Rais Samia kuzindua chanjo ya Corona leo, Watanzania mil 35.6 kuchanjwa
WAKATI Rais Samia Suluhu Hassan leo akitarajiwa kuzindua chanjo dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 kwa kuchanjwa Ikulu, Dar es Salaam, serikali imesema asilimia 60 ya Watanzania watachanjwa kukabili ugonjwa huo.
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alisema jana Dar es Salaam kuwa baada ya uzinduzi serikali itaendelea kupokea chanjo dhidi ya ugonjwa huo ili Watanzania wengi zaidi waipate.
Msigwa alisema shehena ya kwanza ya chanjo yenye dozi 1,058,400 inayotosheleza mahitaji ya chanjo kwa asilimia 20 ya Watanzania, lakini serikali imepanga kuchanja asilimia 60 ya idadi ya watu nchini hivyo itaendelea na utaratibu ili kupata dozi nyingine ili kukamilisha asilimia 40 ya wananchi watakaobaki.
Kwa mujibu wa Mwongozo wa Taifa wa Chanjo ya Corona, Tanzania mwaka huu inakadiriwa kuwa na watu 59,441,988 hivyo asilimia 60 ya idadi hiyo ni watu 35,665,192.
“Hii ni dhamira ya serikali yetu kuhakikisha inaokoa maisha ya watu wake dhidi ya janga la ugonjwa huu ambao umeathiri nchi nyingi duniani kote na zaidi tunamshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa mstari wa mbele katika mapambano haya,” alisema Msigwa alipozungumza katika kipindi cha Morning Trumpet cha Kituo cha Televisheni cha UTV kinachomilikiwa na Kampuni ya Azam Media.
Aidha, aliwataka Watanzania wazingatie ushauri unaotolewa na wataalamu wa afya kuhusu chanjo hiyo na wapuuze taarifa za upotoshaji kwa kuwa serikali imesema chanjo hiyo ni hiyari.
Msigwa alisema chanjo hiyo haina madhara yoyote na wala haitofanywa kwa kificho na ndiyo maana Rais Samia ataonesha mfano kwa kuchanjwa huku Watanzania wakishuhudia.
Aliwataka Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kuzingatia mwongozo uliotolewa na serikali na kwamba kila mtu kwa nafasi yake anapaswa kuwa mbele kwa kujilinda na kulinda wenzake.
Alisema asilimia 40 hadi 60 ya watu waliopata ugonjwa huo nchini wanapumua kwa kutumia usaidizi wa mitungi ya oksijeni hivyo ni vyema kujilinda ili kujiepusha na hatari ya kufikia huko.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima, Tanzania ilijiunga na Mpango wa COVAX Facility kupata chanjo ya ugonjwa wa Covid-19 Juni 15, mwaka huu na baadaye kuiwezesha serikali kupokea shehena ya kwanza ya chanjo yenye dozi 1,058,400 aina ya Jensen.
“Baada ya uzinduzi huo, Wizara ya Afya itaendelea na taratibu zingine za usambazaji wa chanjo hiyo na kutoa utaratibu wa utoaji wa utoaji wa chanjo katika vituo vilivyoandaliwa katika mikoa yetu,” alisema Dk Gwajima.
Dk Gwajima alisema chanjo hiyo ni nyongeza mahususi ya afua zinginezo za chanjo ikiwemo unawaji mikono kwa maji safi tiririka na sabuni, uvaaji wa barakoa katika maeneo hatarishi, ufanyaji wa mazoezi na upataji wa lishe bora na matumizi ya tiba asili zilizosajiliwa na Baraza la Tiba Asili.
Alisema utoaji wa chanjo ni moja ya afua muhimu inayoaminika duniani kote katika kupambana na maradhi hususani ya kuambukiza ikkiwemo ugonjwa wa Covid-19 na hivyo kuwataka Watanzania kuitumia fursa hiyo muhimu.
Awali akitangaza Mwongozo mpya wa 17 wa kujikinga na Covid-19 mwishoni mwa wiki iliyopita, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Profesa, Abel Makubi alisema mwongozo huo unasisitiza masuala mbalimbali ikiwemo kuepuka misongamano katika maeneo yote sambamba na uvaaji wa barakoa, unawaji mikono na maji safi tiririka na mengineyo
from Author
Post a Comment