· Alifuatilia kwa kina ujenzi wa Daraja la Mkapa
· Waandisi Walimpa jina ‘Injinia wa Projekti’
Na: Lillian Shirima – MAELEZO
Ni mwaka mmoja sasa tangu tulipoondokewa na mpendwa wetu Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa T anzania Awamu ya Tatu Hayati Benjamin Wiliam Mkapa aliyefariki usiku wa kuamkia Julai 24, 2021 Jijini Dar es Salaam
Wakati tunaathimisha kumbukiza ya maisha yake, Wahandisi Kitainda Michael – Head of Consultancy Services (Mkuu wa Huduma za Ushauri) na Mohamed Ntunda, Mkurugenzi wa Matengenezo ya Barabara TANROADS ni miongoni mwa wahandisi waliosimamia ujenzi wa Daraja la Rufiji sasa Daraja la Mkapa wameeleza namna ambavyo Hayati Benjamin Mkapa alivyokuwa akifuatilia kwa karibu ujenzi wa daraja hilo kiasi cha kupewa jina la Injinia wa Projekti.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Habari MAELEZO Jijini Dar es Salaam, Mhandisi Kitainda amesema kwamba, Hayati Rais Mkapa alikuwa kiongozi asiyechoka kufuatilia jambo lenye maslahi kwa wananchi na kwamba mara kwa mara alifika eneo la mradi kujua hatua zote za maendeleo ya mradi na kwamba alipenda kuwasikiliza na kutatua changamoto walizokutana nazo wakati wa ujenzi.
‘Mkapa alikuwa anatembelea eneo la kazi mara kwa mara na kila wakati alipofika kuna kitu utajifunza kutoka kwake, alifuatilia kipindi chote cha ujenzi hadi akaitwa Injinia wa Projekti, alitutoa hofu na kutupa ujasiri wa kuendelea na kazi hata tulipokwama aliingilia kati na kusaidia na sisi tulifanya kazi kwa bidii’, alisema Mhandisi ...
Aidha Mhandisi Kaitanda amesema, Hayati Mkapa alikuwa kiongozi aliyebeba maono makubwa, mwenye kutoa hamasa na matumaini kwa wengine kwa kuwaonesha kitu ambacho hawakukiona na aliwapa matumaini kwamba hakuna kisichowezekana.
Alitambua kwamba, kwa miaka mingi uchumi katika mikoa ya kusini mwa nchi ambayo ni Mtwara na Lindi ilikuwa imelala na kwamba ili kujenga uchumi wa Taifa suala la matumizi ya ardhi halinabudi kupewa kipaumbele, hivyo alipoingia madarakani alianzisha taasisi nyingi nchini ikiwemo Wakala wa barabara Tanzania (TANROADS), wahusika wakuu wa ujenzi wa Daraja la Mkapa.
Kabla ya ujenzi wa daraja hilo Mhandisi Kaitanda ameelezea adha walizokutana nazo wananchi hadi kupoteza maisha ni pamoja na kushindwa kuvuka Mto Rufiji kwenda ng’ambo ya pili kufuata huduma kutokana na mto huo kujaa maji pamoja na mamba wengi hususan wakati wa masika.
‘Mara kadhaa kivuko kilikwama kwenye matope kwa siku zisizotabirika na kusababisha msongamano mkubwa wa magari, wanafunzi walitaabika kwa kukosa chakula kwa siku kadhaa na hawakujua lini watanasuliwa na kuweza kuendelea na safari’ anafafanua Mhandisi Kaitanda
Changamoto haikuwa hiyo pekee, akina mama wajawazito waliteseka kwa kusoka huduma za uzazi, wapo waliojifungua njiani, wengine walipoteza maisha yao na ya watoto, hata vitendo vya ukatili wa kijinsia vilikuwa vinafanyika.
Anasema kwamba, kutokana na kukosekana kwa miundombinu imara hususan daraja na barabara, suala la usafiri na usafirishaji wa bidhaa katika mikoa hiyo ya kusini lilighubikwa na changamoto lukuki na hivyo kusababisha gharama za maisha kuwa juu ambapo bidhaa kama sukari ilipanda mara tano ya bei iliyokuwepo wakati huo.
‘Hapakuwa na watu wenye maono ya shughuli za kiuchumi kwa sababu ya kukosa mawasiliano, hakuna masoko, Mfanyakazi wa serikali akipata uhamisho kwenda mikoa ya kusini utasikia watu wakiuliza amekosa nini, ilikiwa ni kama adhabu’.
Akielezea historia ya ujenzi wa daraja hilo Mhandisi Kaitanda alisema, ikumbukwe kwamba mwaka 1974 mikoa ya kusini ilikumbwa na mafuriko makubwa yaliyoharibu makazi ya watu ambapo Serikali ililazimika kuhamisha watu waliokuwa wakiishi bondeni kwenda kijiji ambacho sasa kinaitwa Ikwiriri.
Tukio hilo lilisababisha Serikali kutafuta ufumbuzi wa changamoto ya mafuriko ya mto Rufiji hata ilipofika mwaka 1995 mchakato wa kujenga daraja la kudumu ulipamba moto ambapo daraja hilo lenye urefu wa mita 970 lilianza kujengwa kwa gharama ya fedha za kimarekani dola Milioni 30 ambazo ni fedha za wahisani kutoka OPEC, Kuwait na Serikali ya Saudia Arabia.
Daraja hilo lililopo mkoa wa Pwani wilaya ya Ikwiriri na limejengwa kuvuka Mto Rufiji likiunganisha Pwani na Mikoa ya Lindi na Mtwara ni miongoni mwa alama alizotuchia Hayati Mkapa, lilifunguliwa Agosti 2, 2003.
Tangu kukamilika kwa ujenzi wake shughuli za kiuchumi na kijamii zimeendelea kukua kwa ufanisi. Mathalan, usafirishaji wa mizigo na bidhaa zake umekuwa wa hakika na rahisi hivyo wananchi wananufaika kwa kununua kwa bei nafuu, uwekezaji mkubwa wa viwanda kama vile Kiwanda cha Saruji cha Dangote kimetengeneza ajira kwa wakazi wa Mtwara na mikoa mingine.
Kugunduliwa kwa gesi asilia kumechochea kuongezeka kwa kasi ya ujenzi wa viwanda ambapo wawekezaji wamewekeza katika sekta mbalimbali ikiwemo hoteli na taasisi za kifedha. Kadhalika kukua kwa kilimo cha zao la korosho kumebadilisha maisha ya wakulima katika mikoa hiyo ya kusini.
Mhandisi Kitainda anaweka wazi kwamba ataendelea kumkumbuka Hayati Mkapa kwa kuanzisha Tanroads ambapo mikoa imepewa mamlaka ya kiutendaji hali inayoongeza ufanisi wa kazi kwenye usimamizi, maamuzi na mgawanyo wa majukumu kiutendaji.
"Kabla ya TANROADS kazi zote za kihandisi ziliratibiwa na ofisi kuu ya ujenzi hali iliyosababisha kuzorota kwa kazi, sasa hivi Meneja wa mkoa Tanroads anaweza kusimamia vizuri barabara na madaraja ya mkoa wake kila siku’ alifafanua zaidi.
Naye Mkurugenzi wa Matengenezo ya Barabara Tanroads Mhandisi Mohamed Ntunda amesema, licha ya kwamba Mkapa alikuwa na shauku na miradi ya kusini (Mtwara Corridor) na kwamba mradi wa Daraja la Mkapa ni sehemu ya miradi ya kimkakati.
Amesema, Hayati Mkapa ni kiongozi aliyesisitiza suala la uwajibikaji katika kazi jambo lililosababisha ufanisi katika ujenzi wa daraja hili.
"Daraja halijawahi kufanyiwa matengenezo isipokuwa yale kidogo katika barabara zinazounganisha daraja hilo" amesema Mhandisi Ntunda.
Hayati Mkapa ni Kiongozi aliyekuwa na dhamira ya kujenga mazingira yatakayomwezesha mwananchi kuendesha shughuli zake za kiuchumi kwa faida yake binafsi na maendeleo ya Taifa. Kumuenzi Hayati Mkapa ni kuwa wazalendo kwa Taifa letu, kuwajibika katika kazi, na kuweka maslahi ya Taifa mbele.
By Mpekuzi
Post a Comment