Majaliwa: Wizara Ya Kilimo Hakikisheni Ushirika Unakuwa Endelevu |Shamteeblog.
Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Kilimo isimamie kikamilifu changamoto mbalimbali zinazodumaza vyama vya ushirika nchini ili kujenga ushirika imara unaokuwa na endelevu.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa ameiagiza wizara hiyo ihakikishe inavijengea vyama vya ushirika uwezo wa kujiendesha kiushindani na kuimarisha utafutaji wa masoko ya ndani na nje.
Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo jana (Jumamosi, Julai 3, 2021) kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani yaliyofanyika Kitaifa katika viwanja vya lipuli, Tabora.
Amesema ushirika ni chombo ambacho kinajenga imani kwa wakulima na wanaushirika na kwa kuwa Serikali inaweka nguvu katika jambo hilo kwa lengo la kuona ushirika unaleta manufaa.
“Natambua kuwa ushirika ndicho chombo madhubuti cha kuwauunganisha wakulima, wafugaji na wavuvi na kuwapa uwezo na nguvu ya kutatua matatizo yao ya kiuchumi na kijamii.”
Amesema wizara hiyo inatakiwa iimarishe usimamizi na udhibiti wa vyama hivyo sambamba na kuviwezesha kusimamia mifumo rasmi ya masoko ukiwemo wa Stakabadhi ghalani.
Amesema utoaji wa elimu na mafunzo ya ushirika kwa wanachama, viongozi na watendaji ni vema ukaimarishwa ili waweze kuelewa vizuri dhana ya ushirika, misingi, kanuni na taratibu.
Kadhalika, Waziri Mkuu ameliagiza Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) libadilishe mfumo wa ukaguzi na lihakikishe linatoa taarifa sahihi kwa wakulima.
Waziri Mkuu amesema katika mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika imefanya ukaguzi wa ndani wa vyama vya ushirika 4,494 kati ya 9,185.
Pia, Waziri Mkuu amewataka Warajisi wote wahakikishe kila ushirika katika maeneo yao unakuwa na kanzi data za wanaushirika wote. “Lazima uwe na takwimu za wanaushirika wote.”
Amesema lengo la kuwa na takwimu hizo ni kuweza kufanya makadirio ya kupeleka mahitaji mbalimbali kwa wakulima ikiwa ni pamoja na mbegu, mbolea na dawa za kuulia wadudu.
Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Prof. Adolf Mkenda ametumia fursa hiyo kumpongeza Mheshimiwa Majaliwa kwa jitihada zake za kufufua na kuendeleza vyama vya ushirika nchini.
“Wewe binafsi Mh. Waziri Mkuu umesimamia shughuliza ushirika kwa moyo mmoja. Umetusaidia kurudisha mali za vyama vya ushirika ambazo zilitoka kinyume na utaratibu.”
“Kwa juhudi hizi Mhe. Waziri Mkuu umetusaidia sana kurudisha imani kwa wana-ushirika kwamba wakiwa kwenye ushirika mali zao haziwezi kufanyiwa ubadhilifu wa aina yoyote.”
Waziri huyo ametaja vyama ambavyo Mheshimiwa Waziri Mkuu alisimamia urejeshwaji wa mali zake kuwa ni pamoja na mali za NCU-Mwanza, SHIRECU-Shinyanga, KNCU, KCU.
Pia, Waziri huyo amemuahidi Waziri Mkuu kwamba wataendelea kusimamia ushirika nchini na kuhakikisha unaendeshwa kwa weledi, uwajibikaji na uwazi ili watu wengi wapende kujiunga.
(Mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
By Author
Post a Comment