Na WAMJW- DSM
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima, ameitaka Bodi mpya ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kufanyia kazi changamoto za kiutendaji ambazo Mamlaka inakumbana nazo kwa lengo la kuboresha utendaji wa kazi.
Dkt. Gwajima, ameyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizindua Bodi ya pili ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, tukio limefanyika katika ofisi za Mamlaka hiyo Jijini Dar es Salaam.
” Pamoja na mafanikio makubwa ambayo Bodi iliyopita iliweza kuyapata, bado kuna changamoto ambazo kama Wajumbe wa Bodi wapya mnapaswa kuanza nazo na kuzipa kipaumbele katika utekelezaji wa majukumu yenu, baadhi ya changamoto hizo, ni deni ambalo Mamlaka inadai kutoka kwa taasisi za Serikali ambalo kwa sasa linafikia kiasi cha Shilingi Bilioni 14.4’’ hivyo serikali itaratibu ufuatiliaji Ili kuwe na mpango wa kulipwa fedha hizo zitumike kuendeleza taasisi.
Alisema kuwa, Wizara, Menejimenti na Watumishi wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ina matumaini makubwa kutoka kwenu ya kututoa hapa tulipo na kutupeleka mbele zaidi kiutendaji ili kukidhi kiu ya mafanikio na kusonga mbele zaidi.
Hata hivyo Dkt. Gwajima aliendelea kusisitiza wajumbe watambue wameteuliwa kwa kuzingatia sifa zao, uzalendo na weledi hivyo kutambua kuwa jukumu walilopewa ni kubwa kulingana na hadhi ya taasisi na kuwataka kwenda kufanyia kazi suala la gharama za uchunguzi wa dawa asili.
‘‘Kazi yenu inahitaji uzalendo mkubwa sana maana ina majaribu mengi kulingana na chombo hiki. Mmeaminiwa, mmechunguzwa na mmepitishwa kwenye mifumo na kuonekana mnafaa kuongoza taasisi hii. Mkalifanyie kazi eneo la uchunguzi wa tiba asili. Mna kazi ya kuandaa gharama na tozo za uchunguzi wa dawa za tiba asili ili kuweza kuona namna ya kusaidia eneo hili.”amesema.
Aidha Dkt. Gwajima amesema kuwa, Kwa uwekezaji uliofanywa na Serikali ndani ya taasisi hii kubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki, hivyo ni vyema kujipanga kuona namna gani ntatoa mchango katika mfumo wa Bima ya Afya kwa wote.
Aliendelea kusema kuwa, mnahitajika kushirikiana kwa kwenda kuona taasisi nyingine kama hii katika ukanda wa Afrika Mashariki na kuona namna ya kusaidiana kwa kufanyakazi pamoja na kubadilishana uzoefu ili kuleta tija katika kuwahudumia wananchi.
Mbali na hayo, ameonesha kuwa na imani na Bodi mpya na kusema kuwa itaipeleka mbele taasisi hii kiutendaji na kukidhi kiu na matarajio ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wadau na wananchi wote kwa ujumla kwa kuzingatia Sheria, Taratibu na kanuni.
Mae Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko amesema kuwa, Majukumu ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali yameainishwa kwenye kifungu cha tano cha Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Sheria Na. 8 ya Mwaka 2016.
Amesisitiza kuwa, majukumu haya yanaweza kugawanywa katika maeneo makuu matatu. Jukumu la Kwanza ni kufanya uchunguzi wa kimaabara wa sampuli/vielelezo mbalimbali, Jukumu la Pili ni kusimamia utekelezaji wa Sheria tatu, na Jukumu la Tatu ni Kutoa ushauri wa kitaalamu kwa Serikali, Wadau na Wananchi wa ujumla kuhusiana na masuala mbalimbali ya uchunguzi wa kimaabara.
By Author
Post a Comment