Rais Samia Aipongeza Burundi Kwa Kuadhimishaa Miaka 59 Ya Uhuru |Shamteeblog.


 RAIS wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amewapongeza wananchi wa Burundi kwa kuadhimisha miaka 59 ya uhuru wa nchi hiyo huku wakiendelea kudumisha amani.

Pia, Mheshimiwa Rais Samia amempongeza Rais wa Burundi Mheshimiwa Evariste Ndayishimiye kwa jitihada zake za kukuza amani, demokrasia na uchumi.

Hayo yamesemwa jana (Alhamisi, Julai Mosi, 2021) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipowasilisha salamu za Rais Samia katika sherehe za maadhimisho hayo jijini Bujumbura.

Burundi ilipata uhuru wake kutoka kwa wakoloni wa Ubelgiji Julai 1, 1962.

“Nipo mbele yako nikimuwakilisha Rais wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mheshimiwa Samia. Rais amenituma nilete salamu zake kwako kwamba anawapongeza sana Wana-Burundi kwa kuendelea kukuunga mkono.”

Waziri Mkuu amesema Mheshimiwa Rais Samia amemuhakikishia Rais wa Burundi kwamba ataendeleza uhusiano wa kindugu na wa kihistoria uliopo kati ya nchi hizo mbili na pia ameahidi kuitembelea Burundi.

Kwa upande wake, Rais wa Burundi Mheshimiwa Ndiyashimiye ametumia fursa hiyo kuwasisitiza Wana-Burundi waendelee kushikama na kushirikiana katika kuboresha maendeleo ya nchi yao. “Burundi itajengwa na Warundi wenyewe.”

Amesema kwa sasa wanajivunia hali ya amani na ulivu uliopo Burundi, hivyo amewataka wananchi wa nchi hiyo waendelee kushikamana na wasikubali kulisaliti Taifa lao.

(Mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU


By Author

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post