Rais wa Marekani Joe Biden ametetea uamuzi wake wa kuwaondoa wanajeshi kutoka Afghanistan, akisema uamuzi huo ni wenye tija kwa maslahi ya nchi yake. Ameyasema hayo katika hotuba yake kwa taifa iliyosubiriwa kwa shauku.
Washington Rede Präsident Biden Aghanistan
Hotuba ya Rais Biden, ya kwanza tangu Watalibani walipochukua udhibiti wa mambo nchini Afghanistan ilikuwa ikisubiriwa kwa shauku nchini mwake na miongoni mwa washirika wa Marekani, huku kiongozi huyo akikosolewa kusalia kimya wakati mgogoro wa kibinadamu ukitokota Afghanistan. Biden amekiri kuwa serikali ya Afghanistan ilisambaratika haraka kuliko alivyotarajia, lakini aliilaumu serikali ya mjini Kabul kwa kushindwa kupigana na Wataliban licha ya misaada na mafunzo chungu nzima kutoka Marekani.
Amesema Wanajeshi wa nchi yake hawawezi kuendelea kutoa maisha yao kwa niaba ya Waafghanistan wasio na nia ya kuipigania nchi yao, na kuongeza kuwa yuko tayari kubebeshwa lawama kwa kumaliza uwepo wa miaka 20 wa nchi yake nchini Afghanistan, kuliko kuurefusha uwepo huo na kuurithisha kwa rais atakayefuata.
Afghanistan Kabul Flughafen Evakuierungen Chaos
Rais Biden alikosolewa kusalia kimya wakati hali ya kibinadamu ikizorota Afghanistan
”Nashikilia msimamo wangu bila kutetereka, baada ya miaka 20 nimejifunza ukweli mchungu, kwamba hakuna wakati bora wa kuondoa vikosi vya Marekani, hiyo ndio sababu bado tuko kule, tulijua bayana hatari iliyopo,” amesema Biden.
Kusimamia haki za binadamu na kutetea demokrasia
Biden amesema Marekani itapigia debe diplomasia ya kikanda na kutetea haki za binadamu kwa watu wa Afghanistan, na kuonya kuwa iwapo Wataliban watajaribu kutatiza shughuli ya kuwaondoa Wamarekani katika uwanja wa ndege mjini Kabul, atajibu kwa njia za kijeshi.
Haki za binadamu kwa Waafghanistan zimemulikwa pia na kansela wa Ujerumani Angela Merkel alipozungumza na waandishi wa habari mjini Berlin Jumatatu jioni. Bi Merkel alisema anahofia hatma ya waafghanistan waliopigania uhuru wa maiasha yao.
Deutschland | PK Angela Merkel zu AfghanistanKansela wa Ujerumani Angela Merkel amesikitishwa na hatma ya wanaopigania demokrasia na haki za binadamu nhini Afghanistan
”Huu ni wakati mbaya sana kwa mamilioni ya Waafghanistan waliojitolea kupigania jamii huru, na ambao kwa msaada wa nchi za magharibi,waliweka imani katika demokrasia, elimu na haki za wanawake,” amesikitika Merkel na kuongeza kuwa ”kamwe hatupaswi kuwasahau watu waliopoteza maisha yao kupigania haki hizo, wakiwemo wajerumani 59.”
Ujerumani yasaidia Waafghanistan kufika mahali salama
Hata hivyo, Bi Merkel amesema suala lenye kipaumbele kwa sasa ni kuhakikisha kuwa raia wa Ujerumani wanaondoka nchini Afghanistan na kufika mahali salama. Aliarifu kuwa hadi wakati huo, Waafghanistan wapatao 1900 waliofanya kazi na Ujerumani walikuwa wameondoka Afghanistan na kuwasili Ujerumani au katika nchi nyingine nje ya Afghanistan.
Viongozi wengine wa Ulaya pia wamesema watashinikiza msimamo sawa wa kimataifa kuelekea serikali itakayoundwa na Wataliban nchini Afghanistan. Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson amefanya mazungumzo na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, ambapo wamekubaliana kuzungumza kwa sauti moja juu ya uhusiano na serikali itakayoundwa na Wataliban, na katika kuzuia mzozo wa kibinadamu na mgogoro wa wakimbizi.
from Author
Post a Comment