Wanne wapoteza maisha ajalini Kagera |Shamteeblog.



 
WATU wanne wamepoteza maisha baada ya gari la mizigo aina ya Scania lenye namba za usajili T 654 DRW  walilokuwa wakisafiria kuacha njia na kupinduka katika mteremko wa Kishoju Kata ya Kihanga Wilaya ya Karagwe, Mkoa wa Kagera.

RPC Kagera, Awadhi Haji akitoa taarifa kwa waandishi wa habari hawapo pichani.
Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, Awadhi Haji amesema kuwa gari hilo lenye Trailer yenye namba za usajili T 638 ADD wakati linapata ajali Desemba 23, 2021 saa 03:00 asubuhi lilikuwa limepakia shehena ya magogo likitokea wilayani Karagwe kuelekea mkoani Shinyanga.

Ametaja waliopoteza maisha kuwa ni Said Twalibu (27) mkazi wa Igombero Mkinga mkoani Tanga aliyekuwa dereva wa gari hilo, Mohamed Seif (31) mkazi wa Mkinga pia mkoani Tanga, Emmanuel Salu mfanyabiashara wa Kahama na Yasin Gowa mkazi wa Tarime Mkoa wa Mara.

"Eneo la tukio barabara ina mteremko mkali na kona kali,  uchunguzi wa awali unaonyesha chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva ambaye naye sasa ni marehemu, alishindwa kuchukua tahadhari kwenye mteremko huo, na mvua ilikuwa inanyesha lakini pia kulikuwa na ukungu mwingi" amesema kamanda huyo.

Kwa mujibu wa Kamanda Haji miili ya watu hao imehifadhiwa katika hospitali ya Nyakahanga iliyoko wilayani Karagwe kwa uchunguzi zaidi. 


 
Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi limewaonya madereva kuacha uzembe wawapo barabarani hasa wakati mvua zinaponyesha, na kuwataka kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepusha kutokea ajali ambazo husababisha vifo, ulemavu na uharibifu wa mali.


from Author

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post