KUSANYIKO LA KULA PAMOJA CHAKULA CHA SIKUKUU YA KRISTMASS LAFANYIKA JIJINI TANGA |Shamteeblog.


Na Mashaka Mhando

IMEELEZWA kuwa watu waliokoka wana akili timamu wala si wendawazimu, kama watu wanavyodhani kwamba watu waliopokea wakovu na kujiunga na makanisa ya Assemblies of God, wamekuwa na uwendawazimu.

Hayo yameelezwa na Mchungaji Manase Maganga wa Kanisa la Mountain of Glory lililopo katika viwanja vya Saba Saba Jijini Tanga, wakati wa kusanyiko la kula pamoja chakula cha Sikukuu ya Christmas.

Mchungaji Manase alikuwa akijibu swali aliloulizwa mitizamo ya baadhi ya watu kwamba watu wanaoabudu makanisa ya kilokole ni watu waliochanganyikiwa katika jamii.

Mchungaji Manase alisema kuwa watu lazima wawe wakweli juu ya mitizamo ya wokovu ambayo ndiyo njia sahihi ya kwenda mbinguni kwa kuwa watu waliokoka humuomba mungu kupindukia.

Alisema watu wanapoamua kuokoka hasa wana-ndoa lazima wakubaliane katika njia sahihi ya kuokoka, lakini anapookoka mmoja kisha mwingine akakataa wanaweza kutokea kutokuelewana na hata kupelekea kuachana.

"Watu lazima wawe wakweli juu ya mitizamo hii, wokovu ndiyo njia sahihi ya kwenda mbinguni, kuokoka ni mipango ya kusogea karibu na Mungu," alisema.

Hata hivyo, mchungaji Manase alisema Kanisa hilo, litaendelea kuyajali makundi ya wajane, watu wanaoishi katika mazingira magumu na makundi mengine kila mwaka bila kujali dini zao.

Alisema makundi hayo yaliyopo katika jamii bado hayajapewa umuhimu lakini ni watu wanaohitaji faraja ikiwemo kumjua mungu kwa viongozi wa dini kukaa nao na kuwa karibu kila inapobidi.

Alisema makundi ya wajane, vilabu vya watu waliokuwa wakitumia madawa ya kulenya (Sober House), wanaoishi katika mazingira magumu, wanahitaji upendo kutoka kwa viongozi wa dini lakini pia kuishi katika maisha ya kuwapenda bila kujali dini zao.

"Huu ni mwaka wa 14 tunajumuika kupata chakula pamoja, tunawapa mchele, mafuta na vitu vingine bila kujali dini zao lengo likiwa kuwaweka pamoja maana sisi binadamu ni wabinafsi sana tumeyasahau makundi haya," alisema Mchungaji Manase.

Amewataka wananchi wa Tanga, wanaofika katika sherehe ya kula pamoja kila mwaka, wakitaka kufanikiwa katika maisha wamtafute mungu ili waweze kupata matumaini katika maisha yao.

"Wito wangu watu wazidi kumpenda mungu, maisha yatakuwa na matumaini, matajiri wawajali watu wasiokuwa na uwezo maana hakuna tajiri mwenye akili ya kupata bali ni kwa uwezo wa mungu," alisema mchungaji Manase.

Jumla ya wajane na watu mbalimbali wapatao 600 kutoka Jiji la Tanga, ikiwemo Maramba wilayani Mkinga, wamepatiwa mchele kila mtu mfuko wa kilo tano pamoja na mafuta ya kupikia, lakini pia walipata nguo na vitenge mbalimbali kwa wababa na wamama.
Mchungaji Manase Maganga akizungumza na waandishi wa Habari
Wazee wakiwa katika kusanyiko hilo la chakula cha pamoja
Wakina mama wajane wakiwa katika kanisa hilo
Vijana wakiwemo Waendesha bodaboda walikuwepo wakisikiliza neno la mungu na kula chakula cha pamoja



By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post