Serikali Itaendeleza Uwazi Katika Mipango Ya Kiuchumi Inayohusu Fedha Za Umma |Shamteeblog.
Na Kijakazi Abdalla / Maelezo.
SERIKALI kupitia Ofisi ya Rais Fedha na Mipango itaendeleza uwazi katika mipango yote ya kiuchumi inayohusu fedha za umma ili kuhakikisha kila mwananchi anafahamu hatua zinzoendelea ndani ya serikali.
Hayo ameyasema Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha na Mipango ambae pia Mwenyekiti Jukwaa la Uchumi wa Bajeti, Dk. Juma Malik Akili wakati akifungua jukwaa la uchumi na Bajeti kwa Serikali kuu na Serikali za Mitaa katika Ukumbi wa Shekh Idrissa Abdul Wakil Kikwajuni.
Alisema hatua hiyo itasaidia kwa wananchi kuondoa wasiwasi na Serikali na kuendelea kuiamini katika kupanga mipango yake mbalimbali ya kimaendeleo.
Aidha alisema lengo la jukwaa hilo kushirikisha wadau mbalimbali ambao watachangia kwa kutoa mawazo yao katika maendeleo na kuona hawamuachi mtu nyuma katika jambo hilo.
Katibu huyo alibainisha kuwa jukwaa hilo lipo kisheria ya fedha ya mwaka 2016 kwa mujibu wa kifungu cha 38 ambacho kinawataka kufanya jukwaa hilo huku wakiendelea na mchakato wa kuandaa bajeti ya mwaka ujao.
Alisema matayarisho na utekelezaji wa jukwaa la uchumi unalenga kukidhi matakwa ya sheria na kuendelea na harakati za matayarisho kwa bajeti ya mwaka 2022/2023 pamoja na mapitio ya muda wa kati ‘Middium turn’ ambayo itaendekea hadi mwaka 2025 kwa utaratibu uliozoeleka.
Alisema ni kawada kwa Serikali kushirikisha wadau na wananchi katika majukwaa kama hayo ambayo yanatoa fursa watu kutoa maoni yao katika kuboresha jambo hilo
“Sote ni mashuhuda kuwa viongozi pamoja na shughuli zetu zote zimekuwa ni shirikishi na tumeamua kutekeleza takwa hilo la kisheria la kuwa na bajeti shirikishi kwa kuanza na jukwaa ambalo linalokutanisha watu kutoka sehemu mbalimbali ambao watachangia katika maendeleo na mpango mzima wa bajeti hii ili tusimuache mtu nyuma” alisema.
Akizungumzia changamoto ya Uviko 19 alisema mbali na mikakati hiyo Zanzibar kama zilivyo nchi nyengine duniani zimekuwa na changamoto katika uchumi wake kufuatia athari za maradhi hayo ambayo yamezikuba nchi nyingi hasa zinazotegemea sekta ya huduma hususan utalii hasa Zanzibar.
Alisema ni vyema wanapopanga bajeti hiyo kutengeneza njia ambazo zitasaidia kutekeleza bajeti hiyo huku wakiendelea kukabiliana na changamoto hiyo ambayo inaendelea kuathiri ulimwengu.
Hata hivyo alibainisha kuwa uchumi wa Zanzibar unategemewa kukua kwa takriban asilimia 5.9 pamoja na kuwa na mtikisiko wa maradhi ya Uviko 19.
Kwa upande wake Kamishana wa Bajeti Ofisi ya RaIs Fedha na Mipango, Saumu Khatib Haji, alisema matarajio ni kuona wAnapomaliza mwaka huu ni kuweza kuitekeleza bajeti hiyo vizuri.
Akiwasilisha mada usimamizi wa deni la taifa na uraribu wa kukopa kwa serikali kuu mashirika na serikali za mitaa, Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa deni la Taifa, Ali Tamim alisema kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2018 / 2020 hadi 2021 deni limeongezeka kutoka bilioni 161 hadi kufikia bilioni 222 ambapo ni ongezeko la asilimia 38.
Alisema kwa mwaka huo hadi kufikia Novemba ni bilioni 233 huku deni la ndani likiwa ni shilingi bilioni 202 na deni la nje la Zanzibar ni 28.2 ukilinganisha na mwaka 2020/2021 deni limekuwa kwa bilioni 8.5 sawa na asilimia 4.
Nao washiriki wa jukwaa hilo walisema ni vyema kwa serikali kuweka vipaumbele vyake muhimu ambavyo vitakuwa ni kichocheo kikubwa kwa uchumi wa nchi.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wenye Viwanda na Wakulima, Hamad Hamad, alisema ni vyema kwa serikali kushirikisha sekta binafsi katika kusaidia mikakati yake ya kiuchumi kwani jambo hilo bado halijafikiwa kwa kiwango kikubwa.
Katika mkutano huo mada mbalimbali zilijadiliwa ikiwemo mapitio na mwelekeo wa hali ya uchumi na mpango wa maendeleo 2021/2022/2023, Usimamizi wa deni la taifa na uratibu wa kukopa kwa Serikali kuu, Mashirika na Serikali za mitaa na mapitio na mwelekeo wa hatua za kuimarisha mapato kwa mwaka wa fedha 2021/2022 na 2023 ambapo kauli mbiu ‘Bajeti ya kuhuisha Uchumi Shirikishi kwa Maendeleo ya Pamoja’.
By Author
Post a Comment