Mbunge wa Morogoro Mjini (CCM), Abdulaziz Abood
Na Mwandishi Wetu
MBUNGE wa Morogoro Mjini kupitia chama cha Mapindu (CCM) Abdulaziz Abood, amepongeza kazi kubwa iliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan ndani ya siku 100 akiwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa ni ya kipekee.
Akizungumza leo Julai Mosi, 2021 Abood amesema ndani ya siku 100 Rais Samia ameonyesha mwelekeo sahihi wa nchi kwa jitihada zake za kufungua milango ya uchumi na kuimarisha mifumo ya serikali.
Amesema kama Rais Samia ameweza kufanya mambo makubwa kama haya ndani ya siku 100 basi watanzania watarajie mambo makubwa mazuri siku za usoni na wampe ushirikiano ili aweze kutimiza malengo yake.
"Tumepata kiongozi mwenye maono, mwadilifu na mchapakazi ambaye ataijenga nchi hadi kufikia uchumi wa juu kinachotakiwa ni kumpa nafasi na ushirikiano ili atimize ndoto zake" alisema Abood
Abood amesema Rais Samia ni mtulivu, msikivu na anayejali utawala wa haki, demokraaia na utawala wa sheria wenye mwelekeo ambao umewavutia watanzania wengi wa rika zote.
"Hakika Tanzania imempata kiongozi ambaye atailetea maendeleo makubwa kutokana na kufanya vyema ndani ya kipindi kifupi cha siku 100...,tumeshuhudia namna ambavyo amekuwa na upendo kwa kukaa na kuzungumza na makundi mbalimbali kama wazeee, vijana, wanawake na viongozi wa dini hii inatupa dalili njema kwamba kiongozi tuliye naye ni sahihi. 'Alisema Abood
Ameongeza kuwa watanzania wa rika mbalimbali wamepongeza siku 100 za Rais Samia madarakani hali inayoonyesha kwamba kiongozi huyo anaungwa mkono na asilimia kubwa ya watu.
Amesema hatua ya Rais Samia kushirkisha kwa karibu sekta binafsi kwa kuvutia uwekezaji mpya kutafungua milango ya uchumi kwa haraka sana na kudai kuwa mwelekeo huo mpya wa serikali yake kuondoa urasimu kwenye sekta binafsi kumesababisha mafuriko ya wawekezaji ndani ya muda mfupi.
"Ninachosisitiza tumpe nafasi na tumpe ushirikiano ili atimize majukuku yake, kuna miradi mingi ya kimkakati inaendelea na chini ya usimamizi wake mahiri nina imani kubwa kwamba itamalizika kwa wakati." amesema Abood
By Mpekuzi
Post a Comment