SIKU moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutamka kuwa nchi itakopa ili kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati, wachumi, wanasiasa na wataalamu wa fedha wamepongeza hatua hiyo na kusema itasaidia gharama za maisha ya wananchi kutopanda.
Wamesema miradi mikubwa na ya muda mrefu haiwezi kugharamiwa kwa kutumia makusanyo ya ndani kwa sababu itapandisha gharama za maisha kwa wananchi kwani itahusisha kodi kupanda ili kupata fedha za kutosha za kugharamia miradi hiyo.
Imeelezwa kuwa, mikopo yenye masharti nafuu ndio njia pekee ya kuiwezesha nchi yoyote duniani kutekeleza miradi mikubwa na ya kimkakati bila kusababisha ugumu wa maisha kwa wananchi kwa kuongeza gharama za mahitaji yao.
Wachambuzi wa masuala ya fedha, uchumi, diplomasia na siasa wamesema miradi yote ya kimkakati inatekelezwa kwa mipango ya maendeleo ya muda mrefu ambayo inahitaji mikopo ya muda mrefu kuitekeleza.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Florens Luoga (pichani) alisema jana kuwa, nchi yoyote duniani inakopa kwa ajili ya kutekeleza miradi mikubwa na ya muda mrefu ambayo itaendelea kuzalisha na kuleta uhimilivu mzuri wa deni la nchi.
Alisema serikali haikopi kwa ajili ya kula, bali ni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya muda mrefu ambayo itaendelea kuzalisha na kwa sababu inaendelea kuzalisha uhimilivu wa deni unaendelea kuwa mzuri bila kupanda.
“Ukitumia fedha za ndani peke yake utapandisha kodi, utawafanya wananchi wachangie kwa njia nyingine ambazo ni gharama na itachukua muda mrefu. Badala ya kutekeleza mradi kwa miaka mitatu au minne utatekeleza kwa miaka 20 kwa sababu unategemea uchukue pesa za ndani,” alisema Profesa Luoga wakati akihojiwa na Kituo cha Televisheni cha Clouds.
Mchambuzi wa Uchumi na Siasa nchini, Gabriel Mwang’onda alisema katika utekelezaji wa mipango ya
maendeleo ya muda mrefu, kitu pekee kinachoweza kuharakisha maendeleo kwa haraka ni kukopa mikopo ya masharti nafuu.
Alisema siku zote nchi inayokopa kwa ajili ya mambo makubwa ipo katika mstari sahihi kwa sababu hakuna uwezekano wa kutumia mapato ya ndani kugharamia miradi inayohitaji fedha nyingi kwa sababu serikali inatakiwa kulipa mishahara ya wafanyakazi wote na gharama nyingine nyingi.
“Mfano, mradi mmoja tu wa Reli ya Kisasa (SGR) mpaka sasa serikali imewekeza fedha nyingi sana kiasi cha Sh trilioni 14, hizi ni fedha ambazo haziwezi kupatikana kwa kutumia tozo na kodi mbalimbali za ndani, njia pekee ya kuikamilisha hii ni kukopa kwa masharti nafuu,” alisema Mwang’onda.
Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki alisema serikali inavyokopa kutekeleza miradi muhimu ya maendeleo inapaswa kuungwa mkono na sio kubezwa, bali jambo la msingi ni kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ufanisi na kuzingatia thamani ya fedha zinayotumika.
Alisema si kosa serikali kukopa kwa ajili ya barabara kwani hata nchi tajiri zinakopa kuvumbua teknolojia itakayofanya uzalishaji viwandani ufanywe na roboti badala ya binadamu.
“Kama wenzetu wanakopa kwa ajili ya kwenda mwezini kuna ubaya gani sisi kukopa kujenga reli ya Kaliua-Mpanda-Kalema? Kuna ubaya gani kukopa kupeleka maji Tabora, Dodoma, Singida na Rukwa,” alisema Kairuki.
Alisema hakuna nchi duniani inayotekeleza miradi ya maendeleo bila kukopa na kwamba hata nchi tajiri ulimwenguni zinakopa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.
“Marekani peke yake deni lake lilikuwa asilimia
31.8 ya deni la dunia, Japan asilimia 18.8 ya deni la dunia, Uingereza asilimia
3.7, Ufaransa asilimia 3.8 na nchi 54 za Afrika deni lao kwa pamoja ni asilimia mbili tu,” alisema.
Kwa upande wake, Mchambuzi wa Siasa na Uchumi, Majjid Mjengwa alisema katika sekta ya mikopo, kitu cha kwanza ambacho siku zote serikali inakiangalia ni kuwa inataka kukopa kwa ajili ya miradi gani.
Alisema serikali inatekeleza mipango yake ya maendeleo kwa kuangalia malengo ya miradi yake, kama ni miradi ya muda mrefu serikali itakopa kwa sababu inahitaji fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji.
“Hakuna serikali duniani inayoweza kutekeleza miradi yake mikubwa ya maendeleo kwa kutumia fedha za ndani kwa sababu miradi hiyo inachukua muda mrefu kukamilika wakati ikikopa mradi unachukua muda mfupi kukamilika na kuanza kutumika,” alisema Mjengwa na kuongeza:
“Serikali inayotumia mapato ya ndani kutekeleza miradi mikubwa ni kama mfanyakazi anayelipwa mshahara wa Sh milioni moja akitaka kujenga nyumba ya Sh milioni 100 itamchukua miaka zaidi ya 50 hadi 100 kuikamilisha nyumba hiyo kwa sababu mshahara wake una matumizi mengine ya lazima.”
Alisema ikiwa mfanyakazi huyo ataamua kukopa benki atakamilisha nyumba yake kwa muda mfupi na ataanza kuifaidi huku akikatwa kidogokidogo hadi mkopo wake ukamilike katika kipindi cha miaka 15 au 20.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Kijamii (CCK) kutoka Mkoa wa Pwani na aliyekuwa mgombea wa ubunge Jimbo la
Kibaha Mjini, Dk Gabriel Mziwanda alisema kukopa ili kutekeleza miradi ya kimkakati ni muhimu kwa sababu miradi hiyo ni ya manufaa kwa wananchi.
Mziwanda ambaye pia ni Katibu Mwenezi wa chama hicho Mkoa wa Pwani, aliwataka Watanzania kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan katika utekelezaji wa miradi hiyo yenye faida kubwa kwa maisha ya wananchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Chauma Mkoa wa Pwani na aliyekuwa mgombea ubunge Jimbo la Kibaha Mjini, Jumanne Urembo alisema suala la maendeleo halina chama hivyo jitihada za Rais Samia ni za kupongezwa.
“Tunachokitaka ni kuona miradi inafanyika kwani hatuna sababu ya kupinga hiki kinachofanyika kwani tunajenga nyumba moja hatuna haja ya kugombea fito,” alisema.
Hata hivyo kwa mujibu wa Shirika la fedha Duniani (IMF) kupitia mfumo wake wa kuchambua uhimilifu wa madeni (DSA) ikizungumzia Tanzania kwa taarifa ya Septemba mwaka huu, imesema deni la nje la Tanzania ni himilivu.
Taarifa hiyo imesema kwamba uwiano wa deni kwa pato la taifa limebaki katika asilimia 30 likiwa chini kiwango kinachokubalika cha asilimia 55.
Uwiano huo ni mdogo ukilinganisha na nchi nyingine mfano Angola (90%), Misri (86%), Zambia (80%), Burundi (63%),Ghana (60%), Ethiopia (57%), Kenya (55%), Rwanda (50) na Uganda (44%).
Kwa mifano hiyo ya IMF Tanzania ni miongoni mwa nchi chache zenye viwango vidogo vya deni ukilinganisha na Pato la Taifa (GDP).
Aidha takwimu za Mikopo ya Dunia (Global Debt) za mwaka 2020 zinaonesha kwamba nchi tajiri ndizo zinazoongoza kwa kukopa.
Marekani peke yake deni lake lilikuwa asilimia 31.8 ya deni la dunia; Japan asilimia 18.8; Uingereza asilimia 3.7; Ufaransa asilimia 3.8 wakati nchi 54 za Afrika kwa pamoja deni lao ni asilimia 2 tu.
Uchambuzi huo wa DSA pia unaonesha umuhimu wa ukopaji kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambayo inalipa kwa umma huku utekelezaji wake ukiwa ni wa wazi.
from Author
Post a Comment