Pwani Na Dar Es Salaam Zaongoza Uvamizi Wa Ardhi |Shamteeblog.
Na. Hassan Mabuye, Pwani
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi amesema mkoa wa Pwani na Dar es salaam kwa sasa ndio inaongoza kwa uvamizi wa ardhi za watu kwa kutumia nguvu kinyume na utaratibu.
Waziri Lukuvi ameyasema hayo jana wakati wa uzinduzi wa kampeni maalumu ya kusikiliza, kutatua na kutokomeza kabisa migogoro ya ardhi kwa mkoa wa Pwani katika mkutano uliyofanyika ofisi ya mkuu wa mkoa Pwani na kuhudhuriwa na Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa.
“Hii mikoa miwili ya Pwani na Dar es salaam inaongoza kwa uvamizi wa ardhi na matumizi ya nguvu katika kujimilikisha ardhi za watu wanaomiliki kihalali. Watu wanatoka Dar es salaam wanakuja mkoa wa Pwani kuchukua ardhi za watu na kudai kumilikishwa” Amesema Waziri Lukuvi.
Ameongeza kuwa Mkoa wa Pwani ni eneo muhimu sana kwa uwekezaji kwa hiyo haiwezekani kuwaachia watu kuvamia maeneo ya viwanda, mashamba, maeneo ya umma na maeneo ya wazi ambayo yapo kisheria.
Waziri Lukuvi amemtaka kila mkuu wa wilaya aitambue migogoro ya ardhi katika maeneo yake, awe na taarifa ya kina ya kila mgogoro na atengeneze daftari la migogoro ya ardhi kwa kushirikiana na wataalamu wa ardhi katika kuitatua na kama kuna afisa ardhi sio muadilifu aletwe kwake ili amchukulie hatua.
Katika hatua nyingine Waziri Lukuvi amesema Wakurugenzi ndio wenye mamlaka ya upangaji wa miji, kama wataruhusu utendaji mbovu wa sekta ya ardhi katika halmashauri zao, watawajibika kwa kuwa katika sheria ya ardhi wao ndio wasimamizi wakuu wa sekta ya ardhi.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakar Kunenge ambaye ndiye aliyezindua rasmi Kampeni ya kushughulikia Migogoro ya Sekta ya Ardhi Mkoani Pwani ameeleza kuwa watafanya ziara na Mhe. Waziri wa Ardhi katika Wilaya za Kibaha, Bagamoyo, Mafia, Mkuranga, Rufiji na Kibiti kuanzia Tarehe 14 Julai, 2021 hadi Tarehe 22 Julai 2021 kushughulikia na kutatua Migogoro ya Ardhi.
Kunenge, amewataka Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wote Mkoa wa Pwani kuhakikisha wanatumia nafasi zao katika kutatua migogoro ya Ardhi katika maeneo wanayoyaongoza.
Kunenge pia amewataka Viongozi hao wa Mkoa wa Pwani kuhakikisha wanaboresha Daftari la makazi na kuhakiki idadi ya mifungo iliyopo mkoani Pwani ili kuepukana na Migogoro ya Ardhi.
Katika hatua Nyingine Kunenge amesema kuwa hatosita kumchukulia hatua kali za kisheria kwa yeyote yule atakaefanya uvamizi wa aina yoyote katika mkoa wa Pwani.
“Sheria zipo wazi watu wanavamia lakini hawachakuliwi hatua, hivyo sasa tutachukua hatua kali hatutaonea mtu ila tutatenda haki” alisema Kunenge.
Aidha, Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Pwani Bibi. Lucy Kabyamela amesema kwamba wakazi wengi wa mkoa wa Pwani wamekuwa na kasumba ya kuamini kwamba mtu kumiliki ardhi kubwa kisheria ni makosa, ndio maana wanavamia maeneo ya watu na kujigawia kwa nguvu.
By Mpekuzi
Post a Comment