CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimekataa mwaliko wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) uliokitaka kwenda Ikulu jijini Dar es Salaam leo kuhudhuria hafla ya kukabidhi ripoti ya Uchaguzi Mkuu uliopita.
Mkurugenzi wa Idara ya Itikadi, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa CHADEMA, John Mrema, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, alidai wamepokea mwaliko kutoka kwa Mkurugenzi wa NEC kwa ajili ya Mwenyekiti, Katibu Mkuu na aliyekuwa mgombea urais kupitia chama hicho kuhudhuria hafla hiyo.
Hata hivyo, Mrema alisema kuwa kupitia barua ya Katibu Mkuu wa CHADEMA, wamemjulisha Mkurugenzi wa NEC kuwa hawatashiriki hafla hiyo kutokana na sababu tano.
Alitaja sababu hizo kuwa zinajumuisha alichookiita ukiukwaji wa sheria na haki katika uchaguzi mkuu uliopita.
Mrema alitaja sababu ya pili kuwa ni Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, kufunguliwa kesi ya ugaidi, jambo ambalo chama hicho kinaamini ni chuki za kisiasa.
“Tunaelekeza nguvu na muda tulionao kufanya jitihada za kuhakikisha mwenyekiti wetu, viongozi na wanachama wengine waliokamatwa kwa uonevu na wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi wanaachiliwa huru,” alisema.
Mrema aliitaja sababu ya tatu ya kutoshiriki kwao katika hafla hiyo kuwa ni madai ya kutishwa kwa aliyekuwa mgombea wao wa kiti cha urais katika uchaguzi huo, Tundu Lissu, hadi kufikia hatua ya kulazimika kukimbilia nje ya nchi.
Alidai kuwa Lissu akiwa Ubalozi wa Ujerumani, alikamatwa na Jeshi la Polisi, lakini alisaidiwa na uongozi wa ubalozi huo.
“Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Simon Sirro, amesema hadharani kwamba Lissu hatapatiwa ulinzi wowote na polisi licha ya ukweli kwamba aliponea chupuchupu katika jaribio la mauaji la Septemba 7, 2017, jaribio ambalo halijawahi kuchunguzwa na hatua stahiki kuchukuliwa dhidi ya wahusika,” alisema.
Aliitaja sababu ya nne kuwa ni NEC kutojibu barua ya Katibu Mkuu wa CHADEMA ya Novemba 25, mwaka jana yenye kumbukumbu namba C/HQ/ADM/20/TU/05/14 iliyotaka maelezo ya nani alitia saini barua na fomu za waliotangazwa kuwa wabunge wa viti maalum kupitia chama hicho na nakala ya nyaraka husika kwa ajili ya kuchukua hatua kwa kuzingatia Kamati Kuu haijawahi kufanya uteuzi wala kuwasilisha orodha ya majina NEC.
Alitaja sababu ya tano kuwa ni ajenda yao ya sasa na siku zijazo ya kuhakikisha Katiba Mpya inapatikana ili kutengeneza mfumo huru na wa kidemokrasia wa uchaguzi wa nchi.
Alidai kushiriki katika mialiko na shughuli za NEC ambayo CHADEMA wanaamini hauko huru, ni kuipa baraka za kisiasa tume hiyo na kupunguza nguvu na ari ya jitihada za kufanya mabadiliko wanayoamini yanahitajika nchini.
*Imeandaliwa na Mary Geofrey na Beatrice Inyasi (TUDARCo)
from Author
Post a Comment