SERIKALI YAPONGEZWA KWA KUJENGA SHULE YA SEKONDARI YENYE MIUNDOMBINU RAFIKI KWA WATOTO WENYE MAHITAJI MAALUM |Shamteeblog.

 Charles James, Michuzi TV

TUNASHUKURU! Ndiyo kauli ambayo wameitoa kwa Serikali wanafunzi wanaosoma katika Shule ya Sekondari Patandi Maalum ambayo ni Shule  Jumuishi yenye watoto wenye ulemavu na wasio walemavu.

Shukrani hizo zimetolewa na wanafunzi wenye mahitaji maalum wanaosoma kwenye Shule hiyo ambapo wameeleza kuwa Shule hiyo imejengwa katika mazingira bora ambayo ni rafiki kwa wao wenye ulemavu.

Akizungumza na wandishi wa habari katika ziara ya kutembelea Shule hiyo iliyopo Tengeru Mkoani Arusha, mmoja wa wanafunzi wa kidato cha kwanza, Muhidin Igibuga ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kujenga Shule hiyo ambayo ina mazingira wezeshi na rafiki kwao watu wenye ulemavu.

Amesema uwepo wa shule hiyo umesaidia watoto wengi wenye ulemavu ambao walikua wakipata tabu katika shule walizokua wakisoma awali kiasi cha wengi kukata tamaa ya masomo lakini uwepo wa Sekondari ya Patandi Maalum umeamsha ari na kiu ya kusoma ili kutimiza ndoto zao.

" Kiukweli ujenzi wa shule hii umekua na maana kubwa sana kwetu sisi wenye ulemavu, tuna Walimu bora wenye upendo na sisi, kuna mazingira bora ambayo yanatufanya tufurahie kuishi hapa, hakika tuna kila sababu ya kuishukuru Wizara ya Elimu kwa kujenga Shule hii.

Wengi tulishakata tamaa kwa sababu Shule nyingi hazina miundombinu rafiki ya kutuwezesha sisi wenye uhitaji kuishi na kuyafurahia ila hapa tunafurahia na tunasoma bila changamoto yoyote," Amesema Muhidini.

Kwa upande wake Rebecca Whiston ambaye nae ni Mwanafunzi amesema kwa aina ya mazingira yaliyopo kwenye shule hiyo suala la kufaulu kwao halina mjadala huku akiahidi Serikali kusoma kwa bidii ili kuweza kufaulu na kutimiza ndoto zao.

" Kiukweli uwepo wa shule hii ni kama umeamsha ndoto ambazo wengi wetu zilikua zimeshakufa, tunaahidi Serikali kwamba shukrani yetu kwao kwa kutujengea Shule hii ni kufanya vizuri zaidi kwenye masomo yetu na kuwa miongoni mwa Shule zenye ufaulu mzuri nchini," Amesema Rebecca.

Kwa upande wake Mkuu wa Shule hiyo, Mwalimu Janeth Mollel amesema Shule hiyo kwa sasa ina kidato cha kwanza pekee ambapo jumla ya wanafunzi waliopo ni 185 huku wanafunzi 136 wakiwa ni wenye mahitaji maalum ambapo wapo wenye ulemavu wa viungo, macho, kusikia na kuongea pamoja na wenye ualbino.

Amesema ujenzi wa Shule hiyo umezingatia wanafunzi wenye mahitaji maalum ambapo kuna njia zinazowawezesha kutembea kwa baiskeli lakini pia hata mabweni yao ni tofauti kulingana na mahitaji yao.

"Tunaishukuru Serikali kwa Shule hii imesaidia sana kuamsha ndoto za watoto hawa wenye ulemavu, pamoja na ubora wa shule hii pia Serikali kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia imetuletea Viti mwendo vitatu kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu wa viungo pamoja na vitabu vya kujifunzia.

Wito wangu kwa wazazi wenye watoto walemavu kuacha dhana potofu ya kutowapatia elimu watoto wao kwa kisingizio cha ulemavu kwani tayari Serikali imejenga Shule ambayo ina mazingira bora na Rafiki kwao," Amesema Mwalimu Mollel.

Nae Kaimu Afisa Elimu Sekondari Mkoa wa Arusha, Kabesi Kabejo amesema Shule hiyo imetengenezwa kwa kufuata miundombinu inayotakiwa ambayo ni Jumuishi ili kuwawezesha hata wenye ulemavu kuweza kuyatumia bila changamoto yeyote.

" Kwa Mkoa wetu wa Arusha mwanzo hatukua na Shule ya namna hii, ni wazi Serikali inastahili kupongezwa kwa kuwezesha uwepo wa hii Shule ambayo siyo tu ina manufaa kwa Mkoa wa Arusha bali Nchi nzima kwani kwa sasa inapokea idadi kubwa tu ya wanafunzi wanaotoka Mikoa mingine," Amesema Kabesi.

Ujenzi wa Shule hiyo ya Sekondari Patandi Maalum ulianza mwaka 2017 ambapo ina majengo 10 manne yakiwa ni madarasa 12, Ofisi mbalimbali Sita na majengo manne ya mabweni, jengo la utawala, bwalo na jiko ambapo kiasi cha Sh Bilioni 3.6 ndicho kilichotumika kukamilisha ujenzi wa shule hiyo ya mfano.

Wanafunzi wanaosoma katika Shule ya Sekondari Patandi Maalum iliyopo Tengeru mkoani Arusha ambapo ni Shule Jumuishi yenye watoto wenye ulemavu na wasio walemavu.

Muonekano wa ndani wa vyumba vya wanafunzi wanaosoma Shule ya Sekondari Patandi Maalum iliyopo mkoani Arusha. Vyumba hivi vimezingatia mahitaji ya wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Hili ni jengo la utawala la Shule ya Sekondari Patandi Maalum iliyopo Tengeru mkoani Arusha kama linavyoonekana likiwa na njia zinazowawezesha pia wanafunzi wenye ulemavu wa viungo kupita.

Muonekano wa majengo ya Mabweni katika Shule ya Sekondari Patandi Maalum iliyopo Tengeru mkoani Arusha ambayo ni Shule Jumuishi yenye watoto wenye ulemavu na wasio walemavu.





By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post