Serikali Shinyanga yakanusha kulemewa wagonjwa wa Corona |Shamteeblog.



Na Marco Maduhu, SHINYANGA.

SERIKALI mkoani Shinyanga, imekanusha taarifa ambazo imedai ni za uongo zilizosambazwa na Mwenyekiti wa Baraza la vijana la chama cha demokrasia na maendeleo Chadema (BAVICHA) mkoani Iringa, Vitusi Nkuna kupitia mitandao ya kijamii, kuwa Mkoa wa Shinyanga umelemewa na wagonjwa wa Corona, na ina uhaba wa Mitungi ya Oksijeni.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk. Philemoni Sengati, amekanusha taarifa hizo leo wakati akizungumza na watumishi wa Serikali, na alipo watembelea wagonjwa wa Corona ambao wamelazwa katika Hospitali ya Rufani mkoani humo.

Alisema baada ya kuona tarifa hizo mtandaoni ambazo zimezua taharuki, ndipo akaona ni vyema atembelee pia katika Hospitali ya Rufaa mkoani humo, ili kujionea mwenyewe hali halisi, na kukuta hakuna idadi ya wagonjwa wengi kama ilivyo enezwa kwenye mitandao ya kijamii na Mwenyekiti huyo wa BAVICHA.

“Serikali ya Mkoa wa Shinyanga, tumesikitishwa sana na taarifa hizi ambazo zime enezwa kwenye mitandao ya kijamii na Mwenyekiti wa BAVICHA mkoani Iringa Vitus Nkuna, kuwa tumelemewa na wagonjwa wa Corona na hatuna Mitungi ya Oksijeni kitu ambacho ni uongo,”amesema Dk.Sengati.

“Mwenyekiti huyu wa BAVICHA Lazima Serikali tumchukulie hatua kali za kisheria kwa kuzusha uongo na kuleta taharuki kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga, hatukatai wagonjwa ni kweli wapo, lakini siyo wengi kama inavyoenezwa na wanaendelea kupata matibabu,”ameongeza.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa, akiwa katika Standi ya Mabasi ya kwenda wilayani, amewataka wananchi wa Shinyanga kuendelea kuchukua tahadhari ya kujikinga na ugonjwa huo wa Corona, kwa kunawa mikono kwa sabuni na majitiririka, kuvaa barakoa, kupaka vitakasa mikono, pamoja na kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga DK. Yudas Ndugile, aliwataka wananchi pale wanaposikia dalili za ugonjwa huo, wawahi kwenye huduma za afya, huku akitaja vituo ambavyo vimetengwa kwa ajili ya kutoa huduma hiyo, kuwa ni Hospitali ya Rufaa, Kolandoto, kituo cha afya Kambarage.

Aidha Dk. Ndugile alitaja vituo vingine kuwa ni Kituo cha afya Tinde, Bugharama, Nyamilangano, Hospitali ya Iselamagazi wilayani Shinyanga. pamoja na Hospitali ya wilaya ya Kahama, huku akitaja dalili za ugonjwa huo kuwa ni kuchoka, kusikia homa, viungo kuuma, kushindwa kupumua vizuri, na kuharisha.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk, Philemon Sengati, akizungumza mara baada ya kutembelea wagonjwa wa Corona katika Hospitali ya Rufaa mkoani humo , na kukanusha taarifa kuwa wamelemewa na wagonjwa kama ilivyoenezwa kwenye mitandao ya kijamii.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk, Philemon Sengati kushoto, akiwa na Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa mkoani Shinyanga Dk. Luzila John, alipowasilia kuangalia Wagonjwa wa Corona hospitalini hapo.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk, Philemon Sengati, kulia akisalimiana na Wagonjwa wa Corona katika Hospitali ya Rufaa mkoani humo.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk, Philemon Sengati akitoa elimu ya Corona katika Stand ya Mabasi mjini humo.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk, Philemon Sengati akinawa mikono katika Standi ya Mabasi Mjini humo, alipofika kutoa elimu ya Corona.


By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post