RAIS Samia Suluhu Hassan amesema serikali imejipanga kukamilisha miradi yote ya kimkakati kwa wakati ukiwemo wa Reli ya Kisasa (SGR) na Bwawa la kufua umeme la Mwalimu Julius Nyerere.
Aidha, amesisitiza kwamba hakuna mradi wowote uliosimama wala utakaosimama kwa kukosa fedha kama baadhi ya watu wasioitakia mema nchi wanavyodhani.
Samia aliyasema hayo jana mkoani Dar es Salaam katika hotuba yake baada ya kukamilika utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa SGR kipande cha tatu kutoka Makutupora mkoani Singida hadi mkoani Tabora na kuongeza kuwa kama wapo waliodhani serikali itashindwa ili wapate la kusema, wamekosa la kusema.
Serikali imejipanga kukamilisha kwa wakati miradi ya kimkakati ili kukuza na kufanya kichocheo cha uchumi kati ya Tanzania na majirani zake.
“Niliahidi kuendeleza mema yaliyopita, yaliyopo na kuendeleza mapya. Ujenzi na utekelezaji wa miradi yote inayoendelea tutaendelea kuisimamia na kuhakikisha kuwa inakamilika.
“Sasa kuna wale ambao walipenda sana kuona miradi hii haiendelei na wanathubutu kusema kwamba miradi hii imeshindikana na haiendelezwi, pamesemwa hapa wakandarasi hawadai hata senti moja ila serikali inadai kazi.”
“Vivyo hivyo kwa miradi mikubwa mingine, ujenzi wa bwawa (la kufua umeme la Julius Nyerere) tunakwenda nao vizuri, hatudaiwi ila tunadai kazi na miradi mingine yote iliyoachwa tunakwenda nayo vizuri.
“Mkipitapita huko mtaona kuwa hakuna mradi uliosimama. Mkipita katika barabara za Dar es Salaam kazi inaendelea, daraja la Kigongo-Busisi daraja linaendelea.”
Alisema pia ujenzi wa barabara mikoani kazi inaendelea, hakuna mradi uliosimama, miradi yote inaendelea.
“Kwahiyo kama walidhani kutakuwa kuna miradi itakwama ili wapate la kusema, halipo. Tutaendelea na ujenzi wa miradi, ...” alisema.
Aliwahadharisha viongozi wa Wizara ya Ujenzi, Shirika la Reli Tanzania (TRC) na wakandarasi wanaohusika na miradi mbalimbali nchini, kwamba hatavumilia wala kuruhusu ujenzi wa miradi ya maendeleo usiokidhi viwango na usioendana na thamani ya fedha zilizotolewa kwani miradi hiyo inatarajiwa kudumu kwa zaidi ya miaka 100 ijayo.
Mkataba huo ulitiwa Saini na Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa na Makamu Mwenyekiti wa Kampuni ya Ujenzi ya Yapi Merkez ya Uturuki, Elderm Orioolu.
Alisema ili reli ijengwe kwa viwango vinavyotakiwa, wadau wote wanaohusika katika michakato ya manunuzi ya vifaa mbalimbali wahakikishe kuwa wanafanya manunuzi ya vifaa bora vitakavyoendana na ukubwa wa mradi na ambavyo vitaishi kwa muda mrefu.
Alisema reli ya SGR itakapokamilika itahitaji vifaa kama mabehewa ya abiria, mabehewa ya mizigo na vichwa vya treni ambapo serikali kwa kulitambua hilo na kuepuka makosa yaliyofanywa kipindi cha nyuma imeshaingia mikataba ya ununuzi wa mabehewa ya abiria 89, vichwa vya treni ya umeme 19, seti za umeme wa treni za kisasa 10 zenye mabehewa 80 vikigharimu dola za Marekani milioni 381.4.
Alisema serikali inaendelea kukamilisha ununuzi wa mabehewa ya mizigo 1,430 kwa sababu moja ya malengo ya treni hizo ni kusafirisha mizigo kwenda katika mataifa jirani.
Aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kukamilisha kwa wakati miradi ya kimkakati kwa sababu bila kufanya hivyo fedha zilizotumika katika uwekezaji huo zinazofika Sh trilioni 14 zitapotea bila faida yoyote katika maendeleo ya nchi.
Alisema kwa kuwa malengo ya serikali ni kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara Afrika Mashariki, baada ya mradi huu kukamilika kipaumbele cha serikali kitakuwa ujenzi wa reli katika matawi yanayounganisha Tanzania na nchi jirani za Uganda, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
“Serikali inaendelea na mipango ya kufungua ushoroba wa Kusini kwa njia ya reli ya kisasa kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay na kuunganisha na miradi ya makaa ya mawe huko Mchuchuma hali itakayofungua milango ya fursa kwa mataifa jirani kufanya biashara na Tanzania,” aliongeza Rais Samia.
Mradi wa ujenzi wa SGR kwa kipande cha tatu kutoka Makutupora hadi mkoani Tabora utakuwa na kilometa 368 ukiwa na thamani ya Sh trilioni 4.406. Mradi utakamilika Oktoba 2025 na utachukua miezi 46 kukamilika. Salamu za mkoa Akiwasilisha salamu za Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa, Amos Makalla alisema wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam wanajivunia mkoa wao kuwa lango kuu la biashara kati ya Tanzania na mataifa mengine ya Afrika Mashariki.
Alisema miradi mikubwa kama ya bandari, reli ya kisasa, uwanja wa ndege na miradi mingine ni nyenzo za kuvutia wawekezaji na biashara mbalimbali za ndani na nje ya nchi itakayoleta fedha nyingi kwa taifa.
Naye Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alisema sekta ya uchukuzi ni chachu ya ujenzi wa Tanzania ya Viwanda hivyo wizara yake itaendelea kuwasimamia wakandarasi ili kuhakikisha kuwa miradi inayokabidhiwa serikali inakuwa bora na yenye viwango vinavyotarajiwa.
Aliwashauri wakandarasi kuhakikisha kuwa wanafanya kazi usiku na mchana ili kuwezesha miradi kukamilika kwa wakati na kutoa huduma kwa wananchi na kusaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.
Alisema ujenzi wa miradi ya kimkakati utasaidia bandari za Tanzania hususani Bandari ya Dar es Salaam kuwa na ushindani na kuweza kuvutia wawekezaji na wafanyabiashara wa ndani na nje ya Tanzania
from Author
Post a Comment