BEI YA SUKARI ITAENDELEA KUWA SHILINGI 2000/= KWA KILO- WAZIRI WA BIASHARA NA MAENDELEO YA VIWANDA |Shamteeblog.
Na Issa Mzee Maelezo
Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Omar Said Shaaban, amesema bei ya sukari nchini itaendelea kuwa shilingi 2000 kwa kilo kama ilivyotangazwa mwezi April mwaka jana licha bidhaa hiyo kupanda bei katika soko la Dunia pamoja na kuongezeka kwa gharama kubwa za usafirishaji wa mizigo kutoka nje ya nchi.
Akizungumza na waandishi wahabari ofisini kwake Malindi Mjini Zanzibar, alisema lengo la uamuzi huo ni kuwawezesha wananchi hasa wale wa kipato cha chini kuhimili wimbi la kupanda kwa bei za bidhaa mbalimbali nchini.
Alisema Serikali imepokea maombi ya wafanya biashara wanaoingiza sukari nchini, ya kuiomba serikali kufanya mapitio ya tangazo lake la bei elekezi kwa bidhaa hiyo kutoka 2000 kwa kilo hadi 2300 kwa kilo kutokana na kupanda kwa gharama za usafirishaji wa bidhaa hiyo.
“Serikali baada ya kutafakari maombi hayo imeona ni vyema bei elekezi iendelee kubaki kama awali lakini kwa kuwa hoja iliyotolewa na wafanya biashara ya kutaka kuongeza bei ni ya msingi serikali imeamua kupunguza ushuru wa uingizaji wa sukari kwa asilimia 50 ili kupunguza gharama za uingizaji wa bidhaa hiyo kutoka nje” alisema Waziri.
Alifahamisha kuwa, tafsiri ya uamuzi huo ni kwamba serikali imeamuwa kujinyima mapato yanayotokana na ushuru wa kuagiza bidhaa hiyo ili wananchi wanunuwe sukari kwa bei nafuu.
“Kamwe serikali haitakubali kuona wananchi hawanufaiki na punguzo hilo la ushuru na badala yake wafanyabiashara wanafaidika zaidi” alisisitiza Waziri.
Aidha alisisitiza kuwa serikali haitamvumilia mfanya biashara yoyote atakeuza sukari kwa bei zaidi ya 2000 kwa kilo, na kuahidi kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuwafatilia wafanya biashara Unguja na Pemba ili kuhakikisha bei ya sukari inabaki kama ilivyo..
Sambamba na hayo amesema Serikali itaendelea kufuatilia mwenendo wa bei ya sukari duniani kwa lengo la kusimamia bei elekezi ambayo imekua ikitolewa mara kwa mara kwa mujibu wa sheria.
Katika hatua nyengine Waiziri Shaaban ametoa onyo kwa wafanya biashara ambao wamepewa vibali vya kuingiza sukari lakini hawajawahi kuingiza hata mara moja, kitendo ambacho ni kinyume na matarajio ya kutoa vibali hivyo, na kusema kuwa endapo kampuni hizo ndani ya miezi mitatu zitashindwa kuingiza sukari au kufanya utaratibu wowote wa kuagiza sukari vibali hivyo vitafutwa.
Aidha alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Zanzibar Dkt.Hussein Ali Mwinyi kwa kusamehe sehemu kubwa ya kodi itokanayo na bidhaa ya sukari kwa maslahi ya wananchi wa Zanzibar.
By Mpekuzi
Post a Comment