Watumishi tisa wamesimamishwa kazi katika Kitengo cha upimaji wa COVID - 19 kwa wasafiri katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kwa kosa la kutokufika kazini kutoa huduma ya vipimo hivyo kwa wasafiri bila taarifa.
Agizo hilo limetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Prof. Abel Makubi, alipofanya ziara uwanjani hapo kwa ajili ya kukagua utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa juzi alipofika hapo akiwa ameambatana na Katibu mwenzake wa Wizara ya Uchukuzi.
"Jana watumishi wanane hawakufika na leo mmoja bila kutoa sababu ya msingi, jumla wanakuwa tisa, imeonekana hapa hili zoezi la baadhi ya watumishi kutokuja kazini limekuwepo, sasa hii imenisikitisha sana kwa baadhi ya viongozi kushindwa kuchukua hatua zinazostahili na kulindana kwa kuficha uozo," amesema Profesa Makubi.
"Kwahiyo hawa ambao hawakufika jana na kati yao wanne walikuwa wameajiriwa na Wizara ya Afya na wanne wameajiriwa na Manispaa ya Dar es Salaam, nimeagiza hawa walio chini ya Wizara ya Afya wasimame kufanya kazi ili tufanye uchunguzi na kuchukua hatua stahiki na ambao wameajiriwa na Ofisi ya RAS nitashauri mamlaka husika nao wachukuliwe hatua hivyo hivyo ambazo zimechukuliwa kwa hawa wa Wizara," ameelekeza Profesa Makubi.
from Author
Post a Comment