Dar es Salaam. Hatima ya shauri la kupinga tozo za miamala ya simu lililofunguliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) itajulikana Septemba 8 pale Mahakama Kuu itakapotoa uamuzi wa pingamizi la Serikali.
Kituo hicho kilifungua shauri hilo Julai 27 Mahakama Mahakama Kuu dhidi ya Waziri wa Fedha na Mipango (mdaiwa wa kwanza), Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (mdaiwa wa pili) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (mdaiwa wa tatu).
Katika shauri hilo namba 11 la mwaka huu, LHRC inaomba kibali cha kufungua mapitio ya Mahakama Kuu kuhusu Sheria ya Mfumo wa Malipo ya Taifa Sura 437 na Kanuni zake zilizoweka tozo katika miamala ya simu.
Pamoja na mambo mengine, kituo hicho pia kinasema tozo hizo zimekuwa mzigo kwa wananchi.
Hata hivyo, shauri hilo liko njia panda baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kuweka pingamizi akibainisha sababu tatu za kisheria kuiomba mahakama hiyo kulitupilia mbali.
Katika hoja hizo za kisheria, Serikali imesema maombi ya LHRC hayawezi kutolewa na mahakama hiyo kwa kuwa hakuna uamuzi uliotolewa na wadaiwa ambao taasisi hiyo inaweza kuupinga.
Katika hoja ya pili Serikali inasema shauri hilo ni batili kwa kuwa limefunguliwa bila kufuata mfumo wa kisheria kwani taasisi hiyo imefungua kesi bila kuwapo maazimio ya bodi kuridhia kufunguliwa kwamba ni kinyume wa msimamo wa kisheria.
Sababu ya tatu ya Serikali ni kuwa hakuna kiini au msingi wa madai hivyo hakina haki ya kisheria kufungua shauri hilo.
Pingamizi hili limesikilizwa jana na Jaji John Mgetta huku upande wa wadaiwa ukiwakilishwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Gabriel Malata ambaye alitoa ufafanuzi wa hoja hizo huku LHRC ikiwakilishwana Wakili Mpale Mpoki aliyejibu hoja hizo.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Jaji Mgetta aliahirisha shauri hilo hadi Septemba 8 atakapotoa uamuzi wa pingamizi hilo la Serikali.
Wakati wa usikilizaji wa pingamizi, Wakili Malata katika hoja ya kwanza alifafanua kuwa shauri hilo halina maana bali kufunguliwa kwake ni matumizi mabaya ya mahakama.
from Author
Post a Comment