ya kigamboni inachotakiwa sasa  kuhakikisha maeneo ya mradi huo hayavamiwi  na yanalindwa.



from Author

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post