TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, TAKUKURU Mkoa wa Manyara, imewataka wananchi wa Mjini Babati, kuchukua tahadhari ya kuepuka kuuziwa maeneo inapopita barabara ya mchepuko ili wasipate hasara kwa kutapeliwa fedha zao.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Manyara, Holle Joseph Makungu ameyasema hayo mjini Babati wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya shughuli mbalimbali walizozifanya tangu Aprili hadi Juni mwaka huu.
Makungu amesema watu wanaotaka kununua maeneo ya kata za Babati, Maisaka au Nangara, wawasiliane na ofisi za ardhi ili kupata uhakika wa kutouziwa eneo linapopita barabara za mchepuko na kupata hasara inayoepukika.
“Uzoefu unaonyesha baadhi ya wananchi wakifahamu maeneo yao yatapitiwa na barabara ya mchepuko wanauzia watu wasio na taarifa na kujipatia fedha zisizo halali,” amesema.
Amesema watu hao hupata fedha kinyume cha sheria ya kuzuia na
kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007 na kuwaacha waliowauzia wakiyaendeleza maeneo hayo.
“Majengo hayo huja kubomolewa wakati wa utekelezajiwa mradi bila fidia kwa kuwa fidia zinakuwa zimekwishisha lipwa na wamiliki wa awali wa maeneo husika,” amesema Makungu.
Ametoa wito kwa wana Manyara kutoa taarifa za rushwa, ubadhirifu na
hujuma katika kutekeleza miradi ya maendeleo kupitia namba yao ya
dharura ya 113.
Amewasihi wana Manyara pindi wanapopata wito nje ya mkoa kwa jina la
TAKUKURU, inabidi wajiridhishe kwenye ofisi za karibu ili wapate
uhakika na uhalali wa wito huo kwani kuna matapeli wanaotumia jina la TAKUKURU.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Manyara, Holle Joseph Makungu, akizungumza na waandishi wa habari Mjini Babati.
By Mpekuzi
Post a Comment