Ikiwa Nchi ya Tanzania bado ipo katika gumzo la kujiuzulu kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mgongano wa mawazo umeendelea kutokea kwa wananchi wengi mitaani pamoja na mitandaoni huku kila mmoja akizungumza ya kwake.
Dar 24 imekwenda mitaani na kuzungumza na wananchi ili kupata sauti zao na fikra juu ya kinachoendelea kuhusiana na kujiuzulu kwa Spika wa Bunge.
“Kwa sababu yeye amekaa akaona makosa aliyoyafanya hayawezi kurekebishika, pamoja yeye aliomba radhi ila kaona Radhi yake haijakubalika. Ni sawasawa na tusi kubwa kwa sababu radhi alioyoiomba haiwezi kufuta kile alichokifanya, kwa hiyo bora ajiuzulu,” alisema mmoja wa wananchi.
Mwananchi huyo aliongeza kuwa “kwa viongozi wakubwa wanaochipukia wajifunze kuwa katika uongozi mkubwa kama huo hutakiwi kukurupuka kufanya jambo. Inabidi ufanye utafiti wa hali ya juu sana, ukikurupuka kusamehewa inakua shida sana.” Aliongeza.
Katika kuendelea kutafuta maoni ya wananchi, Dar24 imekutana na mwananchi mwingine aliesema ameshtushwa na swala hilo ingawa baada ya kufuatilia maongezi ya Ndugai yaliyohusu Mikopo na madeni ya Taifa alingundua kuwa watu wengi walishtushwa na wengine walighadhibishwa na kauli yake hivyo ni sawa bora apumzike.
Mwananchi huyo aliongeza kuwa “ni kama wengine tunamuona kawa Chambo kwa sababu ni kama kulikua na watu nyuma yake wanaomwambia ajaribu kuzungumza ili waone nini kitatokea. Yani apumzike tu” Aliongeza.
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Chongolo ameutangazia umma kupokea barua ya kujiuzulu kwa Ndugai kama Spika na kwa sasa hatua zinazofuata ni kuwasiliswa taarifa kwa katibu wa Bunge ili uchaguzi wa spika mpya ufanyike.
Katika hatua nyingine mwananchi mmoja alisema yeye anaona ni maswala ya kisiasa na ukuaji wa kisiasa na haoni kama kuna tatizo kwa sababu Ndugai amekua akifanya kazi na Viongozi hao wa juu kwa muda mrefu na leo kaamua kujiuzulu baada ya shinikizo kubwa kutoka kwa viongozi wenzake na wanasiasa wenzake.
Job Yustino Ndugai aliehudumu kama Spika wa Bunge kwa miaka 7, anaweka rekodi ya kuwa Spika wa kwanza wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufanya uamuzi wa kujiuzulu ambapo kwa maswala ya Kiserikali hasa muhimili wa bunge, aliwahi kujiuzulu kiongozi wa Serikali Bungeni, Edward Ngoyai Lowasa.
from Author
Post a Comment