Na Said Mwishehe, Michuzi TV
WADAU zaidi ya 25 kutoka jamii za kiraia, wasomi,wanasheria na vyombo vya habari wamekutana jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuujadili na kuuchambua kwa kina Muswada wa Haki za Digitali na Uhuru nchini Tanzania katika kutimiza sheria zilizopo za kimtandao.
Majadiliano hayo ambayo yamefadhiliwa na kuratibiwa na Shirika lisilo la kiserikali la Paradigm Initiative ambalo ofisi zake ziko Kamerun, Kenya, Nigeria, Senegal, Zambia, Zimbabwe na kwingineko.Wamekuwa wakifanya kazi kuunganisha vijana wa kiafrika wasio na huduma na maisha bora kupitia ujumuishaji wao wa digitali na mipango ya haki za digitali.
Aidha wakati majadiliano hayo yakifanyika nchini Tanzania kwa njia ya kidigitali katika Jiji la Dar es Salaam kwa kuwakutanisha wadau hao, Muswada kama huo majadiliano yake yamekuwa yakiendelea hivi sasa katika nchini za Kameroon, Malawi, Zambia na nchi zingine za Afrika.
Akizungumza kutoka nchini Kenya kwa njia mtandao, Mratibu Mkuu wa Mradi Afrika Mashariki wa Paradigm Initiative Ekai Nabenyo amewaambia wadau walioko walishiriki majadiliano hayo yaliyofanyika kwa siku mbili jijini Dar es Salaam kuwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, juhudi hizo zilianza mwaka 2020.
Amesema na ni matumaini yao kuwa utawala mpya wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan na kwa msaada wa wadau tofauti na Watanzania wote, mapendekezo yaliyomo katika Muswada huo yatatoa mwangaza kwa siku za usoni na hatimaye kuwa na sheria zenye kulinda haki za digitali zikiwemo na falagha na uhuru wa mtumiaji bila kuvunja sheria za nchi.
"Tunakumbuka pia tayari kuna majadiliano nchini Tanzania kuhusu sheria ya faragha na tunawasihi Watendaji na Bunge kuharakisha mchakato wa sheria kama hizo kuhakikisha usalama wa data na haki za dijiti kati ya Watanzania wote.Kama Shirika la haki za digitali za Pan-Afrika, tumekuwa mstari wa mbele kukuza ushirikiano kati ya Serikali na asasi za kiraia barani Afrika. Ushirikiano kama huo ulisababisha kuanzishwa kwa Muswada wa Haki za Digitali na Uhuru nchini Nigeria.
"Ni imani yetu thabiti kwamba mengi yanawezekana wakati raia, asasi za kiraia, na serikali inafanya kazi pamoja katika kuunda siku zijazo, kupitia hatua za sera zinazounga mkono uvumbuzi na kulinda watu-kama vile Muswada wa Haki za Digitali na Uhuru wa Tanzania, 2021.
"Shirika letu pamoja na washirika wa ndani wataendelea kuwashirikisha wabunge na maofisa wa Serikali kujadili njia ambazo tunaweza kushirikiana kutunga Muswada huu kuwa sheria. Timu yetu ya wadau wa haki za Digitali inayotolewa kutoka kwa wanasheria, wasomi, asasi za kiraia.
"Vyombo vya habari na maofisa wa Serikali watashirikiana kuunga mkono Muswada huu na kutoa mwongozo unaohitajika wakati wa michakato ya ushiriki wa umma. Mpango wa Paradigm unawataka watanzania wote kuunga mkono Muswada huu na kuchangia kwa nafasi zao wakati wa michakato ya ushiriki wa umma itakayoanzishwa na Bunge la Tanzania na idara ya Serikali inayohusika,'amesema Nabenyo.
Pia amesema anatambua umuhimu wa Muswada huo, hivyo hana mashaka ushiriki wa Watanzania katika kuujadili utakuwa mkubwa na ni matamanio yao kuona kila mwananchi anapata nafasi ya kutoa maoni yake na majadliano ambayo yamefanywa na wadau walioko jijini Dar es Salaam ni hatua ya mwanzo tu, hivyo ndio kwanza kazi ya kuujadili Muswada huo imeanza.
Awali Mwezeshaji wakati wa Kongamano la kujadili Muswada huo ambaye pia ni Mratibu Mwandamizi Peter Mmbando amesema Muswada huo ni muhimu na umekuja wakati muafaka hasa kwa kuzingatia kumekuwepo na matumizi makubwa ya mtandao katika kufanya shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Amesema lazima kuwepo na miongozo ambayo itawafanya watumiaji mbali ya haki zao kulindwa wajue ni aina gani za maudhui ambazo wanaweza kuweka mtandaoni bila kuvunja sheria."Ukiangalia nchi nyingi katika kipindi hasa cha janga la Corona tumeishi maisha ya kidigitali, taarifa za kidigitali, watoto na wanafunzi wanaishi kidigitali kwa maana ya kusomea mtandaoni.
"Haki na maudhui ambayo yatatumika yanalindaje utamaduni wetu?Yanalindaje masuala mazima ya maisha kwa pamoja, tusije tukaingiza vitu ambavyo havitakiwi katika nchi yetu, tunahitaji tuendeleze utamaduni wetu na tulinde haki za kidigitali za watu wote ili katika uchumi wa kidigitali tuweze kuendana na mahitaji ya kidunia lakini kuna vitu vya msingi vya kuviangalia na hasa vinavyoendana na usalama katika nchi yetu , kanda yetu na Afrika kwa ujumla.
"Kwa hiyo tumekuwa na siku nzuri katika majadiliano haya yaliyofanyika kwa siku mbili ,tumejadili na kuona ni mchakato huu wa Muswada umeanzia chini lakini kadri unavyoendelea kujadiliwa itapatikana katika makundi ya watu mbalimbali na mwisho wa siku tuwe na kauli moja kuanzia ngazi ya chini hadi kitaifa,'amesema Mmbando.
Wakati huo huo Wakili Salma Kassim kutoka Infinity Excellence Ltd amesema Muswada huo ukijadiliwa na ukapita kuwa Sheria utasaidia ulinzi wa haki za mtumaji wa mtandao lakini utatengeneza wajibu kwa mtumiaji wa mtandao kulinda na kuheshimu usiri wa mtu mwingine.
Aidha amesema kuna umuhimu wa kutolewa elimu kwa jamii kujua wanatakiwa kufanya vitu gani wakiwa mtandaoni na hawatakiwi kufanya vitu gani wakiwa mtandaoni huku akieleza changamoto kubwa kwa vijana wanaotumia mitandao ya kijamii wengi wao wanashindwa kuitumia kama sehemu ya kukuza uchumi wao na badala yake wamekuwa wakihangaika kuangalia mambo yasiyokuwa na tija kwao.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Henry Victor amesema kupitia majadiliano ya Muswada huo ambao wadau wameujadili ni matumaini yake kuna siku utapitishwa hasa kwa kuzingatia kuna haki za raia na Muswada huo unakwenda kuwasaidia wananchi kujua haki zao wa muda gani wa kuweka vitu vyao mtandaoni.
Wakati huo huo Ofisa Uhusiano na Mawasiliano wa Jukwaa la Utu wa Mtoto(CDF) Celina Baragwiha amesema anatamani kuona Musawada huo unakuwa na kipengele ambacho kitazungumzia kwa kina kuhusu haki za mtoto hasa kwa kuzingatia kumekuwepo na udhalilishaji mkubwa wa watoto mtandaoni aidha kwa picha au video zinazowekwa.
"Asasi yetu imejikita zaidi katika haki za mtoto kwa kutambua changamoto nyingi wanazopitia na ni kundi ambalo limetengwa kwasababu tofauti na baadhi ya watu, leo katika siku mbili ambazo tuko hapa tunazungumzia Muswada ambao unakwenda kuzungumzia haki za mtumiaji mtandao haki zake zikoje.Tukiangalia hata watoto wanatumia mitandao ya kijami kujifunza kwa kutumia simu, laptop na kompyuta.
"Lakini je tunafahamu kama wazazi na walezi kunachangamoto ambazo watoto wanazipitia , kwa hiyo katika huu Muswada ni vema kukawa na kifungu kwa ajili ya kuwalinda watoto wanaotumia mitandao hiyo.Kuna watoto wengi wanadhalilishwa mtandaoni , picha zao zinasambaa wakiwa utupu au wanashinikizwa kutumikishwa kingono.kwa hiyo naangalia huu Muswada kwa namna gani utamlinda mtoto anayetumia mitandao ya kijamii."amesema.
By Mpekuzi
Post a Comment